1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wa-Kyrgyzi na Wa-Uzbeki walaumiana kwa mashambulio

16 Juni 2010

Kura ya maoni inayotarajiwa kupigwa wiki ijayo inakisiwa kuzua hofu zaidi.

https://p.dw.com/p/Ns1Z
Mkaazi wa mji wa Osh, Kyrgyzstan hajui wajukuu wake walipo baada ya ghasia za kikabila.Picha: AP

Kyrgyzstan ambayo ina Waislamu wengi imekuwa katika hali ngumu tangu mapinduzi ya mwezi Aprili yalipompindua rais wa nchi hiyo iliyogawanyika katikati mwa bara Asia na kuileta serikali ya muda madarakani.

Machafuko kati ya makabila makuu ya Wa-Uzbeki na Wa-Kyrgyzi yalianza kuchacha kusini mwa Kyrgyzstan Juni 10 na yakakithiri na kuwa mabaya zaidi kwa kipindi cha miaka 20 katika nchi hiyo iliyokuwa katika muungano wa zamani wa Sovieti.

Kiasi ya watu 189 wameuawa hasa katika mji wa Osh, mji mdogo wenye nyumba za udongo ulioko karibu na mpaka wa Uzbekistan. Marekani na Urusi zimefuatilia matukio hayo zikiwa na hofu kwa sababu zina kambi za kijeshi nchini humo.

Machafuko hayo yametulia, lakini kura ya maoni inayotarajiwa kupigwa wiki ijayo inaweza kuzua hali ya wasiwasi.

Mkaazi wa mji wa Osh alisema milio ya risasi ilitanda usiku kucha na mbele ya nyumba kadhaa kuna maandishi yaliyoandikwa kwa rangi nyekundu ’maafa kwa Wa-Uzbeki’. Mji wa Osh ambao kwa sasa una laini za magofu ya magari na duka zilizochomwa moto, hauna raia na wanajeshi wanapiga doria wakiwa ndani ya vifaru.

Unruhen in Kirgistan
'Maafa kwa Wa-Uzbeki' , maandishi yaliyoandikwa mbele ya nyumba kadhaa mjini Osh.Picha: AP

Urusi na nchi za magharibi inahofia kwamba machafuko hayo yanaweza kusababisha pengo na nchi hiyo ikawa ngome ya wapiganaji wenye msimamo mkali wa Kiislamu na magenge ya wahalifu. Wachunguzi wanasema jaribio lolote la kuifanya nchi hiyo iwe chini ya uongozi wa Kiislamu linaweza kushindwa.

Katika mji mkuu, Bishkek bendera zilipepea nusu mlingoti kwa heshima ya waliouawa katika mapigano ya kikabila na Wa-Uzbeki na Wa-Kyrgyzi wamelaumiana kwa mashambulio hayo.

Serikali ya sasa imemtuhumu rais wa zamani aliyeondolewa madarakani, Kurmanbek Bakiyev, ambaye ni MuKyrgyzi kwa kuchochea ghasia hizo. Hata hivyo Bakiyev ambaye yuko uhamishoni Belarus amekana kwamba amehusika. Serikali hiyo inasema kwamba inajitahidi kuendesha kura ya maoni tarehe 27 mwezi huu kuhusu mabadiliko ya kikatiba yatakayoifanya Kyrgyzstan iwe na demokrasia dhabiti lakini ikiwa machafuko yatatokota tena, itakuwa vigumu kuipanga kura hiyo.

Kirgisistan Kirgisien Khirgistan Kyrgyzstan Flash-Galerie
Mamia ya Wa-Uzbeki wamekwama katika mpaka wa Uzbekistan.Picha: AP

Machafuko katika eneo la kusini yalisababisha wakimbizi laki moja kukimbilia Uzbekistan na wengi wao wanakosa maji na chakula. Katika mpaka wa Uzbekistan mamia ya wakimbizi wamekwama huku Uzbekistan ikijitahidi kuhimili kiwango kikubwa cha wakimbizi na iliufunga mpaka wake kwa muda hapo siku ya Jumatatu. Mpiga picha wa shirika la habari la Reuters aliyeko upande wa Uzbekistan amesema watu wengine wanavukishwa kupitia daraja hafifu.

Naibu waziri wa Marekani, Robert Blake, anatarajiwa kusafiri kwenda nchini Kyrgyzstan siku ya Ijumaa kushauriana na maafisa nchini humo.

Mwandishi, Peter Moss /Reuters

Mhariri, Josephat Charo