1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi ya 10 wauwawa katika miripuko miwili Afghanistan

Amina Mjahid
21 Aprili 2022

Kundi la kigaidi la dola la kiislamu limekiri kuhusika na moja ya shambulio baya lililotokea ndani ya msikiti wa waumini wa kishia Kaskazini mwa mji wa Balkh Afghanistan, shambulio lililosababisha vifo vya watu 12.

https://p.dw.com/p/4AFDp
Afghanistan Masar-e-Scharif Moschee
Picha: Valeriy Shustov/Sputnik/dpa/picture alliance

Katika mtandao wao wa habari unaojulikana kama Nashir, kundi hilo lilisema wanajeshi wake waliweka kifurushi kilichojaa vilipuzi ndani ya msikiti mkubwa kwa waumini wa kishia na baadae kukiripua wakati msikiti huo ulipojaa watu. Kundi hilo la dola la kiislamu ambalo haliwatambui waumini wa kishia kama waislamu wa kweli limedai katika taarifa yake kwamba limewauwa zaidi ya washia 100.

Hata hivyo maafisa katika eneo hilo wamesema waliouwawa ni waumini 12, huku wengine 58 wakijeruhiwa na wengine 32 wakiwa katika hali  mbaya, kwenye shambulio hilo lililolenga msikiti wa Say Dokan ambao ni mkongwe na mkubwa katika mji wa Mazar e Sharif.

Picha na vidio zinazoonyesha watu waliojeruhiwa vibaya wakibebwa na kuwekwa kwenye magari ya wagonjwa kwa nia ya kukimbizwa hospitalini, zimesambaa katika mitandao ya kijamii.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa watafuta dola bilioni 4.44 kuisaidia Afghanistan

Ahmad Zia Zindani, ni msemaji wa wizara ya afya mjini Balkh na amesema damu na hofu imejaa kila mahala katika eneo hilo. Zindani ameongeza kuwa jamaa za walioathiriwa wanaendelea kumiminika katika hospitali hiyo ili kuwatafuta wapendwa wao na wengine wakifika huko kutoa damu ili kuwasaidia wanaohitaji.

Bennett asema waliohusika lazima wawajibishwe

Afghanistan - Explosion in Kabul
Muathiriwa wa mripuko wa shule moja mjini Kabul akiwekwa katika gari la kubebea wagonjwa Picha: Wakil Kohsar/AFP

Richard Bennett, Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayesimamia masuala ya haki za binaadamu kwa Afghanistan, amelaani miripuko ya leo. Katika ukurasa wake wa twitter Bennett amesema Afghanistan inaendelea kushuhudia mashambulizi mabaya hasa ile inayolenga shule na misikiti iliyojaa watu. Ametaka uchunguzi wa haraka kufanyika, waliohusika kuwajibishwa na kusitisha uvunjifu wa haki za binaadamu.

Huku hayo yakiarifiwa katika mji mwengine wa Kunduz, watu wengine wanne waliuwawa na wengine 18 kujeruhiwa baada ya bomu moja lililoegeshwa kando na baiskeli kuripuka karibu na mekaniki wanaolifanyia kazi kundi la Taliban. Siku ya Jumanne miripuko miwili nje ya shule moja iliyoko katika maeneo yanayokaliwa na washia mjini Kabul yalisababisha vifo vya watu 6 na kuwajeruhi wengine 25. Hakuna kundi lolote lililokiri kuhusuika na shambulio hili.

Hata hivyo maafisa wa Taliban wanasisitiza kuwa wanajeshi wao wamewashinda nguvu kundi la dola la kiislamu lakini wachambuzi wanasema IS ni changamoto kubwa kwa usalama wa Afghanistan. Baada ya kuchukua madaraka nchini humo, kundi la Taliban mara kwa mara limevamia na kushambulia maficho ya kundi la IS Mashariki mwa mji wa Nangarhar.

Chanzo: dpa/reuters/ap