1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Ugiriki anaendelea na ziara yake Ulaya

3 Februari 2015

Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras, anaendelea na ziara yake Ulaya, huku akiwa na matumaini ya kuungwa mkono na Italia katika jitihada zake za kuujadili upya mpango wa kuunusuru uchumi wa nchi yake.

https://p.dw.com/p/1EUlN
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis TsiprasPicha: picture-alliance/dpa/Maxppp/X. de Torres

Tsipras, ambaye anafanya ziara hiyo wiki moja baada ya kuingia madarakani, leo (03.02.2015) anaelekea mjini Roma, na anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, ambapo watazungumzia marekebisho ya msaada wa Euro bilioni 240. Awali Renzi alitoa matamshi ya kutia moyo, kwamba Ulaya lazima iachane na mpango wa kuinusuru Ugiriki isifilisike, huku akitaka busara itumike zaidi katika kulitafutia ufumbuzi suala la Ugiriki.

Tsipras anayefata siasa kali za mrengo wa kushoto anataka kuyalegeza masharti magumu ya kubana matumizi, yaliyopendekezwa na wafadhili wa pande tatu ambao ni Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha Duniani-IMF. Akizungumza jana na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa Cyprus, Nicosia, Tsipras aliahidi kufikiwa kwa makubaliano ya jinsi ya kuyalipa madeni hayo kwa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakopeshaji hao.

Rais wa Cyprus, Nicos Anastasiades akiwa na Tsipras
Rais wa Cyprus, Nicos Anastasiades akiwa na TsiprasPicha: picture-alliance/dpa/Katia Christodoulou

''Ugiriki iko katika awamu mpya ya mazungumzo na washirika wake. Majadiliano yanafanyika kwa kuzingatia misingi sawa yaliyomo ndani ya mfumo wa Ulaya. Hitimisho la mazungumzo hayo, halitakuwa na manufaa tu kwa Ugiriki na Cyprus, bali kwa manufaa ya watu wote wa Ulaya,'' alisema waziri mkuu huyo wa Ugiriki.

Afutilia mbali mpango wa kuomba msaada wa Urusi

Aidha, Tsipras alisema amefutilia mbali mpango wake wa kuomba msaada nchini Urusi, katika jitihada za kuangalia namna ya kuunusuru uchumi wa Ugiriki. Akiwa Cyprus, Tsipras, alikutana na Rais wa nchi hiyo, Nicos Anastasiades. Serikali mpya ya Ugiriki ambayo imeikodisha benki ya uwekezaji ya Lazard, ili kuishauri namna ya kusimamia madeni yake, imeungwa mkono na Rais Barack Obama wa Marekani, ambaye ameonya kuhusu kuendelea kuiwekea mbinyo Ugiriki.

Tsipras pamoja na Waziri wake wa Fedha, Yanis Varoufakis, wanazuru Ulaya kwa lengo la kutafuta kuungwa mkono wa kuufanyia marekebisho mpango huo, hatua inayopingwa vikali na Ujerumani. Hapo jana, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, alipuuzia hatua ya Ugiriki kutaka kuachana na mpango wa wafadhili wa pande tatu na kusema kuwa mazungumzo magumu yanaikabili Ugiriki. Hata hivyo, Berlin haiko katika orodha ya miji ambayo Tsipras anaizuru.

Waziri wa Fedha wa Ugiriki, Yanis Varoufakis
Waziri wa Fedha wa Ugiriki, Yanis VaroufakisPicha: picture-alliance/dpa

Tsipras, ameukosoa mfumo wa kundi la pande tatu wa kuufatilia uchumi wa Ugiriki, akisema kuwa unakosa hadhi ya kisheria, na ameilaumu Ujerumani kwa kushinikiza masharti magumu, ambayo ameahidi kuyarekebisha. Kesho Jumatano (04.02.2015) Tsipras atamtembelea Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, mjini Brussels. Jana, Varoufakis alikutana na waziri mwenzake wa fedha wa Uingereza, George Osborne, mjini London.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri:Hamidou Oummilkheir