1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi zaidi yatikisa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul

Amina Mjahid
16 Agosti 2018

Maafisa wa Afghanistan wamesema watu waliojihami kwa bunduki wameshambulia kituo cha mafunzo cha kijasusi Kabul, siku moja baada ya mshambuliaji wa kujitolea muhanga kujiripua na kusababisha vifo vya wanajeshi kadhaa

https://p.dw.com/p/33Fjt
Afghanistan Angriff in Jalalabad
Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/M. A. Danishyar

Mapigano ya leo yalitokea karibu na kituo cha  mafunzo kinachoendeshwa na kitengo cha usalama wa kitaifa ambayo pia ni taasisi ya Ujasusi ya Afghanistan. Mpaka sasa hakuna kundi lolote lililokiri kuhusika na shambulizi hilo, lililotokea saa kadhaa baada ya mripuaji wa kujitolea muhanga kujiripua ndani ya shule moja Magharibi mwa Kabul na kusababisha vifo vya watu 37.

Wakati hayo yakijiri  vikosi vya Afghanistan vinasemekana kufanikiwa kuwasogeza wanamgambo wa Taliban mbali na maeneo yao ya kimkakati. Baadhi ya maeneo mjini Kabul yameanza kupokea misaada ya kiutu huku huduma ya simu ikirejea pole pole baada ya mawasiliano kukatizwa na majengo ya serikali kuharibiwa wakati wa mapigano.

Vurugu zinazoshuhudiwa nchini Afghanistan zimetokea  wiki moja baada ya kushuhudia kisichotarajiwa kati ya wanamgambo wa Taliban na vikosi vya serikali,  ambacho ni makubaliano  ya kusimamisha mapigano mwezi Juni mwaka huu hatua iliowafanya raia kupumua . Lakini makubaliano hayo hayakudumu kwa muda mrefu.

Vikosi vya serikali vya Afghanistan
Picha: Reuters/M. Ismail

Majengo ya serikali yalengwa zaidi katika mashambulizi ya Kabul

Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni  imeonyesha kwamba mashambulizi ya wanamgambo pamoja na mashambulizi kutoka kwa watu wanaojitokea muhanga ndiyo chanzo cha vifo vingi katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2018.

Mapigano yameongezeka katika miezi ya hivi Karibuni  baada ya vikosi vya Marekani na vile vya serikali kuimarisha mashambulizi ya angani na ya ardhini dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislamu IS huku wanamgambo wa Taliban nao wakiimarisha vita vyao pia dhidi ya kundi hilo.

Lakini kundi hilo la Taliban halijakiri kuhusika na mashambulizi yoyote ya karibuni mjini Kabul.  Kwa upande wake Kundi la IS limefanya mashambulizi kadhaa Mashariki mwa mji wa Jalalabad pamoja na mji wa Kabul katika miezi ya hivi karibuni likizilenga  wizara za serikali.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman