1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani azuru Afghanistan

Zainab Aziz Mhariri: Daniel Gakuba
11 Machi 2019

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas ambaye anaizuru Afghanistan, amesema ziara yake inaonyesha wazi jinsi Ujerumani ilivyojizatiti katika juhudi za kuleta suluhisho la amani katika mgogoro wa nchini humo.

https://p.dw.com/p/3Enic
Afghanistan Heiko Maas, Außenminister Deutschland in Kabul
Picha: picture-alliance/dpa/Thomas Imo/Photothek.Net/Auswärtiges Amt

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani aliwasili kwenye jimbo la Mazar-e-Sharif Kaskazini mwa Afghanistan hapo jana kwa lengo la kutoa ujumbe wa kusisitiza msimamo wa Ujerumani juu ya kuendeleza juhudi za kuleta  suluhisho la amani katika mgogoro wa nchinini humo.

Ujerumani ni nchi mojawapo ya jumuiya ya kujihami ya NATO inayoiunga mkono Afghanistan kwa kutoa mafunzo kwa majeshi ya usalama ya nchi hiyo na wanajeshi 1200 wa Ujerumani wako nchini Afghanistan kulinda amani. Mwezi uliopita bunge la Ujerumani lilirefusha muda wa kuwepo wanajeshi hao nchini Afghanistan. Ujerumani pia iko tayari kuandaa mkutano juu ya kuleta amani nchini Afghanistan utakaowashirikisha pia Taliban.

Waziri Maas amesema lengo la kufanya ziara nchini Afghanistan na Pakistan ni kutoa ujumbe wazi, kwamba imejizatiti katika kuutekeleza wajibu ilioahidi kuutimiza juu ya Afghanistan. Ujerumani inashika nafasi ya pili kama mfadhili na pia imechangia majeshi nchini Afghanistan.

Maas amesema serikali ya Ujerumani inatekeleza sera ya kuihakikishia Afghanistan kwamba itaendelea kufanya juhudi za kuleta suluhisho la amani na pia kusaidia katika juhudi za kuleta maendeleo ya uchumi katika kanda inayopakana na Afghanistan. Hata hivyo amesisitiza kwamba kufanya mazungumzo na Taliban hakuna maana ya kurejea katika maafa ya miaka iliyopita. Muda wa kuwepo wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan utamalizika mwishoni mwa mwezi huu na kwa hivyo waziri Maas ametahadharisha kwamba mafanikio yote yaliyopatikana yanaweza kusambaratika ikiwa wanajeshi hao wataondolewa.Mafunzo yanayotolewa na wanajeshi wa Ujerumani kwa majeshi ya usalama ya Afghanistan ni muhimu kutokana na kuzidi kuimarika kwa shinikizo kutoka kwa wapiganaji wa kundi la Taliban.

Kushoto: Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas akizungumza na Rais wa Afghanistan Ashraf Ghan
Kushoto: Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas akizungumza na Rais wa Afghanistan Ashraf GhaniPicha: picture-alliance/dpa/Thomas Imo/Photothek.Net/Auswärtiges Amt

Mjadala unaendelea mjini Berlin juu ya muskabal wa wanajeshi wa Ujerumani walioko nchini Afghanistan na bunge la Ujerumani linajadili iwapo litauendeleza muda wa kuwepo wanajeshi hao nchini humo. Waziri wa mambo ya nje Maas anaunga mkono kuendelezwa muda huo.

Wakati huo huo Rais Donald Trump wa Marekani mara kwa mara amekua anatoa kauli za kuashiria kuyaondoa majeshi ya Marekani kutoka Afghanistan, kauli ambazo zimewachanganya washirika wake wa jumuiya ya NATO. Duru zinaarifu kuwa Marekani inafanya mazungumzo na wajumbe wa Taliban kwa lengo la kufikia mapatano, kabla ya mwisho wa mwezi Juni ambapo watu wa Afghanistan watashiriki katika zoezi la kumchagua Rais mpya.

Vyanzo: dpa/p.dw.com/p/3ElHq