1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mpya wa Misaada ya Maendeleo na Siasa mpya ya Maendeleo

17 Machi 2010

<p>Tangu mwezi wa Oktoba 2009, mwanasiasa wa Chama cha Free Democratic cha Ujerumani, Dirk Niebel, amekuwa waziri wa ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo.

https://p.dw.com/p/MVLe
Dirk Niebel, waziri wa Ujerumani wa Ushirikiano wa kiuchumi na maendeleoPicha: dpa
Hata hivyo, wahakiki hivi sasa wanamlaumu kwamba waziri huyo amekuwa karibu sana na wanaviwanda wa Kijerumani. Katika kampeni za uchaguzi, Bwana Niebel alitaka bora wizara hiyo ingefutwa kabisa, lakini sasa anautumia wadhifa wake kuendeleza maslahi ya viwanda vya Ujerumani, badala ya kuendeleza siasa za maendeleo. Kwa hilo analaumiwa na wanasiasa pamoja na jumuiya za kiraia, kama anavoripoti Hicham Driouich...

Wizara ya Bwana Dirk Niebel inaitwa wizara ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, lakini tangu mwezi Oktoba mwaka jana mwanasiasa huyo amekuwa karibu zaidi na wanauchumi. Alipoanza ziara yake ya Asia, akielekea Vietnam na Kambodia, mwezi wa Machi, Bwana Niebel alitangaza kwamba anataka katika ziara hiyo kuendeleza hasa uwekezaji wa makampuni ya Kijerumani huko Vietnam na Kambodia. Alisema anaiona kazi yake ni kujenga hali nzuri ya kuweko ushirikiano mzuri wa kiuchumi na nchi zinazoinukia kiuchumi, kama vile Indonesia na India.

Ulrich Post, mkuu wa shirika la VENRO ambalo lina jumuiya 120 za Kijerumani zisizokuwa za kiserekali, mtu ambaye ni mjuzi wa masuala ya misaada ya maendeleo, anasema anachofanya waziri Niebel sio siasa ya maendeleo, lakini ni kuendeleza uchumi wa Ujerumani...

"Sifahamu kampuni gani ya Ujerumani ingependa kuwekeza Burkina Faso au Mnyanmar au katika nchi ilio  kweli maskini na iweze kurejesha nyumbani faida. Kwa hivyo, naamini mara nyingine waziri anataka kuingiza uliberali kidogo."

Hapa Ujerumani, ushirikiano wa kiuchumi pembeni na sekta nyingine, kama vile misaada ya kiutu, zinafungamana na siasa ya maendeleo. Lakini wahakiki sasa wanahofu kwamba ushirikiano wa kimaendeleo utapunguzwa umuhimu wake na kuwa katika ngazi tu ya kiuchumi pamoja na majukumu yake kubadilika, hivyo kichinichini kuviendeleza viwanda vya Kijerumani. Mbunge wa Chama cha Kijani, Uwe Kekeritz, anasema uchumi usiwe katikati ya shughuli hizo:

" Mimi sipingi pale fedha za ushirikiano wa maendeleo zikirejea na kutiririka hadi Ujerumani, lakini dhamira bila ya shaka iwe kwa maslahi ya nchi inayoendelea na sio kwa maslahi ya makampuni makubwa."

Pia mipango ya waziri huyo kutokea Chama cha FDP ya kupunguza matumizi inakosolewa. Dirk Niebel ameliwekea hadharani alama ya kuuliza lile lengo kwamba misaada ya maendeleo ya Ujerumani ifikie kiwango cha asilimia 0.7 ya mapato ya taifa ifikapo mwaka 2015. Sababu alioitoa ni kwamba uthabiti wa misaada hiyo ndio muhimu zaidi kuliko ukubwa wa misaada yenyewe. Tamko kama hilo kutoka kwa waziri huyo limezusha wasiwasi na hasira kutoka kwa wafanya kazi wake mwenyewe, badala ya kuwa na mazungumzo madhubuti. Hivyo ndivyo alivolaumu Karin Roth, mwanachama wa Chama cha SPD katika kamati ya bunge inayoshughulikia siasa za maendeleo. Alisema hiyo ni vurugu iliopangwa na waziri na haitachangia kuleta imani katika siasa ya maendeleo ya Ujerumani. Bibi Karin Roth anahoji  kwamba suala la kubakia na lengo la kutumia  asilimia 0.7 ya mapato ya taifa kwa ajili ya misaada ya maendeleo sio uamuzi ambao pekee waziri anaweza  kuuchukuwa. Amesema kwamba Ujerumani, kama zilivo nchi nyingine, imefungamana na mapatano ya kimataifa, kwa mfano malengo ya Millenium, ambayo yalikubaliwa hapo Septemba mwaka 2000 na wawakilishi wa nchi 189 katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa mjini New York. Katika kikao hicho, nchi fadhili, yaani nchi za viwanda, ziliahidi kutoa fedha zaidi kwa ajili ya ushirikiano wa maendeleo. Kati ya malengo ya tangazo la Millenium ni kuupunguza kwa nusu umaskini duniani, kupambana na magonjwa na kuwawezesha watu kupata maji ya kunywa na elimu. Nchi wanachama wa wa Umoja wa Ulaya zimekubaliana na mpango huo wenye hatua ambapo ifikapo mwaka 2015 nchi zote zilizokwisha kuwa wanachama wa Umoja huo hadi mwaka 2002 zitatakiwa zitoe asilimia 0.7 ya mapato yao ya taifa kwa misaada ya maendeleo; na majukumu kama hayo hayafai kudharauliwa na waziri, alishikilia mwanasiasa huyo, Karin Roth.

Mwandishi:  Driouich, Hicham/Othman, Miraji/ZR

Mhariri: Mohammed Abdulrahman