1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

WHO yaonya wimbi la kwanza la janga la covid-19 halijaisha

Iddi Ssessanga
26 Mei 2020

Wakati Brazil na India zikipambana na ongezeko la visa vya corona, mtaalamu wa juu wa afya ameonya kuwa dunia bado imo katikati mwa janga, na kufifisha matumaini ya kurejea haraka maisha ya kawaida.

https://p.dw.com/p/3cn5h
Indien Coronavirus Guwahati Medical College Hospital
Picha: picture-alliance/AP Photo/A.Nath

"Bado tuko kwenye awamu ambapo kimsingi ugonjwa unaendelea kuongezeka," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa huduma za dharura wa Shirika la Afya Duniani WHO, Dr. Mike Ryan, wakati akizungumza na waandishi wa habari, akigusia maeneo ya Amerika Kusini na Asia Kusini na maeneo mengine ambako maambukizi yanaendelea kupanda.  

India imeshuhudia ongezeko kubwa la siku la maambukizi kwa siku ya saba mfululizo. Taifa hilo limeripoti maambukizi mapya 6,535 siku ya Jumanne, na kupandisha idadi jumla hadi 145,380, vikiwemo vifo 4,167.

Schweiz PK Michael Ryan WHO
Mike Ryana, Mkurugenzi Mkuu wa Mipango ya dharura wa WHO ameonya kuwa wimbi la kwanza la janga la covid-19 bado halijaisha.Picha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Kirusi cha corona kimeshamiri miongoni mwa jamii za watu maskini zaidi nchini India, na kutilia mkazo changamoto zinazozikabili mamlaka katika kuzuwia usambaji wa virusi hivyo ambavyo hadi wakati huu havijapatiwa chanjo wala tiba.

Visa vingi zaidi nchini India vimejikita katika majimbo ya magharibi ya Maharashtra, nyumbani kwa kituo cha shughuli za kifedha cha Mumbai, na Gujrat. Maambukizi yameongezeka pia upande wa mashariki ambako wafanyakazi wahamiaji waliokwama kutokana na vizuwizi walirejea vijijini kwao kutoka miji mikubwa zaidi ya India.

Licha ya haya, India imeruhusu safari za ndege za ndani kuanza tena siku ya Jumatatu, kufuatia usitishwaji uliodumu kwa miezi miwili, lakini urejeshaji huo ulikuwa wa sehemu tu ya safari za kawaida.

Hali ya wasiwasi Brazil

WHO imetilia mashaka matumaini ya rais wa Brazil ya kufunguliwa tena haraka kwa uchumi, ikionya kwamba serikali inapaswa kwanza kufanya upimaji wa kutosha ili kudhibiti kuenea kwa virusi.

Brazil ina maambukizi 375,000 ya virusi vya corona, ikitanguliwa tu na Marekani yenye jumla ya visa milioni 1.6, na imehesabu vifo 23,000, lakini wengi wanahofia kwamba idadi halisi ya vifo ni kubwa zaidi.

Brasilien Jair Bolsonaro vor einem Hot Dog Stand
Rais wa Brazil Jair Bolsonaro akinunua soseji mtaani wakati wa mripuko wa ugonjwa wa covid-19 mjini Brasilia, Mei 23, 2020.Picha: Reuters/A. Machado

Ryan alisema viwango vikubwa vya maambukizi vya Brazil vinamaanisha inapaswa kubakisha baadhi ya hatua za kusalia nyumbani, bila kujali madhara hasi kwa uchumi wake. "Laazima uendelee kufanya kila unachoweza," alisema.

Lakini Gavana wa jimbo la Sao Paulo, Joao Doria, ameondoa uwezekano wa vizuwizi kamii katika jimbo hilo lenye uchumi mkubwa zaidi nchini Brazil, na anapanga kuanza kulegeza vikwazo Juni 1.

Marufuku ya kusafiri ya Marekani dhidi ya wageni kutoka Brazil ilyokuwa ianze kutekelezwa Jumanne, ilisogezwa siku mbili mbele kuliko tarehe yake ya awali. Marufuku hiyo haiwahusu raia wa Marekani.

Idadi ndogo ya vifo Urusi yaibua maswali

Barani Ulaya, Urusi imeripoti rikodi ya ongezeko la vifo 174, na kufikisha jumla ya vifo vilivyothibitishwa kuwa 3,807. Idadi ya visa jumla vya maambukizi nchini Urusi imevuka 360,000 - ya tatu kwa ukubwa duniani, ambapo visa vipya karibu 9,000 vimerikodiwa.

Idadi ndogo ya vifo nchini humo imezusha maswali miongoni mwa wataalamu. Maafisa wa Urusi hata hivyo, wanakanusha vikali udanganyifu wowote na wanasema idadi ndogo ya vifo inatokana na ufanisi wa hatua za udhibiti zinazotekelezwa na serikali.

Miito ya kufungua mipaka Ulaya

Swali na nani asafiri wapi na lini linasalia kuwa kitendawili ambacho maafisa bado hawajakitengua. Waziri wa mambo ya nje wa Uhispania alisema Jumanne kwamba mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yanapaswa kukubaliana kufungua mipaka na kwa pamoja yaamue mataifa yepi ya umoja huo yanaweza kuwa salama kusafiri.

Belgien Brüssel | Rat fuer Aussenbeziehungen: Arancha Gonzalez Laya und Luigi Di Maio
Waziri wa mambo ya nje wa Uhispania Arancha Gonzalez Laya (kushoto) amesema Umoja wa Ulaya unapaswa kukubaliana kufungua mipaka kwa watalii.Picha: Getty Images/AFP/J. Thys

Arancha Gonzalez Laya amekiambia kituo cha redio cha Cadena SER, kwamba kurejea kwa usafiri wa kuvuka mipaka unapaswa kuamuliwa kwa pamoja hata kama mataifa katika kanda hiyo ya wanachama 27 yanaondoa vizuwizi kwa tarehe tofauti.

"Tutaanza kushirikiana na washirika wetu wa Ulaya kurejesha uhuru wa kusafiri katika ardhi ya Ulaya," alisema. Uhispania ina shauku ya kuwakaribisha tena watalii ili kusaidia sekta inayochangia asilimia 12 ya pato jumla la taifa hilo.

Hali mpya ya kawaida, utaratibu mpya

Indonesia imesema itapeleka vikosi 340,000 vya usalama katika miji 25 kusimamia utekelezaji wa miongozo ya kiafya wakati taifa hilo la nne kwa kuwa na wakazi wengi duniani likijiandaa kufungua tena maduka na bishara nyingine katika mji mkuu Jakarta hapo Juni 4.

"Tunataka kuingia katika hali mpya ya kawaida na kuingia utaratibu mpya," alisema rais wa Indonesia Joko Widodo, baada ya kukagua hatua za kufungua tena huduma za usafiri wa treni za chini ya ardhini na maduka ya bishara mjini Bekasi.

Korea Kusini ilianza Jumanne kuwatka watu wavae barakoa wawapo kwenye usafiri wa umma na taxi. Nchi hiyo inafuatilia dazeni kadhaa za maambukizi yanayohusishwa na vilabu vya usiku na maeneo mengine, wakati ikijiandaa kwa ajili ya kurejea shuleni na vyuoni kwa wanafunzi milioni 2.4 siku ya Jumatano.

Wizara ya afya ya Korea Kusini imesema kuanzia Juni, biashara za hatari kubwa kama vile baa, vilabu vya usiku, majumba ya mazoezi, vyumba vya kuimba na kumbi za matamasha, yatatakiwa kutumia code za QR kuwasajili wateja ili waweze kupatikana kwa wepesi zaidi iwapo maambukizi yatatokea.

Lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yamaitaja hatua hiyo kuwa iliyopitiliza. "Hivyi ndivyo tunavyoingia katika taifa la uchunguzi," walisema katika taarifa.

Coronavirus - Hydroxychloroquin
Dawa ya malaria ya hydroxychloroquin imeondolewa kwenye dawa za majaribio za tiba ya covid-19.Picha: picture-alliance/dpa/Zuma/Quad-City Times/K. E. Schmidt

Hydroxychloroquin yaondolea tiba za majaribio

Katika nyanja ya kitabibu, WHO imesema itasitisha kwa muda dawa ya hydroxychloroquine - dawa ya malaria ambayo rais wa Marekani Donald Trump alisema alikuwa akiitumia - kutoka utafiti wake wa kimataifa wa tiba za mjaribio za covid-19.

Tangazo hilo limekuja baada ya waraka uliyochapishwa kwenye jarida la kitabibu la Lancet, kuonyesha kuwa watu wanaotumia dawa hiyo wanakabiliwa na hatari ya kifo na matatizo ya moyo.

Lakini bado mataifa kadhaa barani Ulaya na Afrika Kaskazini yanatumia chloroquinena hydroxychloroquine kutibu wagonjwa wa covid-19.

Tiba nyingine katika utafiti wa WHO, ikiwemo dawa ya majaribio ya remdesivir na mchanganyiko wa tiba ya VVU, bado zinafuatiliwa. Wakala wa dawa wa Uingereza ulisema Jummane kwamba umeruhusu matumizi ya remdesivir kuwatibu watu wazima na vijana waliolazwa na covid-19 kali.

Majaribio ya hospitali ya dawa za kupambana na virusi yanaendelea kote duniani, lakini matokeo ya awali yanaonyesha inaweza kuharakisha uponaji kwa watu walioambukizwa na virusi vya corona.

Mashirika ya utangazaji yapania kukabiliana na habari za uongo

DW Funkhaus Bonn Claim Made for minds Totale
DW na mashirika mengi ya kimataifa zemeahidi kupambana dhidi ya habari za uongo kuhusu janga la covid-19.Picha: DW/M. Müller

Mashirika saba ya utangazaji ya umma kutoka nchini Marekani, Ulaya, Canada, Japan na Australia, yamesema yatafanyakazi kuzuwia kushamiri, hasa kupitia mitandao ya kijamii, kwa habari za uzushi kuhusu covid-19.

Mashirika hayo ni pamoja na France Medias Monde, Deutsche Welle, BBC, NHK World, CBS Radio-Canada, ABC Australia na shirika la Marekani kwa vyombo vya habari vya kimataifa, ambalo linahusisha Sauti ya Amerika na Radio Free Asia.

Duniani kote, virusi vya corona vimewaambukiza karibu watu milioni 5.5, na kuuwa zaidi ya 346,000, kwa mujibu wa hesabu za chuo kikuu cha John Hopkins cha nchini Marekani.

Ulaya imerikodi karibu vifo 170,000 na Marekani imeshuhudia karibu vifo 100,000. Watalaam wanasema idadi hiyo hainyeshi athari halisi za janga hilo kutokana masuala yanayohusiana na hesabu katika mataifa mengi.

Chanzo:AFPE