1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kadhaa watiwa mbaroni Brussels

8 Aprili 2016

Watu kadhaa wamekamatwa Ijumaa(08:04:2014) kwa kuunganishwa na shambulio la mauwaji ya uwanja wa ndege wa Brussels na njia ya reli ya chini ardhi nchini Ubelgiji.

https://p.dw.com/p/1ISDe
Picha zilizotolewa katika video iliyomnasa Mtuhumiwa wa Ugaidi Mohamed Abrini

Watuhumiwa wanahusishwa na mashambulizi ya Machi 22, ambayo yalisababisha vifo vya watu 32.Taarifa ya mwendesha mashitaka nchini Ubelgiji imethibitisha kufanyika kwa msako huo uliopelekea kutiwa mbaroni watu kadhaa. Hata hivyo taarifa hiyo haikutoa maelezo zaidi kuhusu msako huo.

Kutiwa mbaroni kwa mtuhumiwa sugu

Mapema Ijumaa televisheni ya serikali VRT ilisema watu wawili walitiwa mbaroni, ambapo mmoja miongoni mwa hao alitajwa kuwa Mohamed Abrini,ambae alikuwa akitafutwa kutokana na mashambulizi ya Kundi la Dola la Kiislamu ya mjini Paris, mwezi Novemba. Lakini taarifa hiyo ya televisheni haikutaja chanzo cha habari, kilichotaja jina la mtuhumiwa huyo.

Mashambulizi ya Novemba 13 ya mjini Paris yalisababisha vifo vya watu 130. Abrini mwenye umri wa miaka 31 inaelezwa kuwa ni muhalifu mdogo mdogo wa nchini Ubelgiji na inaaminika alisafiri kwenda Syria kwa ajili ya mapigano katika msimu wa kiangazi wa mwaka uliopita, ambako mdogo wake aliwawa mwaka 2014 katika brigedia ya kikatili ya wapiganaji wanaozungumza Kifaransa.

Inaelezwa mtuhumiwa huyo alikuwa mafichoni tangu yatokee mashambulizi ya Novemba 13 na hajaweza kuonekana hadharani baada ya mkanda wa video kumnasa katika kundi la wapiganaji lililokuwa likielekea mjini Paris. Ana mahusiano na Abdelhamid Abbaud, kiongozi wa mashambulizi ya Paris ambae alikufa katika makabiliano na polisi.

Televisheni VRT iliongeza kwamba Abrini inahisiwa alihusika vilevile na mashambulizi ya mwezi uliopita la mjini Brussels.

Mwandishi: Sudi Mnette RTR/AFP/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga