1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya rais Putin nchini Iran

Oummilkheir16 Oktoba 2007

Kiongozi wa Urusi aonya dhidi ya kutumiwa nchi moja ya eneo la bahari ya kaspian na nchi ya kigeni dhidi ya nchi nyengine ya eneo hilo

https://p.dw.com/p/C77l
Rais Putin na mwenyeji wake wa Iran Ahmadinedjad
Rais Putin na mwenyeji wake wa Iran AhmadinedjadPicha: AP

Rais Vladimir Putin wa Urusi amewasili Teheran leo asubuhi licha ya vitisho vya njama ya kutaka kumuuwa.Mazungumzo yake pamoja na viongozi wa Iran yatahusiana na mgogoro wa kinuklea kati ya jamhuri hiyo ya kiislam na nchi za magharibi.

Akuhutubia mkutano wa viongozi wa mataifa matano yanayopakana na bahari ya Kaspian,ambayo ni Azerbaidjan,Iran,Kazakhstan,Urusi na Turkmenistan,rais Vladimir Putin amesema “matumizi ya nguvu dhidi ya eneo hilo,si jambo linaloweza kukubalika.Amekumbusha msimamo wa Moscow wa kutanguliza mbele mazungumzo kama njia ya kusawazisha mivutano.

Rais Putin amesema:

“Tunataka mivutano yote ifumbuliwe kwa njia ya mazungumzo.Tunabidi tutilie maanani masilahi ya kila upande,tuheshimu milki ya kila nchi na tujiepushe na matumizi ya nguvu.Tusijaribu hata kufikiria juu ya matumizi ya nguvu katika eneo hili.Tunabidi kwa pamoja tukubaliane,”haitawezekana kamwe ardhi ya nchi moja inayopakana na bahari ya Kaspian kutumiwa kwa lengo la kuishambulia nchi nyengine.”

Onyo hilo linaonyesha kuilenga Azerbaidhan ambayo kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Urusi,huenda ikataka kuiruhusu Marekani itumie vituo vyake vya kijeshi.

Vladimir Putin,rais wa kwanza wa Urusi kuitembelea Iran tangu Stalin katika mwaka 1943,alilahikiwa katika uwanja wa ndege wa Teheran-Mehrabad na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Manoucher Mottaki.

Wairan wanaotuhumiwa na jumuia ya kimataifa kutaka kutengeneza silaha za kinuklea kwa kisingizio cha nuklea kwa ajili ya matumizi ya amani wanaiangalia ziara ya rais Putin kama fursa ya kujitoa katika hali ya upweke.

Kiongozi wa Urusi amepangiwa kuzungumza na rais Mahmoud Ahmadinedjad pamoja na kiongozi mkuu wa mapinduzi ya kiislam,Ayatollah Ali Khamenei.

Vladimir Putin, anaejiandaa kung’atuka madarakani,pengine mwakani,ameamua kuendelea na safari yake nchini Iran licha ya onyo kuna njama ya kutaka kumuuwa nchini Iran.


Viongozi wa jamhuri ya kiislam ya
Iran wamezisuta dhana hizo wakisema zimeenezwa na “maadui wa Teheran-“ ili kuvuruga uhusiano kati ya Urusi na Iran.

Vladimir Putin ambae nchi yake ina haki ya kura ya turufu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa anaangaliwa kama mhimili mkubwa kwa Iran,inayohofia vikwazo vikali zaidi vya kimataifa.

Vladimir Putin daima amekua akihoji mbinu za kutaka kuitia kishindo Iran haitasaidia kitu –badala yake anapigania watu wawe na subira na kuendeleza mazungumzo ili kuufumbua mzozo huo .