1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfsburg yaongoza bado Bundesliga

17 Aprili 2009

Chelsea ina miadi na Arsenal katika nusu-finali ya FA

https://p.dw.com/p/HZ5L
Wolfsbur kileleni:Picha: picture-alliance / Pressefoto ULMER / Lukas Coch

Wolfsburg ina kibarua kigumu leo ikijaribu kunyakua pointi 3 nyengine nyumbani kubakia kileleni mwa Bindesliga. Hamburg iliokata pamoja na Bremen tiketi ya nusu-finali ya Kombe la ulaya la UEFA ,iko nafasi ya pili ikiwa pointi sawa na mabingwa Bayern Munich.Katika dimba la Uingereza, macho yanakodolewa mpambano wa nusu-finali wa Kombe la FA baina ya Arsenal na Chelsea-timu 2 kati ya 3 za Uingereza zilizokata tiketi zao za nusu-finali ya Kombe la ulaya la klabu bingwa-champions league baada ya kutlewa Liverpool.

Wolfsburg,viongozi wa Bundesliga Wolfsburg wanataka kwa kila hali, kuondoka na pointi 3 nyumbani jioni hii ili kubakia kileleni.ili kutimiza shabaha hiyo, wanabidi kutamba jioni ya leo nyumbani mbele ya timu pekee iliothubutu kuilaza Wolfsburg msimu huu-Bayer Leverkusen.Leverkusen , inajikuta wakati huu nafasi ya 9 ya ngazi ya Ligi ,lakini ikiwa na washambulizi wakali kama Patrick Holmes na stefan Kiesling, inaweza kuwatia tena munda viongozi hao wa Ligi.

Bayern Munich, mabingwa wananyatia sasa kutoka nafasi ya tatu ingawa wako pointi sawa na Hamburg yenye miadi kesho na hannover,majirani zao wa kaskazini.Hertha Berlin wanacheza na Bremen ambao kama hamburg wametia mfukoni tiketi yao ya nusu-finali wiki hii ya kombe la ulaya la UEFA.

Changamoto nyengine za Bundesliga ni kati ya Armenia Bielefeld na mabingwa Bayern Munich; cologne na stuttgart,Karlsruhe SC inacheza na Hoffenheim.Bochum ina miadi leo na Borussia Dortmund wakati schalke ilikuwa uwanjani Ijumaa ilipocheza na Energie Cottbus.

Huko Uingereza mbali na nusu-finali ya Kombe la FA kati ya Arsenal na Chelsea, mapambano ya Premier League leo ni kati ya Aston villa na West Ham united.Middlesbrough inacheza na Fulham .portsmouth ina miadi na Bolton Wanderes.Stoke City imejiwinda nyumbani kwa changamoto na Blackburn Rovers wakati wenzao Sunderland wanawapokea wageni wao Hull City.Kati ya wiki hii,Uingereza imetia timu 3 tena ,katika nusu finali ya Kombe la klabu bingwa la ulaya:Mabingwa Manchester united, Chelsea ilioitoa Liverpool na Arsenal iliotamba mbele ya Vilarreal.

Huko Spain , viongozi wa Ligi FC Barcelona -timu pekee itakayozima vishindo vya timu 3 za Uingereza katika champions league, inaitembelea Getafe na akina Samuel Eto-o na Lionel Messi, wameazimia kuridi huko na pointi 3.Mahasimu wao katika la Liga-Real Madrid wanacheza na Recreativo Huelva wakati malaga iko nyumbani ikiipokea Real mallorca.Atletico Madrid inacheza na Numancia .kalenda ya La Liga mwishoni mwa wiki hii inakamilishwa na mpambano baina ya Athletico Bilbao na Deportivo la coruna.

Kesho, Espanyol itapambana na Racing Santander wakati Real Valladolid mahasimu wao ni Villareal waliotimuliwa nje ya champions League na Arsenal.Valencia wana kibarua kigumu kesho nyumbani watapopambana na Sevilla.

Ligi ya Itali -au serie A, leo ni zamu ya Genoa kuchuana na Lazio Roma wakati Juventus wanapamnbana na Inter Milan.Kesho AS Roma wanacheza na Lecce wakati Atalanta Bergamo wanakutana na Reggina.Cagliari inacheza na Napoli.Udinese iliotolewa nje ya nusu-finali ya kombe la ulaya la UEFA na Bremen ya Ujerumani inaikaribisha nyumbani Fiorentina.AC Milan inacheza na Torino.

Baada ya timu zitakazocheza nusu-finali ya kombe la ulaya la klabu bingwa kujulikana:Manchester united,mabingwa, Chelsea na Liverpool kutoka Uingereza na FC barcelona viongozi wa Ligi ya Spain, pia katika Kombe la ulaya la UEFA timu 4 za nusu-finali zinajulikana: Mbili zatoka Ujerumani na 2 Ukraine:Dynamo Kiev na Donetsk zinacheza mara ya kwanza nusu-finali ya Kombe hilo .Kutoka Ujeruman i ni Hamburg na Werder Bremen.

Hamburg imeweka miadi na majirani zao wa kaskazini Werder Bremen licha ya kwamba, walilazwa mabao 2-1 na Manchester City hapo juzi wakati klabu 2 za Ukraine Donetsk na Dyynamo Kiev zilipiga hatua hiyo kwa Kiev kuitimua Paris St.Germain mabao 3:0 . Kocha wa Hamburg, Martin Jol alisema timu yake ilionesha kukomaa kiakili na ndio ufunguo wa ushindi wake mbele ya Manchester city.Hamburg imeiwacha nyuma Manchester city kwa mabao 4-3 kutoka duru zote mbili.Brtemen ilitoka sare mabao 3:3 na Udinese ya Itali na imeingia nusu finali kwa ushindi jumla wa mabao 6-4.

Diego wa Brazil alikuwa ufungo tena wa ushindi wa Werder Bremen kwani aliwioka katika mapambano yote 2 nyumbani na nje ya Bremen.Hata Claudio Pizzaro alitia bao na sasa swali ni timu gani moja ya Ujerumani na nyengine ya Ukraine zitakutana katika finali ya Kombe hili.Wakati huu Hambuirg inatamba zaidi ya Bremen katika Bundesliga ,lakini Bremen ikiwa na washambulizi hatari kama Diego na Pizzaro , wanay kila uwezo wa kuwasangaza majirani zao Hamburg.

Pizzaro kutoka Peru, amekuwa akigonga vichwa vya habari nje ya uwanja : na jana Mahkama kuu ya kimataifa ya michezo mjini Geneva, Uswisi, ilifuta faini aliopigwa mperu huyo na shirikisho la dimba la Peru kwa tuhuma za kuvunja nidhamu katika hoteli moja mwaka mmoja na nusu uliopita. Kufuatia rufaa aliokata Pizarro mwaka jana ,Mahkama hiyo iliifuta adhabu ya faini ya dala 80,000 na kusimamishwa kucheza kwa mwaka na nusu .Hii ilifuatia wachezaji kadhaa kutuhumiwa kuvunja nidhamu baada ya Peru kutoka sare bao 1:1 na Brazil katika kinyanganyiro cha kuania tiketi za Kombe la dunia.Adhabu hiyo baadae, ilipunguzwa kutoka miezi 18 na kuwa miezi 3 na faini ya dala 10.000 badala ya dala 80.000. Mahkama jana ilifuta adhabu zote hizo. Mwaka huu, Pizzaro hakuichezea Peru kwa kuhofia adhabu hiyo.

Muandishi: Ramadhan Ali

Mhariri : M.abdul-Rahman

DPAE/AFPE