1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

uhusiano wa Ujerumani na Israel

11 Mei 2015

Ziara ya kansela Angela Merkel mjini Moscow ,miaka 50 ya uhusiano kati ya Ujerumani na Israel na uchaguzi wa baraza la mji wa Bremen ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/1FO0n
Kansela Merkel na rais Putin,wakizungumza na waandishi habari mjini MoscowPicha: Reuters

Ziara ya kansela Angela Merkel mjini Moscow kuadhimisha miaka 70 tangu vita vikuu vya pili vya dunia vilipomalizika,miaka 50 ya uhusiano kati ya Ujerumani na Israel na uchaguzi wa baraza la mji wa Bremen ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tunaanzia lakini Moscow alikofika ziarani kansela Angela Merkel,jana, siku moja baada ya gwaride kubwa kabisa la kijeshi lililofanywa katika uwanja mwekundu kuadhimisha miaka 70 tangu vita vikuu vya pili vya dunia vilipomalizika.Vladimir Putin aliitumia fursa hiyo kuuonyesha ulimwengu nguvu za kijeshi za nchi yake.Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linaandika:

"Katika nchi za magharibi kuna wenye wasi wasi ,wanaosema Putin haaminiki.Hofu zao zinaeleweka.Hata hivyo ziara imestahiki.Nchi za magharibi zinabidi zibainishe kwamba jumuia ya kujihami ya NATO haitoingia Ukraine.Badala yake Putin awaondowe wanajeshi wake kutoka eneo la Donbass na kuiachia pia raasi ya Crimea.Watu wanabidi waamini anachokisema."

Gazeti la kusini magharibi ya Ujerumani,"Stuttgarter Zeitung" linaiangalia pia ziara ya kansela Merkel mjini Moscow pamoja na mazungumzo aliyokuwa nayo pamoja na rais Vladimir Putin.Gazeti hilo linaandika:"Tija kubwa iliyopatikana baada ya kukomeshwa enzi za kikatili za wanazi miaka 70 iliyopita ni kuwa na Ulaya ya kidemokrasia iliyoungana na kupelekea Ujerumani kuungana upya.Hayo ndio madaraka makubwa kabisa yaliyotokana na kushindwa nguvu utawala wa zamani wa Ujerumani ya Hitler.Hakuna,hata Putin hawezi kuvuruga madaraka hayo.Labda sisi wenyewe."

Miaka 50 ya Uhisiano kati ya Ujerumani na Israel

Ujerumani na Israel zinasherehekea hivi sasa miaka 50 ya uhusiano wao.Gazeti la "Rheinpfalz" linamulika uhusiano huyo na kuandika:"Hasa pamoja na serikali mpya ya Israel,ya nne kuongozwa na waziri mkuu Benjamin Netanyahu mambo hayatakuwa rahisi kati ya Jerusalem na Berlin.Ujerumani inayoongozwa na serikali ya muungano wa vyama vikuu inahisi ina wajib wa kufuata sera sawia katika eneo la mashariki ya kati-lakini serikali ya muungano wa vyama vya kizalendo na kidini nchini Israel,inatanguliza zaidi masilahi yake tu,maovu yanakutikana kwa wengine.Kwamba mwaka 2008,kansela Angela Merkel ameutaja usalama wa Israel kuwa,kipa umbele cha siasa ya nje ya Ujerumani hayakuwa maneno matupu la sivyo Ujerumani isingendelea kuipatia kwa mfano nyambizi zenye zana za kinuklea.Lakini serikali ya Ujerumani haiungwi mkono na wananchi walio wengi katika siasa hiyo ya upande mmoja ya kuipendelea Israel.Badala ya kufumba macho,Ujerumani mbali na kuitakia ushindi Israel inabidi pia izishinikize nchi za kiarabu.

Wapiga kura hawakuonyesha hamu ya kuteremka vituoni

Wapiga kura katika mji wa jimbo dogo kabisa miongoni mwa majimbo 16 ya Ujerumani-Bremen,waliteremka vituoni jana kuwachagua wawakilishi wa baraza lao.Gazeti la Flensburger Tageblatt linaandika:"La muhimu zaidi kutokana na uchaguzi huo,sio chama kipi kimeshinda na kipi kimeshindwa..Kinachotisha ni idadi ya walioteremka vituoni-kila mkaazi mmoja kati ya wawili wa Bremen ndiye aliyetoa sauti yake.Na hali hii inatokea katika wakati ambapo Bremen inakabiliwa na changamoto za kila aina.Uchaguzi wa Bremen ni onyo kwa vyama vyote-mmomonyoko wa wapiga kura unawapokonya wanasiasa uwezo wa kuwajibika.Hilo linabidi liwe funzo hata nje ya mipaka ya Bremen.

Mwandishi:Hamibou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga