1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani zu Guttenberg nchini Afghanistan

Oumilkher Hamidou12 Novemba 2009

Hali ya kisiasa na usalama ni miongoni mwa mada zitakazozungumziwa wakati wa mazungumzo kati ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani zu Guttenberg na rais Karzai wa Afghanistan

https://p.dw.com/p/KUWC
Waziri wa ulinzi anazungumza na wanajeshi wa Ujerumani huko AfghanistanPicha: AP

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani,Karl-Theodor zu Guttenberg wa kutoka chama cha CSU amefika kwa ghafla ziarani nchini Afghanistan hii leo.Amepangiwa miongoni mwa mengineyo kuwa na mazungumzo pamoja na rais Hamid Karzai.Mara baada ya kukabidhiwa wadhifa huo,Zu Guttenberg alisema wazi kabisa haitokua miko kwake kuzungumzia juu ya uwezekanao wa kurejeshwa nyumbani wanajeshi wa Ujerumani toka Afghanistan.

Kwa kufanya ziara yake ya kwanza nchini Afghanistan,waziri mpya wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani,Karl-Theodor zu Guttenberg hakuikuta nchi iliyopowa:Kinyume kabisa.Afghanistan ndiyo kwanza imekamilisha mtihani uliosababishwa na uchaguzi uliokua na utata na ambao wadadisi wengi wanaamini haukukudhi kikamilifu maasharti ya kidemokrasi.Na rais mpya ni yule yule wa zamani,Hamid Karzai ambae anakabiliwa na kipindi kigumu,anaashiria mtaalam wa masuala ya kisiasa Haroun Mir:

"Wananchi wanaamini,rais hajachaguliwa kihalali.Waafghanistan wanahisi utaratibu mzima huu umeshindwa.Kwa mara nyengine tena jumuia ya kimataifa ndiyo inayobeba jukumu kama Hamid Karzai anaaminika."

Karzai lazma amekua akifikiria mnamo siku za hivi karibuni namna ya kuunda baraza lake la mawaziri,au pengine akijipasua kichwa.Kwasababu nchi za magharibi zimeshasema kinaga ubaga,zinapendelea kuwaona wenye ujuzi tuu serikalini.Zu Guttenberg kwa hivyo anafika katika wakati ambapo Afghanistan inajikuta ikizongwa na zahma za kisiasa.Lakini hata hali ya usalama inatazamiwa kugubika mazungumzo ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani nchini Afghanistan.Na hata hali katika eneo la kaskazini wanakokutikana wanajeshi wa Ujerumani itazungumziwa.Naibu kiongozi wa vikosi vya ISAF nchini Afghanistan-Hans-Erich Antoni alisema hivi karibuni kupitia kituo cha Radio cha ARD kwa eneo la kusini mwa Asia:

"Hali imezidi kuharibika katika miaka ya nyuma na mwaka huu pia katika eneo la Kunduz.Tumeshuhudia hujuma zilizoandaliwa kwa werevu mkubwa."

Karl-Theodor zu Guttenberg in Afghanistan Flash-Galerie
Waziri wa ulinzi Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: AP

Katika kipindi cha wiki mbili tangu akabidhiwe wadhifa wa waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani,Karl-Theodor zu Guttenberg ameshakurubia kutamka neno vita mara nyingi zaidi ya mtangulizi wake katika kipindi kizima cha miaka minne iliyopita.Katika mahojiano aliyokua nayo alifika hadi ya kuzungumzia juu ya hali inayolingana na vita nchini Afghanistan.Amesema anaelewa mwanajeshi anaposema kuna vita kule.

Jana tuu mwanajeshi mmoja wa Ujerumani alijeruhiwa vibaya sana katika mkoa wa Kundus.Kwa mujibu wa gavana wa eneo hilo,wanamgambo wamevurumisha kombora dhidi ya gari la jeshi la shirikisho Bundeswehr.Baadae risasi zikaanza kufyetuliwa kutoka kila upande kwa zaidi ya saa moja.

Kwa hivyo si jambo la kubahatisha kama waziri mpya wa ulinzi wa Ujerumani ameamua kufanya ziara yake ya kwanza nchini Afghanistan.

Mwandishi:Küstner,Kai.N Delhi(NDR)/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul-Rahman

: