1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi wauawa Guinea

Admin.WagnerD18 Novemba 2010

Jeshi la Guinea latangaza hali ya hatari baada ya watu wapatao kumi kuuwawa na wengine 200 kujeruhiwa katika vurugu za siku tatu baada ya matokeo ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia kumpa ushindi Alpha Conde

https://p.dw.com/p/QCQ8
Familia ya kabila la Malinke ikikimbia makaazi yake baada ya nyumba yao kuchomwa moto na watu wasioujulikana
Familia ya kabila la Malinke ikikimbia makaazi yake baada ya nyumba yao kuchomwa moto na watu wasioujulikanaPicha: AP

Hali hiyo ya hatari inalipa jeshi la polisi nchini humo nguvu zaidi ya kuimarisha sheria na utulivu, ambapo kwa mujibu wa mkuu wa jeshi, Nouhou Thiam, hali hiyo itasalia hadi pale mizozo ya kisheria kuhusu uchaguzi huo itakaposuluhishwa.

Matokeo ya awali ya uchaguzi huo uliofanyika tarehe 7 Novemba 2010, yaliashiria ushindi wa kiongozi wa upinzani Alpha Conde, lakini uamuzi huo unatarjiwa kupingwa mahakamani na mpinzani wake ambaye pia alikuwa waziri mkuu Cellou Dalein Diallo anayedai kumefanyika udanganyifu.Hali hiyo ya hatari itasalia hadi mahakama kuu itakapo toa uamuzi wa mwisho.

Mshindi wa kiti cha urais wa Guinea, Alpha Conde
Mshindi wa kiti cha urais wa Guinea, Alpha CondePicha: AP

Uchaguzi huo ni wa kwanza wa kidemokrasia katika nchi hiyo iliyo magharibi mwa Afrika tangu ijinyakulie uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo mwaka 1958,na unatarajiwa kumaliza utawala wa kijeshi wa miaka miwili sasa, tangu kufariki kwa rais Lansana Conte.

Wakati huo huo Marekani hapo jana imeshutumu vikali vurugu hizo za baada ya uchaguzi nchini Guinea ikisema kwamba uhalifu hauna nafasi katika nchi hiyo inayoazimia kuwa ya kidemokrasia.

Msemaji katika wizara ya mambo ya nje nchini humo, Philip Crowley, amesema Marekani inashutumu mapigano hayo makali kati ya wafuasi wapinzani wakisiasa kufuatia kutolewa kwa matokeo ya kwanza ya uchaguzi huo. Hivyo basi Marekani imetoa wito kwa viongozi wa kisiasa nchini humo kuwaomba wafuasi wao kuacha vurugu wakati huu wa hali hiyo ya hatari.

Crowley ameendelea kusema kwamba wale wanaopinga matokeo ya uchaguzi wanapaswa kutumia njia za kisheria kumaliza mzozo huo.

Akizungumza hapo awali, Alpha Conde alisisitiza umuhimu wa kuweka tofauti za kisiasa kando kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Mkuu wa jeshi Nouhou Thiam ameeleza kwamba jeshi lilitumwa kuwasaidia maafisa wa polisi kuimarisha usalama barabarani. Kufikia jana jioni, kulikuwa na utulivu katika maeneo mengi mjini Conakry lakini palikuwa na taarifa za ufyatulianaji risasi wa maafisa wa Usalama katika eneo la Ratoma ambalo lina wafuasi wengi wa Cellou Diallo. Kiongozi huyo anasema kwamba wafuasi wake wamelengwa kukandamizwa na kwamba wengi wameuwawa.

Nchi ya Guinea ina historia ya kufanyika maandamano na ukandamizaji unaosababisha vifo vya watu, na vikosi vya usalama vinaangaliwa kwa makini baada ya tukio la kuuwawa kwa watu 150 katika msako uliofanyika mnamo mwezi Machi mwaka uliopita, dhidi ya watu wanaounga mkono demokrasia.

Wito umetolewa kwa vikosi hivyo vya usalama kujizuia kutumia silaha.

Mwandishi: Maryam Abdalla/AFPE/RTRE

Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhan