1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky adai Urusi inajiandaa kwa mashambulizi makali

Sylvia Mwehozi
1 Aprili 2022

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema Urusi inaandaa "mashambulizi ya nguvu" katika maeneo ya mashariki na kusini mwa nchi ikiwemo mji wa Mariupol, licha ya ahadi ya Urusi kwamba ingepunguza mashambulizi yake.

https://p.dw.com/p/49Kcm
Ukraine | Zerstörung in Charkiw
Picha: Aziz Karimov/Zuma/picture alliance

Kwa zaidi ya mwezi mmoja tangu Urusi alipomvamia jirani yake, vikosi vya Moscow vimeharibu miji kama Mariupol kwa mabomu na kuua watu takribani 5000 katika mji huo pekee. Kwenye mazungumzo ya kusaka amani ya wiki hii, Urusi ilisema kwamba ingepunguza mashambulizi yake katika mji mkuu wa Kyiv na ule wa Chernigiv, lakini maafisa wa Ukraine na nchi za magharibi walikataa ahadi hiyo wakisema vikosi vya Moscow vinajipanga upya.

Katika hotuba yake aliyoitoa Alhamis usiku, Zelensky amedai kuwa "hiyo ni sehemu ya njama" za Urusi, akiongeza kwamba wanafahamu vikosi vya Urusi "vinaondoka katika maeneo ambayo vimeshindwa na kulenga maeneo mengine muhimu" yanayoweza kuwa changamoto kwa Ukraine. Rais Zelensky amesema hali katika maeneo ya kusini na mashariki kuwa" ngumu sana".

Ukraine Der Präsident Volodymyr Zelenskyy
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy Picha: Ukrainian Presidency via AFP

"Kuna maneno mengine kuhusu kile kinachotajwa kama kujiondoa kwa wanajeshi kutoka Kyiv na Chernigiv, kinachoelezwa kama kupungua kwa shughuli za wavamizi katika mwelekeo huu. Tunajua kuwa hii sio kujiondoa, lakini ni matokeo ya kufurushwa, matokeo ya kazi ya watetezi wetu. Lakini wakati huo huo, tunaona mkusanyiko wa wanajeshi wa Urusi kwa mashambulizi mapya huko Donbas."

Marekani kupitia afisa mwandamizi wa ulinzi imeunga mkono tathmini hiyo ikidai kwamba hatua ya Urusi kujielekeza zaidi Donbas kunaweza kuurefusha mgogoro. Wataalamu wa kijeshi wanaamini kwamba Moscow inajaribu kuachana na juhudi za kusonga mbele kwa wakati mmoja katika maeneo yote baada ya kupata upinzani mkali kutoka kwa jeshi la Ukraine ambao haukutarajiwa. Badala yake inataka kuanzisha eneo kubwa la ardhi kati ya Crimea ambayo iliikalia mwaka 2014 na maeneo mawili ya Donbas ya Donetsk na Luhansk ambayo inayaunga mkono.

Ukraine yawahamisha kutoka mji wa Mariupol uliozingirwa

Hayo yakijiri kampuni ya gesi ya Urusi, Gasprom, imesema hii leo inaendelea na usambazaji wake wa gesi barani Ulaya licha ya muda wa mwisho uliotangazwa na Rais Vladimir Putin wa kusimamisha ugavi, hadi pale wanunuzi watakapoanza kulipa kwa sarafu ya Urusi, Rubles.

Putin alitia saini agizo la kuweka tarehe ya mwisho ya Ijumaa kwa wanunuzi kutoka nchi "zisizo rafiki" kulipia gesi kwa kutumia sarafu hiyo ya Rubles au kukabiliwa na kitisho cha kukatiwa masharti ambayo nchi za Magharibi zimeyakataa kama jaribio la kuandika upya mikataba inayotaka malipo kwa euro.

Naye Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, ameanza mikutano na viongozi wa India mjini New Delhi baada ya kukutana na waziri mwenzake wa China, wakati Moscow ikijaribu kuyasogeza karibu mataifa yaliyo na nguvu barani Asia katikati mwa vikwazo vya magharibi. China na India ndio mataifa pekee makubwa katika ukanda wa Asia ambayo hayakulaani uvamizi wa Urusi mwishoni mwa Februari.

Vyanzo: AFP/Reuters