1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky asema wanajeshi wake wanakabiliwa na hali ngumu

Tatu Karema
20 Februari 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema vikosi vya nchi yake vinakabiliwa na hali ngumu katika mapambano yake na vikosi vya Urusi kwasababu ya kucheleweshwa kwa msaada wa kigeni

https://p.dw.com/p/4cbtW
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky (kulia) azungumza na kamanda wa vikosi vya ardhini vya Ukraine Oleksandr Syrsky (kushoto) wakati wa ziara yake mjini Izium eneo la Kharkiv mnamo Septemba 14, 2022
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky (kulia) azungumza na kamanda wa vikosi vya ardhini vya Ukraine Oleksandr Syrsky (kushoto)Picha: Ukrainian Presidential Press Off/ZUMAPRESS/picture alliance

Baada ya kuwatembelea wanajeshi wake wanaopambana na vikosi vya Urusi katika eneo la Kharkiv nchini Ukraine,  Zelensky amesema kuwa hali katika eneo hilo ni mbaya na vikosi vya Urusi vimejiwekea akiba kubwa ya silaha huku vikitumia kikamilifu fursa ya kucheleweshwa kwa msaada wa kigeni kwa Ukraine ambayo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa silaha na mifumo ya ulinzi wa anga.

Soma pia:Zelensky ahimiza msaada zaidi kwa ukraine, mkutano wa Munich

Jeshi la Ukraine pia limesema linakabiliwa na uhaba wa risasi na makombora, hali inayofanywa kuwa mbaya zaidi kwa kuzuiwa kwa kitita cha dola bilioni 60 za msaada kutoka Marekani.

Biden aelezea matumaini ya bunge la Marekani kupitisha msaada kwa Ukraine 

Siku ya Jumapili, Rais wa Marekani Joe Biden alimwambia Zelensky kwamba ana matumaini bunge la Marekani linalotawaliwa na chama cha Republican litaidhinisha msaada huo unaohitajika kwa dharura.

Soma pia:Vikosi vya Urusi vyasonga mbele uwanja wa vita mashariki mwa Ukraine

Wakati huo huo, waziri mkuu wa Ukraine Denys Shmygal amesema leo kuwa pia ana matumaini kwamba bunge hilo la Marekani litapitisha msaada huo litakapoanza tena vikao vyake baada ya kipindi cha mapumziko na kwamba nchi yake itaendelea kupambana katika mapigano hayo kwa msaada kutoka nje.

Urusi yarusha droni 23 kuelekea Ukraine

Jeshi la Ukraine limesema leo kuwa Urusi imerusha droni 23 kuelekea nchini humo usiku kucha kuamkia leo lakini mfumo wake wa anga ulifanikiwa kudungua mashambulizi hayo.

Rais wa Marekani Joe Biden akitoa taarifa kuhusu msaada wa dola bilioni 95 za msaada kwa Ukraine katika Ikulu ya White House mnamo Februari 13, 2024
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram, jeshi hilo limesema kuwa kutokana na operesheni za jeshi la Ukraine, droni zote aina ya Shahid ziliangushwa katika maeneo ya Kharkiv, Poltaba, Kirovohrad, Dnipro, Zaporizhzhia, Kherson na Mykolaiv.

Hata hivyo shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha ripoti ya jeshi hilo la Ukraine kwa njia huru. Pia hakukuwa na tamko la haraka kutoka Urusi.

Idara ya usalama ya Urusi FSB yamkamata mwanamke mmoja kwa kosa la uhaini

Idara ya usalama ya Urusi FSB katika mji wa Yekaterinburg ulioko eneo la katikati la Ural imesimamisha shughuli ilizoziita haramu za mwanamke mwenye umri wa miaka 33, mkazi wa Los Angeles mwenye uraia wa nchi mbili, na kumweka chini ya ulinzi.

Inasemekana kuwa mwanamke huyo ambaye hakutajwa jina, amekuwa akikusanya pesa ambazo baadaye zilitumika kununua vifaa vya matibabu na vya vita kama vile risasi kwa ajili ya vikosi vya kijeshi vya Ukraine.

Soma pia:Vikosi vya Ukraine vyajiondoa katika mji wa mashariki wa Avdiivka

Shirika la habari la serikali ya Urusi RIA Novosti, lilichapisha video kutoka kwa FSB ikiwaonesha maafisa waliokuwa wamevalia kofia wakimkamata mwanamke huyo.

FSB imesema kuwa mwanamke huyo amekuwa akifanya vitendo kinyume na usalama wa nchi hiyo na amekuwa akilisaidia jeshi la Ukraine wakati akiwaMarekani.

Kosa la uhaini linabeba adhabu ya kifungo cha maisha jela chini ya sheria iliyoimarishwa tangu kuanza kwa mashambulizi ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine.