1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

William Hague kukutana na viongozi wa muungano wa upinzani Syria

MjahidA16 Novemba 2012

Viongozi wa muungano wa upinzani nchini Syria ulioundwa hivi karibuni, leo wanatarajiwa kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague mjini London.

https://p.dw.com/p/16kL9
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William HaguePicha: AP

Kulingana na shirika la utangazaji la BBC, Mkuu wa muungano huo wa Upinzani nchini Syria, Ahmed Moaz al-Khatib, pamoja na wanachama wengine watatu wa muungano huo wanatarajiwa kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague. Uingereza inania ya kuutaka muungano huo kuweka wazi mpango wao juu ya kipindi cha mpito nchini Syria.

Uingereza imesema pindi tu muungano huo utakapofanya hivyo, basi itatilia maanani swala la kuwatambua rasmi kama muungano halali wa upinzani kwa utawala wa rais Bashar Al Assad. Tayari Ufaransa, Uturuki na mataifa ya eneo la Guba yanautambua rasmi muungano huo wa upinzani.

Huku hayo yakiarifiwa ndani ya Syria kwenyewe, wanaharakati wa upinzani wanasema vikosi vya serikali vimeanza kulishambulia eneo linalokaliwa na waasi la al Rastan mjini Homs. Mashambulizi mengine yameripotiwa katika mji wa al-Zabadani nje kidogo ya mji mkuu Damascus. Kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria lililo na makao yake mjini London, takriban watu 140 wameuwawa katika mashambulizi ya jana pekee.

Wanachama wa muungano mpya wa upinzani, Syria
Wanachama wa muungano mpya wa upinzani, SyriaPicha: Reuters

Kwa upande mwengine Ufaransa imesema itazungumza pamoja na wanachama wengine 27 wa Umoja wa Ulaya juu ya pendekezo la kupunguza vikwazo vya silaha vya Umoja huo ambavyo kwa sasa vinazihusu pande zote mbili zinazohusika na vita vya Syria. Lakini Urusi imesema hatua yoyote ya aina hiyo itakuwa ni kukiuka sheria ya kimataifa .

Kwa Upande wake waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema hatua ya waasi kupewa silaha ni njia moja ya kuwalinda kutokana na mashambulizi makali yanayofanywa na vikosi vya serikali ya Assad.

Jengo moja likiwaka moto nchini Syria
Jengo moja likiwaka moto nchini SyriaPicha: dapd

"Hakuna haja ya kuupa sura ya kijeshi mzozo huu. Lakini haikubaliki pia kuona maeneo yaliyokombolewa,yanashambuliwa kwa mabomu. Lazima pawepo wizani,na si rahisi. Kwa upande mmoja kutoingilia upande wa kijeshi na upande wa pili kuzuwia maeneo yaliyokombolewa yasibomolewe. Ndio maana suala la kupelekwa silaha za kujilinda linabidi lizushwe hapa." amesema Laurent Fabius

Umoja wa Mataifa walalamika

Wakati huo huo kwa mujibu wa barua iliyolifikia shirika laahabari la AFP hapo jana Umoja wa mataifa umelalamika kwa serikali ya Syria kwa kudai kwamba ilikuwa na ruhusa ya umoja huo kuwashambulia waasi katika eneo la milima ya Golan ambalo halipaswi kuwa na harakati zozote za kijeshi.

Katika barua iliotumwa kwa balozi wa Syria, Mkuu wa Umoja huo anayeshughulika na swala la amani Herve Ladsous, aliitaka Syria kusimamisha mashambulizi hayo mara moja katika maeneo hayo ya kijeshi yalio kati ya Syria na Israel ambayo huenda yakahatarisha maisha ya raia pamoja na waangalizi wa Umoja wa Mataifa walioko huko.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia amani Herve Ladsous
Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia amani Herve LadsousPicha: picture-alliance/Kyodo

Tangu kuanza kwa mapigano nchini Syria miezi 20 iliopita tariban watu 39,000 wameuwawa

Mwandishi: Amina Abubakar/ dpa/ AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman