1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa kusitishwa kwa mapigano Syria watolewa

Admin.WagnerD11 Septemba 2018

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan De Mistura amekutana na maafisa wa Urusi, Iran na Turkey leo Jumanne kutafuta uungaji mkono wa mazungumzo kati ya Syria na pande zinazotofautiana.

https://p.dw.com/p/34gnE
Russland Sotschi Staffan de Mistura, UN-Sondergesandter für Syrien
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan De MisturaPicha: picture-alliance/dpa/M. Tereshchenko

De Mistura anataka uungaji mkono kutoka Urusi na Iran, mataifa ambayo yanamuunga mkono Rais wa Syria Bashar al-Assad, na kutoka Uturuki, ambayo inawaunga mkono waasi, ili kuanzisha mazungumzo ya amani yakiwemo yanayohusu katiba mpya ya Syria. Ajenda ya kisiasa ya mkutano mjini Geneva ulifunikwa na matukio ya kijeshi katika eneo la mwisho lililokuwa limeshikiliwa na waasi la Idlib nchini Syria, ambalo limeshuhudia mashambulio kutoka kwa majeshi ya Syria na wale wa Urusi katika siku za hivi punde.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa takriban watu elfu thelathini wamelazimika kutoroka vita Idlib mwezi huu pekee. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameiomba Marekani na Umoja wa Ulaya, pamoja na mataifa ya Urusi na Iran, kuzuia mashambulizi ya kijeshi katika eneo la Kaskazini Magharibi ambayo inapakana na Uturuki.

Msemaji wa ofisi ya ushirikishi ya masuala ya kibinadamu Jens Laerke anasema,´´ Ninasikitishwa na mashambulio katika eneo la Kaskazini Magharibi ya Syria, ambao umesababisha vifo vya raia wengi. Kutaabika kwa raia kumechangiwa na mashambulio katika vituo vya afya. Chini ya wiki moja, hospitali nne eneo la Idlib zimeshambuliwa.´´

Syrien Idlib Luftangriffe der Regierungskoaliltion
Picha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Idlib ni makazi ya watu milioni tatu na inadhibitiwa na muungano wa Kiislamu kwa jina Hayat Tahrir al-Sham HTS, kundi linalohusishwa na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda. Rais Erdogan aidha ameyataka mataifa ya Urusi na Iran kusitisha kile alichokitaja kuwa janga la kibinadamu katika eneo la Idlib akisema raia wa Syria wanaoishi eneo hilo hawawezi kuachwa katika mikono ya Rais Bashar al-Assad.

Mataifa ya Magharibi yatakiwa kuwajibika

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye jarida la Wall Street, Erdogan amesema mataifa ya Magharibi yana jukumu la kusitisha umwagikaji damu upya lakini utawala wa Urusi na Iran vile vile wana jukumu la kukomesha janga la kibinadamu.

Matamshi yake yanajiri siku nne baada ya kukutana na wenzake wa Urusi na Iran katika kongamano mjini Tehran, ambapo Erdogan alitaka kuepusha shambulio la umwagikaji damu eneo la Idlib. Wachambuzi wanasema kwamba Erdogan alishindwa kuafikia lengo lake katika kongamano hilo, na matamshi yake yanaonekana kuongeza wasiwasi nchini Uturuki kwamba Iran na Urusi hayana nguvu dhidi ya Assad.

Wakati Uturuki ikitajwa kuwa mojawapo ya wanaowaunga mkono waasi nchini Syria na kuitisha kuondolewa kwa Assad, nchi hiyo hadi sasa imefanya kazi kwa karibu na washirika wa Assad ambao ni Urusi na Iran kutafuta suluhu ya mapigano. Wakati uo huo Rais Erdogan amekosoa hatua ya Rais Assad kuhalalisha mapigano Idlib kama oparesheni ya kukabiliana na magaidi.

Türkei Grenze - Syrische Flüchtlinge
Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Ikumbukwe Uturuki imewapokea zaidi ya wakimbizi milioni tatu kutoka Syria na kwamba inahofia kwamba mapigano zaidi huenda yakachangia ongezeko la wakimbizi milioni mbili zaidi kutoka Idlib. Mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe yamesababisha vifo vya watu elfu 350 tangu mwaka 2011.

 

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE/DPAE

Mhariri: Josephat Charo