1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WTO yahofia mustakabali wake Trump akirudi madarakani

Saumu Mwasimba
26 Februari 2024

Mkutano wa Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) umefunguliwa Abu Dhabi kwa wanachama kuhimizwa kukumbatia mageuzi, wakati shirika hilo likihofia mustakabali wake ikiwa Donald Trump atarejea madarakani nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/4cswB
Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Ngozi Okonjo-Iweala.
Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Ngozi Okonjo-Iweala.Picha: Britta Pedersen/dpa/picture alliance

Mkutano huo wa kilele unaofanyika kila baada ya miaka miwili ulifunguliwa rasmi siku ya Jumatatu (Februari 26) mjini Abu Dhabi kwa kauli za kuuonya ulimwengu juu ya wasiwasi uliopo katika uchumi wa dunia kufuatia vita na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Pamoja na kwamba shirika hilo linakabiliwa na shinikizo kutoka Marekani na mataifa mengine, mkuu wake, Ngozi Okonjo-Iweala alilipongeza akizitaka nchi wanachama kukumbatia mageuzi katika wakati ambapo chaguzi zinazotarajiwa katika mataifa mbalimbali huenda zikasababisha changamoto mpya.

Okonjo-Iweala alizungumzia kuhusu hatari zinazoweza kuukabili uchumi wa ulimwengu katika kiwingu cha kushuhudiwa kupanda kwa bei za vyakula, nishati na mahitaji mengine muhimu kutokana na hali za kisiasa.

Alikiri kwamba watu kila mahala wana wasiwasi kuhusiana na hatma ya maisha na hili litaonekana dhahiri kupitia chaguzi zitakazofanyika mwaka huu.

Ngozi Okonjo-Iweala, mkurugenzi mkuu wa WTO.
Ngozi Okonjo-Iweala (wa pili kushoto) akiwa na viongozi wengine katika mkutano ulioitishwa na Ujerumani mwaka 2022.Picha: Carsten Koall/Getty Images

"Tusijifanye tunajua kila kitu kitakuwa rahisi. Ikiwa tulidhani ulimwengu ulikuwa katika hali ngumu mwezi Mei mwaka 2022, wakati tulipokuwa tunajikwamuwa taratibu kutokana na janga la korona na vita vya Ukraine kutokana na kukosekana usalama wa chakula na nishati, basi tuko katika hali ngumu zaidi hivi sasa." Alisema mkuu huyo wa WTO, akiongeza kwamba kuna mashaka na ukosefu wa uthabiti kila mahala.

Ongezeko la mivutano ya kisiasa

Akionesha wasiwasi wake juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa mivutano ya kisiasa ya kikanda, Okonjo-Iweala alisema "migogoro imesambaa kama tunavyoshuhudia hapa Mashariki ya Kati na katika maeneo mbalimbali ya Afrika na nchi nyingine za Kiarabu, ambayo haiangaziwi kwenye vyombo vya habari."

Makao makuu ya WTO mjini Geneva nchini Uswisi.
Makao makuu ya WTO mjini Geneva nchini Uswisi.Picha: Lian Yi/Xinhua/picture alliance

"Hatupaswi kusahau mgogoro nchini Sudan ambao umewaacha takribani watu milioni 8 bila makaazi ndani na nje ya mipaka yake au mgogoro katika Mashariki mwa Kongo.'' Alionya.

Mkuu huyo wa WTO aliweka wazi kwamba kwa shirika hilo, uchaguzi wa rais nchini Marekani utakaofanyika Novemba 5 ndio muhimu zaidi.

Hofu ya ushindi wa Trump

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, ambaye mara hii anagombea tena kiti hicho, aliwahi kutishia kuiondowa nchi yake katika shirika hilo na mara kadhaa alikuwa akitangaza hatua za kuongeza viwango vya kodi kwa  bidhaa kutoka mataifa yaliyotazamwa kuwa washirika wa Marekani na hata yale yaliyokuwa mahasimu.

Mgombea mtarajiwa wa urais wa Marekani kupitia chama cha Republican, Donald Trump.
Mgombea mtarajiwa wa urais wa Marekani kupitia chama cha Republican, Donald Trump.Picha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

WTO inahofia kuwa ushindi wa Trump huenda utamaanisha kitisho katika biashara duniani.

Hata hivyo, hata ikiwa rais wa sasa, Joe Biden, atarudi tena madarakani, Marekani kwa ujumla wake hairidhishwi kwa kiasi kikubwa na shirika hilo lililoanzishwa miaka 75 iliyopita.

Marekani pia inaikosoa China kwa kuendelea kujiita nchi inayoendelea kama ilivyokuwa mwaka ilipojiunga na WTO mwaka 2001.

Katika mkutano huo wa Abu Dhabi, mataifa wanachama yatajadili mpango wa kupiga marufuku ruzuku ambazo zinachangia uvuvi wa kupitiliza, kurefusha hatua ya kusitisha kodi katika majukwaa ya kidijitali kama vile ile inayotowa burudani ya filamu na michezo ya kompyuta na vile vile watajadili pia masuala ya kilimo.

Katika kikao cha ufunguzi, visiwa vya Komoro na Timor Mashariki zimejiunga na shirika hilo na kulifanya sasa kuwa na wanachama jumla ya 166.