1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Francis Sweden kushinikiza umoja

31 Oktoba 2016

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis yuko nchini Sweden kwa awamu ya mwisho ya mpango wake wa kuimarisha mapatano na umoja miongoni mwa wakristo.

https://p.dw.com/p/2Rvh0
Vatikan Papst Franziskus hält Pfingsrede vor dem Petersdom
Picha: picture-alliance/dpa/S. Spaziani

Papa Francis  yuko katika mji wa Lund Kusini mwa Sweden kwa ibada itakayoadhimisha mwanzo wa mwaka wa sherehe za kuadhimisha miaka 500 tangu kuanzishwa kwa mashauriano ya marekebisho hayo.

Hafla hiyo pia itaadhimisha miaka 50 ya mashauriano ya mapatano kati ya kanisa katoliki na lile la kilutheri, hali ambayo wakati mmoja haikuingiliana vyema na usimamizi na mafundisho ya Vatican.

Kwa kukubali kuhudhuria mashauriano hayo, Papa Francis amechukuwa hatua ambayo haingeweza kufikiriwa na wengi.

Viongozi wakuu wa kanisa Katoliki katika karne ya 16 walitumia fedha nyingi na wakati kurejesha nyuma marekebisho hayo yaliozinduliwa na mtawa wa kiume wa kijerumani Martin Luther alipopigilia misumari hoja zake 95 katika mlango wa kanisa huko Wittenberg mnamo Oktoba 31 mwaka 1517.

Mkutano wa leo unajiri miezi minane baada ya papa Francis kuwa baba mtakatifu wa kwanza katika muda wa takriban miaka 1000 kukutana na maaskofu wa madhehebu ya Orthodox.

Kiongozi huyo wa kanisa katoliki pia amelisogeza karibu kanisa la kiangalikana .

Na kabla ya mkutano wake wa leo nchini Sweden, alisisitiza umuhimu wa umoja wa wakristo wakati ambapo waumini wengi na imani ya kikristo inapokabiliwa na shinikizo nyingi katika sehemu nyingi za dunia.

Vatikan Papst Franziskus hält Pfingsrede vor dem Petersdom
Papa mtakatifu Francis akisalimiana na waumini Picha: picture-alliance/dpa/S. Spaziani

Alisema kuwa wakati wakristu wanaposhtumiwa na kuuawa, wanachaguliwa kwasababu ni wakristo na sio kwasababu ni wa madhehebu mbali mbali kama vile katoliki, anglikana, orthodox, Lutherani na madhehebu mengineyo.

Hata hivyo baadhi ya waumini wa kikatoliki wanatilia shaka iwapo kuna sababu yoyote ya kusherehekewa katika marekebisho hayo.

Kwasababu hiyo, kila neno katika mahubiri ya leo ya baba mtakatifu huko Lund yatafuatiliwa kwa makini ikiwa ni pamoja na matamshi ya Mounib Younan, Kiongozi wa wakfu kilutheri duniani ambaye ni mpalestina . Huku kanisa la kilutheri likiwa limeidhinisha wanawake kushikilia nyadhifa mbali mbali za uongozi wa kanisa hilo pamoja na kukubali ndoa za watu wa jinsia moja na kuweko kwa maaskofu mashoga, kanisa hilo lina uhuru ambao hauingiliani vyema na kanisa katoliki. Madhehebu hayo mawili pia yanatofautiana katika uongozi wake ,kwakuwa kanisa katoliki linafuata mpangilio wa matabaka ya uongozi huku la kilutheri likiwa halina mpaangilio maalumu.

Younan pia aliliambia shirika la habari la AFP kuwa angependa kuona wakati mmoja wakristo wakishiriki kwa pamoja katika kupokea sakramenti takatifu katika kuonyesha umoja wa wakristo swala ambalo kwa sasa linapingwa na kanuni za Vatican.

Katika saa za alasiri, baba mtakatifu atahudhuria sherehe ya pili katika eneo la Malmo na kukutana na ujumbe wa makanisa mbali mbali watakaohudhuria hafla hiyo.

Mwandishi: Tatu Karema

Mhariri: Yusuf Saumu