1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaidhinisha chanjo ya Kichina ya Sinovac

2 Juni 2021

Shirika la Afya Duniani WHO limeidhinisha chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa na Sinovac Biotech kwa ajili ya matumizi ya dharura. Uamujzi huo utaiwezesha chanjo hiyo ya Kichina kutumika katika nchi masikini.

https://p.dw.com/p/3uKzg
WHO-Zulassung für chinesischen Impfstoff Sinovac Biotech
Picha: Chaiwat Subprasom/SOPA Images /ZumaWire/dpa/picture alliance

Idhini ya WHO ni uthibitisho kwa wasimamizi wa kitaifa juu ya usalama na ufanisi wa bidhaa za kiafya. Hivyo uamuzi huo utairuhusu chanjo ya Sinovac kuingizwa katika COVAX, mpango wa kimataifa unaotoa chanjo haswa kwa nchi masikini, ambazo hivi sasa zinakabiliwa na matatizo makubwa ya usambazaji, kutokana na ukomo wa mauzo ya nje nchini India.

Jopo huru la wataalam la WHO limesema katika taarifa yake kwamba inaipendekeza chanjo hiyo ya Sinovac kwa watu wazima waliopindukia miaka 18.

Soma zaidi: Ujerumani kusaidia utengenezaji chanjo Afrika Kusini

"Ulimwengu unahitaji sana chanjo za aina nyingi za COVID-19 ili kuziba pengo la ukosefu mkubwa unaojitokeza kote ulimwenguni," amesema Mariangela Simao, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa WHO wa upatikanaji wa bidhaa za afya, akiunga mkono uamuzi huo.

Aliongeza, " WHO inahimiza watengenezaji wa chanjo kushirikiana na kituo cha COVAX, kubadilishana maarifa na data ili kulidhibiti janga hilo la maambukizi ya virusi vya corona."

Aidha Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema chanjo hiyo ni salama na yenye ufanisi, na mahitaji yake ya uhifadhi pia ni rahisi  jambo linayoifanya iwe inafaa kwenye maeneo ya joto kali.

WHO-Zulassung für chinesischen Impfstoff Sinovac Biotech
WHO yaidhinisha chanjo ya Kichina Sinovac BiotechPicha: Donal Husni/ZumaWire/dpa/picture alliance

China yaripoti maambukizi mapya ya virusi vya corona

Wakati huo huo China Jumatano imeripoti maambukizi mapya 24 ya virusi vya corona. Kati ya maambukizi hayo, 14 yaliingizwa nchini kutoka nchi za nje, kulingana na taarifa za Tume ya Kitaifa ya Afya. Na maambukizi mengine 10 yaliyobakia yameripotiwa katika mkoa wa kusini wa Guangdong. Hata hivyo hakuna vifo vilivyoripotiwa.

Halikadhalika Uingereza haikuripoti vifo vyovyote vinavyotokana na maambukizi ya virusi vya corona kwa mara ya kwanza tangu mwezi Machi.

Waziri wa Afya wa Uingereza Matt Hancock amesema matokeo hayo yanamaanisha wazi kwamba chanjo zinafanya kazi.

Soma zaidi:Mchakato wa kutafuta dawa ya corona umefikia wapi?

Ujerumani kwa upande wake imeripoti ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona kwa siku ya pili mfululizo kulingana na Taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch.

Kulingana na taarifa za leo asubuhi, idadi ya maambukizi mapya ilikuwa ni watu 36 kati ya wakaazi 100,000 katika siku saba zilizopita, ikilinganishwa na maambukizi 35 ya siku iliyopita. Hata hivyo takwimu hizo bado zinaonyesha kupungua kwa maambukizi ikilinganishwa na maambukizi mapya 46.8  katika kila watu 100,000 ya Jumatano iliyopita.

Vyanzo: rtre,dpa