1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi jengine la maandamano ya wapalestina Gaza

Oumilkheir Hamidou
6 Aprili 2018

Maelfu ya wapalastina wameanza kuandamana katika eneo la mpakani kati ya Israel na Gaza ambako wanajeshi wa Israel waliwauwa watu 19 wiki iliyopita katika tukio baya kabisa kushuhudiwa tangu vita vya mwaka 2014.

https://p.dw.com/p/2valo
Palästina Proteste Gaza Streifen
Picha: Reuters/M. Salem

 

Mikururo ya wapalestina wanaelekea katika eneo la mahema karibu na mpaka unaoigawa Gaza na Israel, kwa kile ambacho viongozi wa Hamas wanataraji litakuwa wimbi la pili kubwa kabisa la maandamano katika mlolongo wa maandamano yaliyopangwa kuendelea hadi Mei 15 inayokuja.

Mamia wameanza kumiminika kabla ya sala ya alfajiri leo katika mojawapo ya kambi za mahema karibu na mpaka wa mkoa wa Khuzaa.

Kwa upande wao wanajeshi wa Israel wamepiga kambi tangu alfajiri katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa mashahidi vikosi vya Israel vilifyetua gesi za kutoa machozi ndani ya kambi hizo za mahema na kupelekea umati wa watu kusukumana.

Wanaharakati wa kipalestina wanatarajiwa kutia moto mipira ya magari kwa lengo la kuwazuwia wanajeshi wa Israel wasiwaone.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Stéphane Dujarric
Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Stéphane DujarricPicha: Imago/ZUMA Press/M. Brochstein

Umoja wa Mataifa wazisihi pande zinazohusika zijizuwie

Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa katika eneo la mashariki ya kati, Nickolay Mdalenov amezungumzia wasiwasi wake kutokana na kuzidi makali matumizi ya nguvu katika eneo hilo la mpakani kati ya Gaza na Israel. Zaidi ya watu 20 wameuwawa tangu wapalastina walipoingia njiani kudai kurejea katika mkaazi yao wiki iliyopita.

Akizungumza na waandishi habari mjini New York, msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa  Stephane Dujarric ametilia mkazo wito wa mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa na kusema:"Bwana Mladenov anawatolea wito waisraeli wajizuwie na wapalastina wajiepushe na ugomvi katika uzio wa Gaza. Maandamano na malalamiko yanastahiki kuruhusiwa kuendelea kwa njia ya amani.Lakini raia na hasa watoto wasitumiwe kwa lengo la kuyatia hatarini maisha yao kwa vyovyote vile."

Ripoti zinasema wapalastina watatu wamejeruhiwa hivi punde wanajeshi wa Israel walipofyetua risasi katika maeneo matatu tofauti karibu na mpaka wa Gaza. Msemaji wa jeshi la Israel anasema wanajeshi wamefyetua risasi ili kutoa onyo. Shirika la hilali nyekundu la Wapalastina limeweka vituo vya matibabu katika eneo hilo la mpakani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP/dpa

Mhariri:Josephat Charo