1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yasifu 'mafanikio' ya utafiti wa dawa ya kutibu COVID-19

John Juma
17 Juni 2020

Shirika la Afya Duniani WHO, limeyakaribisha matokeo ya awali ya utafiti wa dawa ya dexamethasone kutibu COVID-19 na kuyataja kuwa ‘mafanikio’. Dawa hiyo inaweza kupunguza hatari ya kifo kwa wagonjwa mahututi.

https://p.dw.com/p/3dtYc
Dexamethasone Medikament gegen corona
Picha: Getty Images/AFP/B. Guay

Watafiti katika chuo kikuu cha Oxford wamesifia kile walichokitaja kuwa ‘hatua kubwa' katika kuwatibu wagonjwa wa COVID-19. Hii ni baada ya dawa aina ya steroidi dexamethasone kuthibitishwa kuwa na uwezo wa kuepusha hatari ya kifo miongoni mwa wagonjwa mahututi.

Utafiti uliofanywa kwa zaidi ya wagonjwa 2,000, umeonyesha kuwa dawa hiyo ilipunguza hatari ya mgonjwa kufa kutoka asilimia 40 hadi asilimia 28, haswa wagonjwa ambao hawangeweza kupumua bila usaidizi wa mashine.

Dexamethasone yapunguza hatari ya kifo

Soma pia: WHO yaahirisha majaribio ya hydroxychloroquine kwa COVID-19

Matokeo ya awali pia yameonyesha kuwa dawa hiyo iliweza kupunguza hatari ya vifo kutokea miongoni mwa wagonjwa waliowekewa oksigeni bila ya mashine kutoka asilimia 25 hadi 20.

Mtafiti kwa jina Peter Horby katika chuo cha Oxford amesema hiyo ndiyo dawa pekee ambayo hadi sasa imethibitishwa kuweza kupunguza hatari ya kifo kwa wagonjwa mahututi wa COVID-19.

Daktari Peter Bach ambaye ni mtaalamu wa sera ya afya katika kituo cha kutibu saratani mjini New York amesema madaktari wanapaswa kuitumia dawa hiyo.

Dawa ya Dexamethasone inaweza kupunguta hatari ya kifo miongoni mwa wagonjwa wa COVID-19 ambao wako katika hali mahututi. Watafiti wasema.
Dawa ya Dexamethasone inaweza kupunguta hatari ya kifo miongoni mwa wagonjwa wa COVID-19 ambao wako katika hali mahututi. Watafiti wasema.Picha: Reuters/Y. Herman

"Huu ni utafiti mmoja tu lakini ni bayana kutokana na matokeo yake kwamba dexamethasone itapunguza hatari ya kifo. Kwa hivyo ikiwa madaktari wana wagonjwa mahututi kutokana na COVID-19 na hawana tiba mbadala, wanapaswa kutumia dexamethasone, hadi tutakapofahamu mengi zaidi” Amesema Daktari. Peter.

Soma pia: Kampuni ya dawa ya Sanofi yahakikisha kutoa chanjo ya COVID-19

WHO yakaribisha matokeo na kuyataja kuwa hatua kubwa

Shirika la Afya Duniani WHO, limeyakaribisha matokeo hayo ya awali na kuyataja pia kama ‘mafanikio'.

Kwenye taarifa yake hapo jana, mkuu wa shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema kuwa hiyo ndiyo dawa ya kwanza kuthibitisha inaweza kupunguza hatari ya kifo kwa wagonjwa wanaohitaji oksijeni au kuwekwa kwenye mashine ya kusaidia katika kupumua.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: picture-alliance/Xinhua/WHO

Ghebreyesus ameisifu serikali ya Uingereza, chuo kikuu cha Oxford, hospitali pamoja na wagonjwa walioshirikishwa kwenye utafiti huo.

Dexamethasone imekuwa ikitumika tangu miaka ya 1960

Watafiti hao wa Uingereza wameripoti kuwa majaribio yalionyesha kuwa vipimo vidogo vya dawa hiyo kwa wagonjwa mahututi walioko kwenye mashine ya kuwasaidia kupumua, vilikuwa na uwezo wa kupunguza theluthi moja ya vifo. Aidha vingeepusha moja juu ya tano ya vifo vya wagonjwa ambao wanapewa oksijeni.

Watafiti hao wametaja matokeo ya utafiti huo kama hatua kubwa itakayookoa uhai wa wagonjwa.

Corona: Juhudi za kutafuta chanjo ya COVID19 zapamba moto

Martin Landray ambaye ni miongoni mwa watafiti wa chuo kikuu cha Oxford na ambaye alihusika kwenye moja kati ya majaribio, amesema dexamethasone, dawa ambayo imekuwa ikitumika tangu miaka ya 1960, kutibu uvimbe pamoja na maradhi kama ya pumu, inaweza kuwa njia nafuu ya kupambana na janga la COVID-19.

Maambukizi ya COVID-19 yapindukia watu milioni nane

Soma pia: Mabilioni kuchangwa kwa ajili ya kutafuta chanjo ya corona

Hadi sasa hakuna chanjo ambayo imepatikana kukabili virusi vya corona.

Idadi ya maambukizi ulimwenguni kote imepindukia watu milioni 8, na zaidi ya 430,000 wamefariki, tangu mripuko huo ulipotokea nchini China Disemba mwaka uliopita.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amewaambia waandishi wa habari kwamba matokeo ya utafiti huo ni jambo la kusherehekea mafanikio ya Uingereza kisayansi.

Chanzo; DPAE, DW