1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni saba wahitaji msaada wa kibinaadamu Syria

19 Aprili 2013

Wakati mzozo wa Syria ukiendelea kugharimu maisha ya watu Umoja wa Mataifa unasema kuwa takriban watu milioni saba wanahitaji msaada wa kibinaadamu na kuilaumu serikali ya nchi hiyo kwa kukwamisha usambazaji wa misaada.

https://p.dw.com/p/18Jfz
Wakimbizi wa Syria.
Wakimbizi wa Syria.Picha: Reuters

Valerie Amos, mkuu wa Masuala ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kwamba mahitaji ya msaada wa kibinaadamu yanazidi kuongezeka kwa haraka na hali ni mbaya zaidi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi katika nchi hiyo iliokumbwa na vita.

Ameongeza kusema taarifa zinaonyesha kwamba watu milioni sita na laki nane wanahitaji msaada katika nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 20.8 wakiwemo milioni 4.25 waliopoteza makaazi yao ndani ya nchi ikiwa ni ziada ya wengine milioni moja nukta tatu waliotafuta ukimbizi katika nchi za jirani.

Wito wa Baraza la Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kujulishwa hayo limeitaka serikali ya Syria na upinzani kutowa ushirikiano wao kwa mashirka ya Umoja wa Mataifa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika vikao vyake vya kuijadili Syria.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika vikao vyake vya kuijadili Syria.Picha: dapd

Baraza hilo limewahimiza wahusika wote kuhakikisha misaada inayatolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa inawafikia wale wanaoihitaji katika maeneo yote ya Syria kwa salama na bila ya vikwazo. Limelaani vikwazo vinavyokwamisha utowaji wa misaada ya kibinaadamu na kusisitiza haja ya dharura kuondowa vikwazo vyote vya aina hiyo vikiwemo vile vya urasimu.Taarifa hiyo pia imetaka shehena zote za misaada zihuruhusiwe kuvuka mipaka inapobidi.

Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limezitaka pande zote mbili serikali na waasi kuwalinda raia na kuheshimu sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu na sheria ya ubinaadamu na kukumbusha wajibu wa msingi wa serikali ya Syria katika kutimiza hilo.

Urasimu ni kikwazo

Kwa mujibu wa Amos, msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinaadamu na mratibu wa misaada ya dharura, idadi ya mashirika yasio ya kiserikali yalioidhinishwa nchini Syria hivi karibuni imepunguzwa kutoka 110 na kubakishwa 29 na Umoja wa Mataifa umejulishwa kwamba kila lori litahitaji kibali kilichosainiwa na mawaziri wawili kuweza kuvuka vituo vya ukaguzi vya serikali.

Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa Valerie Amos.
Valerie Amos Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa.Picha: Reuters

Inaelezwa kwamba msafara wa malori kutoka Damascus kwenda Allepo hupitia vituo vya ukaguzi 50 nusu yao vikiwa chini ya udhibiti wa serikali.

Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kiunganisho cha video amesema idadi ya wakimbizi inaweza kupindukia milioni 3.5 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Syria kusambaratika

Wakati huo huo Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry hapo jana ameonya kwamba mzozo unaoendelea kupamba moto nchini Syria unaweza kuisambaratisha nchi hiyo kugawika kuwa katika maeneo yenye tawala tafauti zinazohasimiana.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry.Picha: AFP/Getty Images

Kerry ametowa kauli hiyo wakati akijiandaa kwa mkutano wa mwishoni wa juma kuhusu mzozo wa Syria uliopangwa kufanyika Uturuki.

Kerry amesema madhumuni ya mkutano wa Marafiki wa Syria mjini Istanbul hapo Jumamosi ni kuhakikisha kunakuwepo makubaliano juu ya suala la Syria inavyopaswa kuwa baada ya kumalizika kwa utawala wa Assad. Amesisitiza haja ya kuhakikisha wahusika wote ya nchi za Qatar,Saudi Arabia,Falme za Umoja wa Kiarabu,Uturuki na Ulaya kuwa na malengo ya aina moja.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef