1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gate, ziarani Mashariki ya Kati.

Omar Babu19 Aprili 2007

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gates, amewasili kwa ziara ya ghafla nchini Iraq, ambapo amesema amepanga kuwaarifu viongozi wa Iraq kwamba Marekani imepania kuisaidia nchi hiyo kujisimamia kijeshi. Mapema akiwa nchini Israil, punde kabla ya safari yake kwenda Iraq, Robert Gates aliwaambia waandishi wa habari mjadala unaoendelea sasa nchini Marekani kuhusu ufadhili zaidi wa kijeshi nchini Iraq ni thibitisho kwamba umma wa Marekani umechoshwa na vita hivyo.

https://p.dw.com/p/CB4a
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates.

Waziri wa ulinzi, Robert Gates, amewasili nchini Iraq wakati ambapo taifa hilo lingali kwenye wimbi la majonzi kutokana na maafa yaliyosababishwa na mabomu yaliotegwa kwenye magari yaliyowaua watu takriban mia mbili jana.

Waziri Robert Gates alishauriana na Waziri Mkuu wa Israil, Ehud Olmert, leo mara baada ya kusisitiza kwamba msimamo wa Marekani nchini Iraq hautateleshwa na mashambulio hayo ya jana yaliyosababisha vifo vya watu mia moja na tisini.

Waziri Mkuu Ehud Olmert alimsifu Robert Gates kwa kuwa Waziri wa kwanza wa ulinzi wa Marekani kuitembelea Israil tangu mwaka 2000.

Ziara ya Robert Gates katika eneo la Mashariki ya Kati imenuiwa kukabiliana na tishio la Iran ambayo ni taifa hasimu mkubwa wa Israil, na pia kudhihirisha kwamba taifa lake bado linaiunga mkono Iraq.

Mara alipotua mjini Tel Aviv, waziri huyo wa ulinzi wa Marekani alielekea moja kwa moja kukutana na waziri wa ulinzi wa Israil, Amir Peretz.

Kwenye mkutano wa waandishi wa habari baada ya mashauriano kati yake na waziri mwenyeji wake, Robert Gates alilaani waliohusika na mashambulio ya mabomu nchini Iraq.

Waziri Robert Gates pia hakusita kulizungumzia suala la mradi wa Iran wa nishati ya nyuklia baada ya mashauriano yao.

Waziri Robert Gates alisema:

"Nadhani kwanza kabisa hatua muhimu imeshapigwa. Kuna maazimio mawili ya umoja wa mataifa. Jumuiya ya kimataifa kwa pamoja imeshaipa Iran maagizo ya kuzingatia kuhusu mradi wake wa nyuklia. Hili si jambo la kupapia. Kwangu mimi njia mwafaka ya kulitanzua tatizo hili ni njia ya mashauriano ya kibalozi"

Waziri Robert Gates aliwasili nchini Israil kwa mkondo wa tatu wa safari yake baada ya kuzitembelea Jordan na Misri.

Suala la mazungumzo yaliyokwama kati ya Wapalestina na Israil ndilo lililoyamiliki mashauriano kati ya Robert Gates na viongozi wa Jordan na Misri.

Ingawa haijatangaza rasmi, Israil ndilo taifa la pekee katika mashariki ya kati ambalo lina silaha za kinyuklia.

Hoja ya Iran kuwania kupata nishati ya kinyuklia inaitatiza Israil hasa ikizingatiwa kuwa Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad amewahi kusema kwamba taifa hilo linapaswa kuondolewa duniani.

Waziri Robert Gates akiwa bado kwenye ziara yake ya Mashariki ya Kati amefika nchini Iraq na kufululiza moja kwa moja hadi Fallujah kushauriana na wakuu wa majeshi ya Marekani.

Mji wa Fallujah katika jimbo la Al-Anbar ndio ngome ya zamani ya wanamgambo wa Kisunni.

Siku nenda siku rudi majeshi ya Marekani yamekuwa yakipambana na wanamgambo hao wa Kisunni wanaosemekana wanaungwa mkono na kundi la Al-Qaeda.

Waziri Robert Gates anashikilia msimamo wa Rais George W Bush wa nyongeza ya wanajeshi wa kudhibiti hali nchini Iraq.

Wakuu wa Iraq na Marekani wamewajumuisha wanajeshi kiasi elfu nane ili kurejesha usalama nchini humo lakini mashambulizi ya mabomu yamekuwa yakiendelea kila uchao.