1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimesalia siku 12 kabla ya uchaguzi mkuu wa rais nchini Marekani.

Kalyango/ Kitojo, Sekione22 Oktoba 2008

Zimesalia siku 12 kabla ya uchaguzi wa rais nchini Marekani ambapo Barack Obama anaongoza katika kura ya maoni nchini humo.

https://p.dw.com/p/FeqD
Seneta Hillary Clinton (Kushoto) na mgombea wa chama cha Democratic seneta Barack Obama wakiwapungia mashabiki wao walipofanya mkutano wa pamoja wa kampeni mjini Orlando Florida nchini Marekani hivi karibuni.Picha: AP


Barack Obama anaendelea kuongoza katika maoni ya wapiga kura hadi sasa ikiwa ni siku 12 zimesalia kabla ya uchaguzi wa rais nchini Marekani , lakini wataalamu wanasema kuwa mbio hizo za kuingia Ikulu ya Marekani hazijafikia ukingoni ikiwa kuna uwezekano wa John McCain mgombea wa chama cha Republican kupunguza mwanya huo.


Wachunguzi pamoja na wanaochunguza maoni ya wapiga kura wanakubaliana hata hivyo kuwa Obama kutoka chama cha Democratic anaelekea kushinda, wakati mgombea mwenzake wa chama cha Republican John McCain akikabiliwa na uwezekano wa kazi ngumu ya kutoka hapo alipo.

Katika wakati huu nafasi ya kupata ushindi wa kishindo kwa seneta John McCain ni ndogo sana, amesema Peter Brown , mkurugenzi msaidizi wa taasisi ya kukusanya maoni ya wapiga kura ya chuo kikuu cha Quinnipiac.

Anaburura mkia katika uchunguzi mwingi wa maoni kutoka kiwango cha kati hadi cha juu kabisa. Kurejea katika kiwango cha juu cha maoni na kuweza kushinda , litakuwa jambo la ajabu kwa sasa.

Akiwa na matumaini ya kuzuwia kurejea kwa McCain na kupata ushindi wakati akiwa na alama za chini kabisa , Obama ameonya dhidi ya kujisahau wakati akihutubia mikutano yake ya kampeni, akiwataka wale wanaomuunga mkono kuchukua nafasi ya mapema ya sheria za kupiga kura katika jimbo la Florida na majimbo mengine muhimu.

Uchunguzi unaonyesha kuwa mmoja kati ya kila wapiga kura watano bado hawajaamua nani wa kumpigia kura ama wako tayari kubadilisha maamuzi yao. Kambi ya McCain inaweka matumaini yao kwa wapiga kura hawa.

Inawezekana kumpa nafasi kubwa Obama kushinda kwasababu amekuwa mbele katika maoni yote ya wapiga kura kwa muda wa wiki kadha zilizopita sasa, amesema Frank Newport, mkurugenzi mtendaji wa kundi linalochunguza maoni ya wapiga kura la Gallup.

Lakini hali inakaribiana sana chini ya matokeo kama haya ambapo huwezi kuondoa uwezekano wa McCain kushinda, Newport ameliambia gazeti la Chicago Tribune.

Wakati baadhi ya uchunguzi wa maoni unaonyesha Obama akiwa amepanua mwanya kwa alama zaidi ya kumi, mgombea huyo wa chama cha Democratic anazidisha mashambulizi yake dhidi ya mapendekezo ya kiuchumi ya Mrepublican John McCain , wakati huo huo pia akionyesha tofauti za masuala ya usalama wa taifa katika siku hizi za mwisho za kampeni.

Kuidhinishwa kwake mwishoni mwa wiki na mwanachama mwandamizi wa chama cha Republican Colin Powell ,waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Marekani chini ya utawala wa rais George W. Bush , kunampa Obama nafasi ya kufungua njia kuelekea kushambulia zaidi eneo la masuala ya mambo ya kigeni. Mada hiyo inaonekana kuwa ni eneo dhaifu kwake dhidi ya McCain, lakini uungwaji wake mkono na Powell umepunguza kile kinachoonekana kuwa hilo ni suala linalompa nguvu McCain.

Kinachotoa nguvu zaidi kwa kambi ya Obama hata hivyo ni kuungwa mkono jana na mhafidhina mwandamizi Ken Adelman ambaye amefanyakazi chini ya marais Ronald Regan, Gerald Ford na George W. Bush , na ambaye amekuwa miongoni mwa viongozi wa ngazi ya juu wa chama cha Republican hivi karibuni kubadilisha kambi na kumuidhinisha Obama kuwa rais.

Ken Adelman , mhafidhina mamboleo akiwa na mahusiano ya karibu na makamu wa rais Dick Cheney na waziri wa zamani wa ulinzi Donald Rumsfeld, aliliambia jarida la New Yorker kuwa ameamua kuachana na kambi ya McCain kutokana na jinsi alivyolishughulikia suala la mzozo wa fedha na uteuzi wake wa gavana wa Alaska Sarah Palin kuwa mgomea wake mwenza.


►◄