1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westerwelle akutana na waandamanaji Kiev

5 Desemba 2013

Shinikizo dhidi ya Rais wa Ukraine Viktor Yanukovych linaendelea kushamiri baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle kukutana na waandamanaji wanaotaka nchi yao ifikie makubaliano na Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/1ATJ3
Guido Westerwelle und Vitaly Klitschko in Kiew
Picha: DW/O. Sawitsky

Naye Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry amesema raia wa Ukraine wanastahili kupewa nafasi ya kuamua mustakabali wao. Mawaziri wa Kigeni wa Umoja wa Ulaya wanakutana katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev, ambao umegubikwa na maandamano makubwa ya kuupinga uamuzi wa serikali kukataa kusaini makubaliano ya ushirikiano na Umoja huo, na badala yake kuigeukia Urusi. Maelfu ya wanaharakati wanaendelea kufanya maandamano wakati baraza la mawaziri la Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya likianza mkutano wake mjini humo.

Hayo yanajiri wakati mbinyo ukiendelea kuwekwa dhidi ya Rais Viktor Yanukovych. Marais watatu wa zamani wa Ukraine, Leonid Kravchuk, Leonid Kuchma and Viktor Yushchenkopia wamejitokeza kwa kuyaunga mkono maandamano ya umma dhidi ya serikali. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle aliwasili mjini Kiev jana usiku kwa ajili ya mkutano wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya – OSCE na akaelekea moja kwa moja katika uwanja wa kihistoria wa Uhuru ambako alizungumza ana kwa ana na waandamanaji.

Alitembea kwa miguu kuelekea katika uwanja huo, ambako yalifanyika maandamano yaliyojulikana kama vuguvugu la rangi ya chungwa, ambalo lilileta mageuzi ya mwaka wa 2004. Westerwelle aliandamana na Vitali Klitschko, bingwa wa ndondi ambaye ni kiongozi wa upinzani nchini Ukraine, na ambaye hufanyia mazoezi yake nchini Ujerumani. Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani aliwaunga mkono waandamanaji. Guido amesema "Inatambulika kuwa Ukraine inaendeleza mazungumzo makubwa ya kindani. Na hapa lazima Ulaya ichangie, kwa sababu yanahusu Ulaya".

Kiew Ukraine Protest EU Regierung
Maandamano ya kuipinga serikali mjini KievPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry pia alipaza sauti yake akisema Waukraine wana haki ya “kuchagua mustakabali wao” bila shinikizo la nje, akionekana kumaanisha Urusi, ambayo Ukraine imesema iliilazimisha kuukataa muafaka wa Ulaya.

Huku Ukraine ikitafuta fedha za kuimarisha uchumi wake, rais Viktor Yanukovych aliendelea na ziara yake ya siku tatu nchini China, ambayo huenda ikamzawadia mikataba muhimu ya kifedha.

Tangu maandamano yaliyoanza mwishoni mwa wiki iliyopita yalipopungua, upinzani umefanikiwa kutwaa udhibiti wa uwanja wa uhuru, na kuezeka hema ambapo chakula na mavazi vinapatikana. Takribani wafuasi 10,000 wa rais Yanukovych jana walifanya maandamano ya kuupinga upinzani katika ngome yake ya Donetsk. Huku ikitafuta uwiano baina ya Urusi na Umoha wa Ulaya, serikali ya Ukraine imesema inataka kufanya mazungumzo na pande hizo mbili.

Waziri Mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev, ambaye serikali yake inataka Ukraine ijiunge na muungano wa forodha unaoongozwa na Urusi, aliupokea ujumbe wa Ukraine hapo jana. Maafisa wa Ukraine pia wanafanya mazungumzo ya kuutuma ujumbe mwingine mjini Brussels. Umoja wa Ulaya ulionekana kutokuwa na haraka ya kutangaza tarehe halisi, lakini Rais Herman van Rompuy amesema “matarajio makubwa ya Waukraine” yako wazi na kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari kuyashughulikia.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba