1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito kufungamanisha Biashara na Haki za Watoto

P.Martin17 Mei 2008

Umoja wa Ulaya katika uhusiano wake wa kibiashara na nchi za kigeni,umehimizwa kuwa na masharti yatakayosaidia kupunguza ajira ya watoto na hatimae kuiondosha kabisa kote duniani.

https://p.dw.com/p/E1XW

Kwa mujibu wa Shirika la Ajira la Umoja wa Mataifa-ILO,kiasi ya watoto milioni 218 hapa duniani, wanalazimika kufanya kazi,wengi wao wakiwa chini ya umri wa miaka 14.Ingawa taasisi za Umoja wa Ulaya zinasaidia mipango ya elimu katika nchi masikini ili watoto waweze kwenda shule badala ya kutafuta kazi kwa azma ya kuongeza pato dogo la familia zao,taasisi hizo bado hazina mkakati dhahiri unaopinga ajira ya watoto.

Richard Howitt,mbunge wa chama cha Labour cha Uingereza katika Bunge la Ulaya amelalamika kuwa hakuna juhudi inayofanywa kujumuisha masharti ya kisheria katika makubaliano ya biashara kati ya Umoja wa Ulaya na nchi zingine,yatakayopelekea nchi hizo kuondosha ajira ya watoto.

Kundi liitwalo "Stop Child Labour" linapigania kusitisha ajira ya watoto na linataka kuona Umoja wa Ulaya ukiweka masharti ya kuziwajibisha nchi za kigeni kukomesha ajira ya watoto katika muda utakaokubaliwa,ili bidhaa za nchi hizo zinufaike kuingia katika masoko ya Umoja wa Ulaya kwa urahisi..

Ripoti ya "Stop Child Labour" iliyotayarishwa na Gerard Oonk inasema,nchi masikini hulazimika kutia saini makubaliano ya kimataifa kuhusu haki za binadamu na ajira,ili bidhaa zake ziweze kuingia masoko ya Ulaya bila ya vikwazo vingi.Kwa ufupi,mfumo huo hujulikana kama GSP na kuna nchi 15 zinazofaidika. Colombia na Bolivia katika Amerika Kusini ni miongoni mwa nchi hizo,lakini zote mbili zina tatizo kubwa - kwani nchini humo watoto hutumiwa kufanya kazi.Oonk anasema,nchi kama hizo hazistahili kurahisishiwi kuingiza bidhaa zake katika masoko ya Umoja wa Ulaya.

Kwa upande mwingine,kundi la Kiholanzi "Hivos" linalopiga vita umasikini,limesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika miradi ya shule,kwani hiyo ni njia bora kabisa kusaidia kukomesha ajira ya watoto na kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi hizo masikini baadae utaweza kuendelea kwa msaada wa watu wazima walioelimika.

Hivi karibuni ripoti ya kundi la Umoja wa Mataifa linalopigania elimu kwa wote,imesema baadhi ya nchi za Ulaya hazitoi mchango wa kutosha kusaidia miradi inayotaka kuhakikisha kuwa kila mtoto wa kike na kiume anamaliza shule ya msingi.

Ingawa tatizo la ajira ya watoto limepunguka kwa asili mia 20 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita,barani Afrika hilo bado ni tatizo kubwa hasa katika nchi zilizo kusini ya jangwa Sahara,ambako watoto mara nyingi hutumiwa kufanya kazi mashambani.

Kwa maoni ya mratibu wa masuala ya kisheria wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels,lazima ziwepo sheria za kulazimisha makampuni kutoa dhamana kuwa hazitumii ajira ya watoto.Mratibu Ruth Casals anaamini kuwa Umoja wa Ulaya una wajibu wa kiadilifu,kuyazuia makampuni ya Ulaya kupata faida kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu.