1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa ulinzi wa Marekani aishauri Uturuki kujizuia katika operesheni ndani mwa Irak

Kalyango Siraj28 Februari 2008

Marekani yaishawishi Uturuki isikawie sana Irak

https://p.dw.com/p/DF36
Helikopta ya jeshi la Uturuki ikipaa angani katika maeneo ya milimani karibu na mpaka wake na Irak.Picha: picture-alliance/ dpa

Jeshi la Ururuki linasema litabaki kaskazini mwa Iraq kwa mda utakaohitajika ,huku Marekani ikiambia kuwa ni lazima majeshi yake yasikae huko mda mrefu.Iraq kwa upande wake imetaka operesheni hiyo isitishwe mara moja.

Waziri wa ulinzi wa Marekani-Robert Gates-amekutana na cheo somo wake wa Uturuki-Vecdi Gonul mjini Ankara na mazungumzo yamejikita katika suala la operesheni za jeshi la Uturuki dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi wa kundi la PKK kaskazini mwa Iraq.

Baada ya mkutano wao Bw. Gates amesema kuwa Marekani inaamini kuwa operesheni hiyo itachukua mda mfupi na kulenga shabaha zake. Akaongeza kuwa operesheni hiyo isizidi wiki moja au mbili.Operesheni hiyo ilianza Febuari 21 ambapo leo imefikisha siku yake ya nane.

Serikali ya Iraq ambayo inaungwa mkono na Marekani imeitaka Uturuki kukomesha mara moja operesheni hiyo.

Lakini msemaji wa masuala ya nje wa waziri mkuu wa Uturuki-Ahmed Davutoglu amesema kuwa majeshi yao hayataondoka kaskazini mwa Iraq hadi pale lengo lake litakapokamilishwa.

Nae waziri wa Ulinzi wa Uturuki -Vecdi Gonul amewaambia waandishi habari punde tu baada ya kukutana na mgeni wake wa Marekani kuwa jeshi la Uturuki litabakia Iraq kwa mda wanaouhisi kuwa unafaa.

Akafafanua kuwa majeshi yake yanawasaka tu wapiganaji wa PKK na kuongeza kuwa haina nia yoyote ya kuikalia ardhi ya Iraq.

Robert Gates ambae baadae amepangiwa kukutana na waziri mkuu wa nchi hiyo pamoja na rais na vilevile mkuu wa majeshi, amesema kuwa serikali ya Ankara ni lazima ishughulikie masuala ya wa Kurdi ya kiuchumi na kijamii.Wapiganaji wa Kikurdi wanataka kujitawala katika eneo la kusini mashariki mwa Uturuki.Walianza kupigana wakitaka uhuru wao kuanzia mwaka wa 1984.

Gates ameongeza kuwa hatua za kijeshi pekee hazitamaliza tisho hilo la kigaidi.

Marekani inawasiwasi kuwa kuendelea kwa operesheni ya Uturuki nchini Iraq kutahatarisha amani ya eneo hilo hususan Iraq yenyewe.

Majeshi ya Uturuki yakitumia askari wa nchi kavu,ndege za kivita pamoja na Helkopta yaliingia kaskazini mwa Iraq Febuari 21 kwa lengo la kuwang'oa wapiganaji wa kundi la PKK kutoka maeneo hayo ambayo wanayatumia kushambulia Uturuki.

Hii ndio mara ya kwanza ya jeshi la Uturuki kutuma majeshi ya nchi kavu ya kiwango hicho kaskazini mwa Iraq katika mda wa muongo mmoja.

Serikali ya Ankara inawalaumu wapiganaji wa PKK kwa kuwauwa watu takriban laki nne tangu waanzishe harakati za kujitenga mwaka wa 1984.

Pia Uturuki inadai kuwa wapiganaji wa PKK wanaokadiriwa kufika 3,000 wametumia eneo la kaskazini mwa Iraq kuwashambulia wanajeshi na raia wa kawaida nchini Uturuki.

Huku shinikizo la kuitaka Uturuki iondoe majeshi yake kutoka kaskazini mwa Iraq likiongezeka,habari zingine zinasema kuwa wanajeshi zaidi wa Uturuki wametumwa nchini Iraq.Habari zaidi zinasema kuwa wanajeshi hao wa ziada walipelekwa huko hiyo jana jumatano kwa kutumia ndege za helikopta.

Duru za kijeshi zinasema kuwa operesheni ya sasa ya Uturuki inawahusisha wanajeshi wanaofikia elf 10.

Jeshi hilo linadai kuwa hadi kufikia sasa limewauwa wapiganaji wa PKK zaidi ya 230,na kupoteza wanajeshi 24.

Lakini wao wapiganaji wa PKK wanasema wamewauwa wanajeshi wa Uturuki zaidi ya 100.Hata hivyo hawakutoa idadi ya wapiganaji wake waliouliwa ama kujeruhiwa.