1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Ndani Italia awataka Wafaransa wamuondowe Macron

Mohammed Khelef
23 Januari 2019

Mzozo wa kidiplomasia na kisiasa unazidi kufukuta kati ya wanachama wawili waanzilishi wa Umoja wa Ulaya, Italia na Ufaransa na sasa waziri wa ndani wa Italia anatoa wito kwa Wafaransa kumuondoa Rais Emmanuel Macron.

https://p.dw.com/p/3C0yz
Italien Parlament Matteo Salvini, Innenminister
Picha: picture-alliance/dpa/R. Antimiani

Siku ya Jumanne (22 Januari), Waziri wa Mamboy Ndani wa Italia, Matteo Salvini, alitumia ukurasa wake wa Facebook kumshambulia vikali Rais Macron wa Ufaransa akimuita rais mbaya sana anayependa maneno lakini asiye na matendo. Salvini anayeongoza chama kinachopinga wahamiaji, amemtuhumu Macron kwa kuipa darasa Italia na kumtaka badala yake awaruhusu wahamiaji walioko kwenye mpaka wa nchi yake na Ufaransa.

"Ikiwa kweli Macron ni mzuri hivyo, anaweza kuthibitisha kwa kuwaruhusu maelfu ya wakimbizi waliopo Italia na ambao aliwaahidi ukarimu pamoja na mataifa mengine ya Ulaya. Si suala la Matteo Salvini kuingia siasa za Ufaransa, lakini natarajia wananchi wa Ufaransa hapo tarehe 26 Mei watamchaguwa mtu mwengine anayewawakilisha zaidi, aliye makini zaidi, aliye wa matendo zaidi. Namfikiria mtu kama Marine Le Pen...", alisema Salvini.

Lakini akimjibu Salvini, waziri anayeshughulikia masuala ya Ulaya katika serikali ya Ufaransa, Nathalie Loiseau, alisema kuwa Wafaransa walikuwa na muda wa kuchaguwa baina ya Le Pen na Macron na wakafanya chaguo lao. Akitumia mtandao wako wa Twitter, Loiseau aliandika: "Matteo Salvini anawatukana Wafaransa. Wataliano wanafaidika nini? Hawafaidiki kitu. Je, matusi haya yanabadili kitu kwenye siasa za Ufaransa? Hapana!"

Lawama za Italia kwa Ufaransa

Emmanuel Macron
Rais Emmanuel Macron wa UfaransaPicha: Reuters/L. Marin

Wakati serikali ya Italia ikikabiliwa na lawama kwa vifo vya wahamiaji kadhaa vilivyotokea hivi karibuni kwenye Bahari ya Mediterania, Naibu Waziri Mkuu Luigi Di Maio alijaribu Jumapili iliyopita kuzihamishia lawama hizo kwa Ufaransa.

Di Maio alisema Ufaransa ilitumia sera za kikoloni barani Afrika ambazo ziliwatia ufukara Waafrika na kuwafanya sasa wakimbilie pwani za Ulaya.

Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa ilimuita balozi wa Italia siku ya Jumatatu kutokana na kauli hiyo.

Vuguvugu la Nyota Tano la Di Maio linaunga mkono vuguvugu la Vizibao Manjano nchini Ufaransa linaloipinga serikali ya Rais Macron.

Mapema jana, Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte alisema kuwa mzozo wa wakimbizi hautishii urafiki wa kihistoria kati ya mataifa hayo mawili majirani, akisema kuwa mahusiano yao yataendelea kusalia madhubuti na imara licha ya mzozo huu wa kisiasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa
Mhariri: Josephat Charo