1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zadi ya watu 90 wauwawa Baghdad

3 Julai 2016

Watu zaidi ya 90 wameuwawa Jumapili (03.07.206) katika miripuko miwili ya mabomu mjini Baghdad likiwemo shambulio kubwa linalodaiwa kufanywa na kundi la Dola la Kiislamu llilouwa watu zaidi ya 86 wakiwemo watoto 15.

https://p.dw.com/p/1JIK4
Picha: Reuters/Khalid al Mousily

Takriban watu zaidi ya 90 wameuwawa Jumapili (03.07.206) katika miripuko miwili ya mabomu katika mji mkuu wa Iraq likiwemo shambulio kubwa linalodaiwa kufanywa na kundi la Dola la Kiislamu ambalo limeuwa watu zaidi ya 86 wakiwemo watoto 15.

Miripuko hiyo imeonyesha uwezo wa wanamgambo hao wa itikadi kali kufanya mashambulizi ya kiwango kikubwa licha ya kushindwa katika mapambano makubwa ikiwa ni pamoja na kuupoteza mji wa Fallujah ambao serikali imetangaza kuwa umekombolewa kikamilifu kutoka kundi la Dola la Kiislamu wiki moja tu iliopita.

Shambulio lililosababisha maafa makubwa limetokea katika wilaya ya Karada ilioko katikati ya mji mkuu wa Baghdad ambapo mshambuliaji aliliripuwa lori lake lililokuwa limesheheni miripuko nje ya kituo cha maduka na kuuwa watu 86 na kujeruhi wengine 170.Kwa mujibu wa afisa wa polisi miongoni mwa waliouwawa ni watoto 15,wanawake 10 na polisi sita.

Mripuaji huyo wa kujitowa muhanga alijiripuwa muda mfupi baada ya kuigia saa sita usiku wakati familia na vijana zilipokuwa nje mitaani baada ya kufuturu kutoka saumu ya mchana kutwa kwa ajii ya mwezi mkutukufu wa Ramadhan.Maafisa wanasema wengi ya waliouwawa walikuwa kwenye jengo la maduka la ghorofa na eneo la kujipumbaza ambapo wengi waliteketea kwa moto na wengine kukosa pumzi.

Muda mfupi baadae kundi la Dola la Kiislamu lilidai kuhusika na mripuko huo katika taarifa walioyoiweka kwenye mtandao ambapo imesema iliwalenga makusudi Waislamu wa madhehebu ya Shia.Shirika la habari la AP halikuweza kuyakinisha ukweli wa taarifa hiyo lakini iliwekwa kwenye tovuti ambayo kwa kawaida hutumiwa na watu wenye itikadi kali.

Taharuki katika eneo la tukio

Katika eneo la tukio wazima moto na wananchi wameonekana wakizibeba maiti ambazo zimefunikwa na mablankenti na mashuka. Moshi ulikuwa umeligubika jengo hilo la maduka ambalo lilikuwa limezungukwa na mabaki ya gari yaliyoteketea na vibanda vya biashara.Kundi la wanawake lilikuwa limeketi sakafuni likiwalilia vipenzi vyao.

Hali baada ya shambulio la kigaidi Baghdad.
Hali baada ya shambulio la kigaidi Baghdad.Picha: picture-alliance/dpa/A. Abbas

Katika shambulio la pili bomu lililotengenezwa kienyeji limeripuka kaskazini mwa Baghdad katika eneo la Shaab na kuuwa watu watano na kujeruhi wengine 16. Hakuna kundi lililodaia kuhusika na shambulio hilo lakini lina alama ya wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu ambao mara nyingi hulenga wilaya za kibishara na maeneo ya Washia.

Idadi kubwa ya maafa inalifanya shambulio hilo kuwa la maafa makubwa kutokea katika mj huo mkuu mwaka huu.Hapo tarehe 11 mwezi wa Mei wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu (IS) waliripuwa magari matatu yaliyotegwa mabomu mjini Baghdad na kuuwa watu 93.

Abadi azomewa

Masaa machache baada ya kutokea kwa miripuko ya Jumapili Waziri Mkuu wa Iraq Haider al Abadi na wabunge walilitembelea eneo la tukio ambapo video zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha umma wenye ghadhabu ukimwita al-Abadi "mwizi" na kuuzomea msafara wake.Mashuhuda wamesema umati huo ulilirushia gari la al-Abadi mawe,viatu na mapipa ya plastiki.

Moto ukiteketeza eneo la maduka baada ya shambulio la kigaidi Baghdad.
Moto ukiteketeza eneo la maduka baada ya shambulio la kigaidi Baghdad.Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Mohammed

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Iraq Jan Kubis amesema shambulio la Karada ni la woga na kukihirisha lisilo methali na ameitaka serikali ya Iraq kuongeza juhudi za usalama kuwalinda wananchi wa Iraq wakati wa sherehe za Eid-al-Fitry ambazo zinaadhimisha kumalizika kwa mwezi wa Ramadhan.

Amesema wanamgambo wa IS ambao wamekuwa wakipata vipigo na kushindwa katika medani za mapambano wanalipiza kisasi kwa kuwashambulia raia wasiokuwa na hatia.

Kundi la Dola la Kiislamu bado linadhibiti mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Mosul na maeneo makubwa ya ardhi kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri : Yusuf Saumu