1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Westerwelle mjini Benghazi

14 Juni 2011

... Uturuki na uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano kati ya walinzi wa mazingira na chama cha CDU, ndizo mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/11ZtR
Waziri wa mambo ya nchi za nje Gudio Westerwelle na mwenzake wa misaada ya maendeleo Dirk Niebel wakiteremka katika ndege ya jeshi la shirikisho huko BenghaziPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie lakini Benghazi ambapo mawaziri wawili wa serikali kuu ya Ujerumani na wote wawili ni wa kutoka chama cha kiliberali cha FDP waliitembelea kwa pamoja ngome hiyo ya waasi wa Libya. Gazeti la "Märkische Allgemeine la mjini Postdam linahisi:

Serikali kuu ya Ujerumani imekosolewa vya kutosha kwa kujizuwia kuunga mkono opereshini za kijeshi dhidi ya Libya. Guido Westerwelle na Dirk Niebel wasingekwenda Benghazi ingekuwa washirika hawakuamua kuingia kijeshi dhidi ya Gaddafi. Ziara hiyo huenda ikatoa sura ya kuwajibika kisiasa na kiuchumi, lakini pia inalenga kupunguza athari katika siasa ya nje. Hata hivyo, uamuzi wa serikali ya Kansela Angela Merkel haukuwa mbaya, hivyo mtu akitilia maanani yanayotokea Syria. Ukweli ni kwamba kwa miezi kadhaa sasa, jumuia ya kujihami ya NATO haijafanikiwa kumpigisha magoti Gaddafi. Na ikiwa watu watachukulia hoja zilizopelekea kuamuliwa opereshini za kijeshi dhidi ya Libya, basi hoja hizo hizo zingebidi pia zitumiwe dhidi ya Syria.

Wahlen in der Türkei Recep Tayyip Erdogan
Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mkewe AminePicha: picture-alliance/dpa


Mada ya pili magazetini inatufikisha Uturuki ambako chama cha kihafidhina cha kiislamu-AKP- kinachoongozwa na waziri mkuu, Racep Tayyeb Erdogan, kimeibuka na ushindi wa uchaguzi wa bunge. Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linaandika:

"Matokeo ya uchaguzi wa bunge la Uturuki sio tu ni ushindi wa kihostoria kwa waziri mkuu Erdogan na chama chake cha kidini na kihafidhina cha AKP. Ni ishara pia ya kukomaa kisiasa nchi hiyo ambayo miaka kumi iliyopita ilikumbwa na misuko suko na ambayo hakuna aliyeweza kukadiria inaelekea wapi. Ushindi bayana wa chama cha AKP na kukataa kwake kujiamulia mambo peke yake ni mambo yanayoweza kuijongeza mbele zaidi Uturuki.Yote hayo yanaweza kuigizwa na wenye kupigania demokrasia katika eneo la mashariki ya kati.

Winfried Kretschmann Ministerpräsident Baden-Württemberg Dossierbild 2/3
Waziri mkuu wa jimbo la Baden-Württemberg,Winfried Kretschmann wa chama cha walinzi wa mazingira-die GrünePicha: picture-alliance/dpa


Mada yetu ya mwisho inaturejesha hapa hapa Ujerumani ambako kuongezeka imani ya wapiga kura kwa chama cha walinzi wa mazaingira imegeuka sababu ya watu kuashirikia uwezekano wa kuundwa siku moja serikali ya muungano kati ya chama hicho na kile cha kihafidhina cha CDU.Gazeti la "Heilbronner Stimme" linaandika:

Ikiwa walinzi wa mazingira watataka kuendelea kuogelea katika bahari ya ushindi, basi watabidi waachane na baadhi ya misimamo yao shupavu. Winfried Kretschman ameonyesha mfano. Alikuwa na moyo wa kusifu mkondo mpya unaofuatwa na kansela Angela Merkel, badala ya kuufuja, kama ilivyo kawaida kisiasa. Amefanya hivyo akitambua fika kwamba mvutano mkubwa uliokuwepo kati ya CDU na walinzi wa mazingira umeshamalizika na uwezekano wa kuundwa muungano wa CDU/CSU na Chama cha kijani umechomoza. Hayo ndio mwanasiasa huyo mwerevu aliyokuwa akiyataka miaka mitano iliyopita katika jimbo lake la Baden Württenberg. Mkuu wa kundi la wabunge wa CDU wakati ule, Stefan Mapus, hakutaka watu wajongeleane. Halikuwa kosa pekee lakini lilikuwa kubwa kuliko yote.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Miraji Othman