1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Yemen: Watu 53 wauawa katika mapigano kuwania mji wa Marib

Daniel Gakuba
10 Aprili 2021

Mapigano ya kuwania jimbo muhimu la Marib nchini Yemen yamepamba moto Jumamosi yakisababisha vifo vya wapiganaji 53 wanaoiunga mkono serikali na waasi wa Houthi katika muda saa 24 zilizopita.

https://p.dw.com/p/3rp1W
Jemen Waffenruhe
Picha: Getty Images/N.Hassan

Jeshi la serikali ya Yemen kwa msaada wa Saudi Arabia na washirika wake wanapigana vikali kuulinda mji wa Marib ambao ni makao makuu ya mkoa muhimu kwa nishati ya mafuta.

''Waasi wa Houthi wamelikamata eneo dogo katika mapigano ya karibuni'' katika mji huo wa kaskazini-mashariki mwa mji wa Marib, kimearifu chanzo kimoja kutoka upande wa serikali, kwa maana kwamba mji wenyewe haukuwa ukikabiliwa na kitisho.

Soma zaidi: Oman yasema muafaka wa Yemen upo njiani

Chanzo hicho cha upande wa serikali kimesema kuwa wanajeshi wake 22 walikuwa miongoni mwa waliouawa, huku wengine 31 wakiwa ni kutoka upande wa Wahouthi.

Kwa kawaida upande wa Wahouthi huwa hautoi taarifa kuhusu wapiganaji wake wanaouawa.

Wahouthi waendelea kuimarika tangu kuuteka mji mkuu

Mwaka 2014 waasi hao wanaoungwa mkono na Iran waliukamata mji mkuu wa Yemen, Sanaa, ulioko umbali wa KM 120 magharibi mwa mji wa Marib unaogombaniwa sasa.

Ölraffinerie Jemen
Mkoa wa Marib ni muhimu kwa kuwa una utajiri wa mafutaPicha: picture-alliance/dpa/epa Yahya Arhab

Hatua hiyo ya kuukamata mji mkuu iliifanya Saudi Arabia na washirika wake kuingilia kati mnamo Machi 2015, kwa azma ya kuiunga mkono serikali ya Yemen inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Wapiganaji wa upande wa serikali wamesema kuwa ndege za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia zimeshambulia ngome za waasi, lakini waasi hao wamejibu mapigo.

Soma zaidi: Waasi wa Kihouthi wafanya mashambulizi zaidi nchini Saudi Arabia

Tangu mwezi Februari waasi wa Houthi wamekuwa wakijaribu kuchukua udhibiti wa jimbo la Marib lenye utajiri mkubwa wa mafuta na ngome muhimu ya mwisho kwa serikali ya Yemen kaskazini mwa nchi hiyo.

Serikali yapigana kufa na kupona kubakia Marib

Ikiwa mji huo utaangukia mikononi mwa Wahouthi litakuwa pigo kubwa kwa serikali ya Yemen ambayo kwa sasa inayo makao yake katika mji wa Aden, na pia kwa washirika wake wanaoongozwa na Saudi Arabia.

Jemen Sanaa | Mann füllt Container mit Wasser
Mapigano yanayoshamiri yanazidisha matatizo ya kibinadamu YemenPicha: Mohammed Mohammed/Xinhua/picture alliance

Shughuli za msaada wa kibinadamu pia zitaathirika pakubwa, kwa sababu watu wengi walioyapa kisogo makaazi yao walihamia katika kambi zilizojengwa katika mkoa wa Marib.

Zipo kambi zipatazo 140 zilizotapakaa katika mkoa huo, zikiwahifadhi wakimbizi takribani milioni 2, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Yemen.

Mnamo miezi ya hivi karibuni waasi wa Houthi wamekuwa wakizidisha mashambulizi dhidi ya Saudi Arabia wakitumia ndege zisizo na rubani, wakishinikiza kufunguliwa kwa anga ya Yemen pamoja na bandari zake.

Soma zaidi:  Umoja wa Mataifa waonya mzozo wa Yemen umeongezeka

Wakati huo huo, waasi hao wamekataa wito wa Saudi Arabia wa kutaka makubaliano ya kusitisha mapigano.

Mwezi Machi wapiganaji 90 waliuawa wakati pande hizo hasimu walipopambana magharibi mwa mji wa Marib.

Umoja wa Mataifa ulilaani kuongezeka kwa uhasama, na ulitoa tahadhari juu ya janga la kibinadamu linaloweza kufuata.

 

afpe