1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Macron na Merkel mjini Washington Magazetini

Oumilkheir Hamidou
24 Aprili 2018

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanamulika mazungumzo kati ya rais Donald Trump na rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, na baadaye na kansela Angela Merkel, na wito wa kupatiwa jeshi la Ujerumani vifaa vya kimamboleo.

https://p.dw.com/p/2wYPk
G20-Gipfel - Erste Arbeitssitzung
Picha: picture-alliance/dpa/AP/J. Macdougall

 

Wiki hii, Rais Donald Trump wa Marekani anawakaribisha viongozi wawili wa nchi  zinazotajwa kuwa injini ya  Umoja wa ulaya:  Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na kansela Angela Merkel wa Ujerumani. Wahariri wanahisi wizani hautokuwa sawa kati ya mazungumzo atakayokuwa nayo Trump na rais wa Ufarasa , kulinganisaha na yale atakayokuwa nayo ijumaa inayokuja pamoja na kansela Merkel. Mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine" anaandika: "Donald Trump amemkaribisha kwa madaha rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani rais huyo wa Marekani amempokea kwa hishma zote  za itifaki rais huyo wa Ufaransa na wakati huo huo kutoa ishara ulimwenguni: Ushirikano imara kati ya Barack Obama na Angela Merkel, nafasi yake inashikiliwa na mtandao kati ya Washington na Paris. Trump anamuangalia Macron kama kiongozi mwenzake wa magharibi anaeonyesha azma ya kutaka angalao kuuelewa mtindo wake. Angela  Merkel atakaefika ziarani mjini Washington ijumaa inayokuja anatoa picha kinyume na hiyo. Ataingia ikulu ya White House mtu anaweza kusema, kwa mlango wa nyuma. Kwa kansela wa Ujerumani la muhimu zaidi  lakini ni kuendeleza haraka iwezekanavyo mazungumzo pamoja na Trump baada ya kuapishwa kama kansela badala ya kusubiri matukio maalum ya kidiplomasia yatokee."

Mapokezi tofauti msimamo lakini ni mmoja

Gazeti la "Berliner Morgenpost" linasema hata ratiba ya ziara ya viongozi hao wawili ni tofauti. Gazeti linaendelea kuandika: "Sio tu kwamba mapokezi ya Emmanuel Macron hayatokuwa sawa na yale ya kansela Angela Merkel atakapofika ziarani mjini Washington. Muda wa ziara zao nao pia ni tofauti. Rais wa Ufaransa atabakia siku tatu wakati ambapo kansela Merkel anapanga kubakia siku moja tu. Sababu ya hali hiyo ni kwamba Macron amemkumbatia Trump tangu mwanzo. Na kansela kwa upande wake hakuficha tangu mwanzo pia kwamba hakubaliani na siasa inayofuatwa na Trump. Muhimu lakini ni kwamba katika mada muhimu mfano biashara huru au Urusi, Macron na Merkel wana msimamo mmoja."

Bundeswehr kupatiwa vifaa vya kisasa

Mada yetu ya mwisho magazetini inaturejesha Ujerumani ambako jeshi la shirikisho, Bundeswehr, litapatiwa vifaa vipya  vyenye thamani ya mamilioni ya Euro baada ya lawama kwamba vifaa vya jeshi hilo vimepitwa na wakati. Gazeti la "Rhein Zeitung" linaandika: "Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen amedhamiria kugharimia miradi 18 mikubwa mikubwa ya jeshi la shirikisho ili liweze kukidhi majukumu yake nchi za nje. Na hilo lilipaswa kufanyika tangu zamani. Jeshi la shirikisho linahitaji vifaa vya kimambo leo katika kutekeleza majukumu yake nchi za nje; naiwe upande wa usafiri wa angani, mawasiliano, upelelezi, ulinzi na kinga. Ni suala la mustakbali pia wa jeshi la shirikisho ambalo von der Leyen  na kwa masilahi yake mwenyewe hawezi kulikwepa."

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef