1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yahimizwa kulinda haki za binadamu

11 Julai 2018

Ripoti mpya ya shirika la kimataifa la utetezi wa haki za binadamu la Amnesty International imeonya kuhusu visa vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu, wakati Zimbabwe ikielekea kufanya uchaguzi mkuu Julai 30.

https://p.dw.com/p/31Gv5
Kampeni za uchaguzi Zimbabwe
Picha: Getty Images/AFP/Z. Auntony

Kulingana na ripoti hiyo, visa hivyo ni pamoja na mauaji ya watu wengi, wakosoaji waliotoroshwa kwa nguvu pamoja na kuzuiwa maandamano ya amani.

Kaimu mkurugenzi wa Amnesty International, Kusini mwa Afrika, Muleya Mwananyanda, amesema, ni wakati sasa kwa taifa hilo kuachana na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, uliodumu nchini humo kwa muda mrefu. Zimbabwe inafanya uchaguzi wake wa kwanza bila ya rais wake wa zamani Robert Mugabe kushiriki. Chini ya utawala wa rais Robert Mugabe, nyakati za uchaguzi ziligubikwa kwa kiasi kikubwa na mauaji, watu kutoroshwa kwa nguvu na wengine kukamatwa.

Ripoti hiyo iliyobeba kichwa cha habari kinachosema "Kuachana na ya nyuma:Ilani ya haki za binaadamu kwa vyama vya siasa na wagombea nchini Zimbabwe", inatoa mapendekezo saba kwa wagombea na vyama vya siasa vinavyogombea kwenye uchaguzi huo wa Zimbabwe, Julai 30. Roselina Muzerengi ni mratibu wa kampeni wa shirika hilo nchini Zimbabwe. "Kwa kuwa Mugabe amekwishaondoka, kuna fursa muhimu kwa Zimbabwe kuanza upya, lakini pia nafasi ya kuachana na historia ya nyuma pamoja na kuhakikisha kwamba haki za binaadamu zinaheshimiwa kikamilifu katika mazingira ya chaguzi na baada ya chaguzi." 

Enzi mpya bila Mugabe?

Chaguzi zilizopita zilikuwa na sifa ya ukiukwaji wa haki za binaadamu, na Amnesty International na waangalizi wa chaguzi wamekuwa wakihifadhi kumbukumbu ya baadhi ya visa hivyo. Zaidi ya watu 200 waliuawa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2008, kutokana na vitendo vya kikatili dhidi ya wafuasi wa upinzani. Tangu mwaka 2000, Amnesty imerekodi visa vya matumizi makubwa ya nguvu za kijeshi, lakini sasa ikiwa na imani kwamba chini ya uongozi mpya vitaondoshwa, kama Muzerengi anavyosema. "Maafisa wa juu wa jeshi la polisi, ZRP  wameshindwa kukemea vitendo vya ukiukwaji wa haki za binaadamu vilivyofanywa na maafisa wa polisi, hususan vipigo kwa raia, mateso na vitendo vingine vibaya walivyofanyiwa wakiwa mahabusu ama kwenye vituo vya polisi. Mabadiliko ya uongozi wa jeshi hilo ni lazima yabadilishe historia hiyo ya ukiukwaji."

Moja ya alama moja kubwa ambayo utawala wa Mugabe umeiacha ni hatua kali na za kikatili dhidi ya wanaharakati wa haki za binaadamu. Mwandishi wa habari na muungaji mkono wa masuala ya demokrasia Itai Dzamara alitoroshwa kwa lazima tangu Machi 9, 2015, baada ya kumtaka Mugabe kujiuzulu kutokana na kukiuka haki za binaadamu na kushindwa kuimarisha hali ya uchumi.

Wanaharakati wengine waliotekwa, kupotea ama kuuawa kutokana na sababu za kisiasa ni pamoja na Paul Chizuze, Tonderai Ndira, Patrick Nabanyama, Cain Nkala na Gilbert Moyo. Wanaharakati wengine kama Felix Mzava na Gabriel Shumba walitekwa ama kuteswa na baadae kuachiwa huru.

Zimbabwe itafanya uchaguzi wa kitaifa Julai 30 mwaka huu wa rais, wabunge na serikali za mitaa. Utakuwa ni uchaguzi wa kwanza bila ya Mugabe tangu Zimbabwe ilipopata uhuru wake mwaka 1980 kutoka kwa Waingereza. Mugabe alijiuzulu Novemba 21 mwaka 2017, baada ya kuwa madarakani kwa miaka 37.

Mwandishi: Lilian Mtono/Amnesty International

Mhariri: Saumu Yusuf