1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa kwanza Mwislamu katika serikali ya jimbo Ujerumani

Abdu Said Mtullya27 Aprili 2010

Waziri wa kwanza mwislam aapishwa leo katika jimbo la Lower Saxony.

https://p.dw.com/p/N87P
Bibi Aygül Özkan, waziri wa kwanza mwenye nasaba ya kituruki katika serikali ya jimbo Ujerumani.Picha: AP

Waziri wa kwanza mwislamu katika serikali ya jimbo ameapishwa leo nchini Ujerumani.

Hata hivyo kabla ya kuapishwa waziri huyo Aygül Özkan alitifua tufani kutokana na kutoa mwito wa kupiga marufuku misalaba mashuleni.Waziri huyo mwenye nasaba ya kituruki aliapishwa leo alasiri mjini Hannover katika jimbo la Lower Saxony kaskazini magharibi mwa Ujerumani baada ya zogo kubwa lililotokana na mwito huo alioutoa.

Waziri huyo alitoa mwito huo katika mahojiano na jarida maaruf la Ujerumani Focus mwishoni mwa wiki iliyopita.Özkan alisema shule siyo mahala pa misalaba au hijabu.Kauli hiyo ilitifua tufani ndani ya chama chake cha CDU na katika sehemu zingine za jamii nchini Ujerumani kote.

Hata hivyo waziri Mkuu wa jimbo la Lower Saxony Christian Wulff amemtetea waziri wake kwa kusema kwamba lawama zilizotolewa zilitiwa chumvi mno. Waziri Mkuu huyo amesema kuwa bibi Özkan amesharekebisha msimamo wake

Na waziri masuala ya wahamiaji katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Ujerumani Northrhein Westphalia bwana Armin Armin Laschet amesema jambo la furaha ni kwamba kwa mara ya kwanza mtu mwenye nasaba ya kituruki ameapishwa kuwa waziri katika serikali ya jimbo la Ujerumani.Lakini mwenyekiti wa masuala ya kijamii kwenye baraza la wakatoliki Thomas Goppel amesema kauli ya waziri Özkan ni ya makosa.

Hata hivyo waziri huyo mwenyewe ameshaomba radhi kwa kauli aliyoitoa.Waziri Özkan ameurekebisha msimamo wake na ameomba radhi kwa mkanganyiko na machungu aliyoyasababisha katika hisia za watu.

Waziri wake mkuu Christian Wulff amesema anatumai kuwa waziri Özkan atakuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa vijana wenye nasaba za uhamiaji nchini Ujerumani.

Waziri Aygül Özkan alizaliwa katika mji wa Hamburg mnamo mwaka 1971 .Wazazi wake walihamia Ujerumani kutoka Uturuki mnamo miaka ya 60. Baada ya kufuzu masomo ya sekondari alijiunga na chuo kikuu kusomea sheria.Kuanzia mwaka 1999 hadi 2004 alikuwa meneja wa kampuni ya simu ya Ujerumani Deutsche Telekom.Na mnamo mwaka 2004 alijunga na chama cha CDU.

Mwanasiasa huyo atakuwa waziri wa masuala ya kijamii na uhamiaji katika jimbo la Lower Saxony lililopo kaskazini magharibi mwa Ujerumani.

Mwandishi:Abdul Mtullya /dpa,rtr Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman