1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZAPCO, Ation-aid zataka bei bora ya Karafuu

Christopher Buke16 Oktoba 2006

Serikali ya Mapinzuri kupitia ZSTC yashaurikuwa kujitoa uuzaji Karafuu

https://p.dw.com/p/CHmM

Uzalishaji wa zao la Karafuu visiwani Zanzibar umeporomoka kwa kiwango kikubwa na wakulima wa zao hilo visiwani humo wanaibebesha lawama moja kwa moja Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar SMZ.

Katika warsha maalumu ambazo zinaendeshwa na Chama cha wakulima wa Karafuu Zanzibar ZACPO wakifadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Action Aid wakulima hao hawajamung’unya maneno bali wamesema bayana kuwa “hakuna haja ya kutafuta mchawi wa kwa nini Karafuu imeporomoka” bali serikali imesababisha hali hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Masoko wa ZACPO Bwana Rehari Salim uvunaji wa karafuu umepungua kutoka tani 25,000 kwa msimu mwaka 1978 hadi tani 5 hivi sasa. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za utafiti uliofanywa na Taasisi ya SMZ inayohusinana na mauzo ya Karafuu ZSTC.

Sababu zinazotolewa na taasisi hiyo ya Zanzibar State Trading Corp oration za kuporomoka uzalishaji wa Karafuu ni Mvua chache na zisizonyesha kwa msimu, Mikarafuu mingi kuzeeka wakati wakulima hawapandi mikarafuu mipya na Magendo ya biashara hiyo nje ya nchi.

Wakulima katika warsha hiyo wanakubali uzalishaji wa Karafuu umepungua mno lakini zaidi wao wakidai ni kutokana na SMZ kuhodhi uuzaji pekee wa zao hilo nje ya nchi lakini bila kuwalipa wakulima malipo yanayoridhisha.

Akizungumza kwa niaba ya Wakulima wa zao hilo Naibu Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazalishaji Karafuu Zanzibar ZAPCO Bwana Ally Mhaji Haji, alisema hali hii inarudisha nyuma hata heshima ya Zanzibara akidai “kama karafuu hatuiendelezi basi ZNZ haijawa”.

Alisema kumekuwa na matukio mengi ya wakulima kuikata mikarafuu yao kutokana na mfumo uliopo, akifafanua kuwa pale baadhi ya wakulima wanapokamatwa na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi wakati mwingine kufungwa au kupewa adhabu kali pale wanapokuwa wakijaribu kupeleka mazao yao nje ambapo hupata alau malipo mazuri.

Anaongeza kuwa pale wanaporudi au kuachiwa au kumaliza adhabu zao huamua kuikata mikarafuu yao.

“ Mikarafuu imepotea, mikarafuu inachanjwa kuni, mtu akipata misuko-suko kidogo akisafarisha nje kwa magendo akikamatwa basi akirejea anasema hii mikarafuu, ndiyo iliyonisababisha nimi kufungwa, anafika anaikatilia mbali, anasema mkarafuu wangu mwenywe nimeupanda mwenye leo hii unanifungisha” anasisitiza Bwana Haji mbele ya wakulima na viongozi wa SMZ.

Kwa upande wake mwakilishi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika mkutano huo Abdallah Mwinyi Khamis ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi aliunga mkono moja kwa moja hoja ya kuwa sifa ya Zanzibar haiwezi kutenganishwa na Karafuu.

“ Kuna nchi zinatajikana kwa sababu ya uchumi wake, kuna nchi zinatajikana kwa sababu ya wema wa watu wake, kuna nchi zinatajikana labda kwa sababu ya ubaya wake, sasa Zanzibar ni Karafuu, na karafuu ni Zanzibar, kwa sababu hapo ndipo zilipoanza”.

Lakini wakati akisema hayo wakulima wangali wakiinyoshea kidole serikali kuwa imekuwa kama kizingiti cha kuwazuia wasipate bei bora kwa zao lao. Akizungumza na waandishi wa habari juu ya madai hayo Bwana Abdalah aliivua lawama serikali yake akidai kuwa kupungua bei ya zao la Karafuu inatokana na mwenendo wa bei ya zao hilo katika soko la dunia.

Badala yake anatoa mwito kwa wakulima wazidi kutunza mikarafuu kwani siku bei ikipanda katika soko la kimataifa nao watanufaika badala ya kuanza kupanda zao hilo.

“ Maana (Mikarafuu) ni kama mwanamke. Mtunze uzuri ndio azae, maana mwanamke akishafika umri mkubwa, anakuwa hazai tena, uko umri mtu hazai sasa tunahimizana kwamba tuipande mikarafuu mipya, tuitunze tuilimie, kwa sababu jina la Zanzibar lipo na Zanzibar ni karafuu na karafuu ni Zanzibar”.

Akiteta na waandishi wa habari mara baada ya mgeni huyo wa serikali ya SMZ kuondoka kwenye ukumbi wa mkutano Bwana Haji hakuonekana kukubaliana moja kwa moja na hoja za serikali. Yeye anadai licha ya sababu za soko la dunia lakini ungalipo mkono wa mtu.

“ Wapo watu wamekalia hapa hili suala la biashara, na dunia sasa hivi ni utandawazi. We ukikalia hapa dunia inasema soko liko hivi, hasa mzalishaji anamwambia bei iko hapa, soko linazungumza hivi, katika utandawazi”.

Michango ya mawazo iliyotolewa na wanachama wa chama cha wakulima wa zao hilo inadhihirisha nao hawakubali kuwa makali waliyonayo ya bei hafifu ya zao lao inasababishwa na soko la zao hilo kimataifa pekee.

Wanadai nchini Kenya zao hilo linauzwa hadi shilingi 6,000 wakati wao wanalipwa sh. 2,000 kwa korosho daraja la kwanza. Wanajoho wafanyabiashara hao “Kenya wanaiuza wapi karafuu baada ya kuinunua kwa bei hiyo”?

Baadhi ya wakulima kama Bi Tunza Ally Ali ambaye ni mwakilishi wa vikundi vya akina mama alitoa mwito SMZ kwa kupitia ZSTC iachie udhibiti wa bei na ununuzi wa zao hilo na kazi hiyo ifasimamiwe na kuendeshwa na wakulima wenyewe.

Anahisi kufanya hivyo wakulima watapata kipato kikubwa na hali hiyo itahamasisha wakulima wa Karafuu “ na mapato yatangazwe kwenye vyombo vya habari ili ihamasishe walikuma”.

Lakini licha ya sababu za bei hata idara mbalimbali za SMZ zimetajwa tena na wakulima kuwa zinadumaza maendeleo ya zao la Karafuu.

Bwana Rashid Zubeir mkulima wa karafuu eneo la Kihanga anatoa mfano wa jinsi Halmashauri ilivyogawa viwanja maeneo maalumu ambapo karafuu hiyo inasitawi badala ya kutenga eneo lingine kwa ajiri ya ujenzi.

Anadai sio sahihi kufanya hivyo kwani sio kila eneo karafuu inasitawi bali ni kwenye maeneo maalumu.

Lakini pia anadai Idara ya kilimo imechangia kufisidi zao hilo kwa kupanda miti kwenye maeneo yaliyokuwa yakioteshwa na kupandwa mikarafuu akiyataja maeneo hayo kuwa ni Misingini, Kitope, Chahani, Kizimbani sehemu ya Kijichi.

Wachangiaji wengine walidai kuwa umasini mkubwa unaowakumba hivi sasa wananchi wengi visiwani Zanzibar unatokana na madhila ya kuporomoshwa kwa makusudi kipato cha karafuu kwa wananchi.

Bwana Khamis Muhamed Mkulima wa karafuu kwenye visiwa vya Pemba ambaye anasema alilazimika kuhamia Unguja alianza kulima zao hilo tangu mwaka 1956 anasema siku zilizopita Karafuu lilikuwa zao la kutumainiwa.

“ Sikuoa, sikuozesha, sikutahiri, sikufanya jambo lolote hata karafuu iingie! lakini sasa tutizame nani adui wa Karafuu, leo”. Analalama Mkulima huyo.

Lakini mkulima huyo akashukuru kuwa ni hatua kubwa iliyofikiwa hasa akilishukuru shirika la Action aid kuwa imewezekana sasa wakulima wanaweza alau kujadili juu ya machungu waliyo nayo dhidi ya bei hafifu ya zao lao.

ZSTC huuza zao hili zaidi katika nchi za Asia na Mashariki ya kati maana soko la karafuu katika nchi za Jumuia ya Ulaya limekuwa si zuri kutokana na kudaiwa kuwa ubora wa Karafuu ya Zanzibar unapungua kila uchao.

Wakati wa majumuisho Bwana Lawrence Wambura, afisa mwandamizi wa Action-aid alisema ametiwa moyo na semina hizi kwani pande mbili yaana Serikali kwa upande mmoja na wakulima kwa upande mwingine wameweza kukaa pamoja na kujadiliana.

“Watu wamekuwa huru kuzungumzia karafuu tofauti na zamani” anasisitiza Wambura na kuongeza “ huo ni mwanzo mzuri”.

Zao la karafuu linachangia takliban asilimia 80 ya pato lote linaloingizwa serikali kutokana na mazao ya kilimo na pia inachangia asilimia 20 ya pato lote la jumla la serikali ya mapindizu ya Zanzibar.

Tangu mkarafuu kupandwa hadi kuvunwa huchukua kipindi cha muda wa tangu miaka 5 hadi 7.

Lakini wataalamu wa zao hilo wanaasa kuwa lazima mti huo upewe uangalizi na uangalifu unaotakikana hasa palizi na kuulishia mbolea za aina mbalimbali zinazotakikana hasa samadi.

Semina hii inaendeeshwa na na kufadhiliwa na shirika la kimataifa la Action Aid chini ya mpango maalum wa shirika hilo uliobatizwa jina la “ONDOA UMASIKINI TANZANIA”.

Falsafa ya shirika hili ni kuwa Tanzania sio masikini hasa zinapochunguzwa rasilmali za nchi hii bali ni tatizo la kisera na watoa maamuzi.

Mwisho.