1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 29 wafa katika mkanyagano, Liberia

Admin.WagnerD20 Januari 2022

Watu wapatao 29 wamekufa baada kukanyagana kwenye kusanyiko la maombi katika mji mkuu wa Liberia, Monrovia hii leo. Polisi wamesema kuwa idadi ya watu waliofariki huenda ikaongezeka. 

https://p.dw.com/p/45qEa
Massenpanik in Liberia
Picha: Augustine D Wallace/AP Photo/picture alliance/dpa

Kwa mujibu wa vyombo vya habari katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi maafa hayo yalitokea usiku wa kuamkia leo. Msemaji wa polisi Moses Carter ameliambia shirika la habari la AFP kwamba idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka kwa sababu baadhi ya watu waliojeruhiwa wamo katika hali mahtuti. Amesema watoto ni miongoni mwa waliofariki.

Dixon Seebo, mwakilishi wa kitongoji cha walala hoi cha New Kru ambako mtafaruku huo ulitokea, amesema watoto 11 wamepoteza maisha. Vyombo vya habari vimesema kuwa bado kuna utatanishi kuhusiana na maelezo juu ya tukio hilo lililohudhuriwa na mkusanyiko mkubwa wa watu kwenye maombi ya Kikristo yaliyofanyika kwenye uwanja wa mpira wa miguu katika kitongoji hicho cha New Kru.

Mchungaji Abraham Kromah, muhubiri maarufu nchini Liberia, aliandaa maombi ya siku mbili ambayo yaliuvutia umati mkubwa wa watu, kulingana na picha zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii.

Flash-Galerie Fußball Senioren George Weah
Ofisi ya rais George Weah imeagiza kufanyika uchunguzi wa tukio hilo.Picha: AP

Ofisi ya Rais wa nchi hiyo George Weah, imetangaza muda wa siku tatu za maombolezo ya kitaifa na imeamuru uchunguzi ufanyike. Baadhi ya vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti kwamba majambazi waliokuwa na visu na mapanga waliwavamia waumini hao na huenda ikawa ndio sababu ya kutokea mkanyagano.

Bi Elisabeth Wesseh aliyehudhuria maombi hayo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kundi la wahalifu la vijana wenye umri mgogo linalojiita "Zogo Boys", waliwatishia waumini kwa visu, wakitaka wapewe pesa na simu. Ameeleza kuwa watu waliingiwa na hofu na ndipo walipoanza kukimbilia mlangoni, ambapo haikuwa rahisi kwa kila mtu kuweza kupita haraka.

Liberia, jamhuri kongwe zaidi barani Afrika, ni nchi masikini ambayo inaendelea kufanya juhudi za kujijenga upya baada ya kukumbwa na mfululizo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1989 hadi 2003. Takriban watu laki 2 na nusu waliuawa. Pia nchi hiyo ilikabiliwa na janga la Ebola katika ukanda wa Afrika Magharibi mnamo mwaka 2014 hadi 2016.

Kulingana na Benki ya Dunia, asilimia 44 ya wakazi wa Liberia wana kipato cha chini ya dola 1.9 kwa siku. Ajali na majanga mengine yamekuwa yakitokea mara kadhaa. Tukio jengine kama hilo la mkanyagano wakati wa maombi lilitokea katikati mwa mwezi Novemba mwaka jana ambapo watoto wawili wachanga walikufa.