1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zu Guttenberg ajiuzulu

1 Machi 2011

Taarifa za hivi punde (saa 5.15 asubuhi kwa saa za Ulaya ya Kati) zinasema kuwa zu Guttenberg amejiuzulu wadhifa wake wa uwaziri wa ulinzi leo hii.

https://p.dw.com/p/10R7V
Karl-Theodor zu Guttenberg
Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: dapd

Kwa mujibu wa vyanzo kutoka mashirika ya habari nchini Ujerumani, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg, ambaye amekuwa akikabiliwa na kashfa ya kutumia marejeo ya watu wengine kwenye shahada yake ya uzamifu bila ya kuwatambulisha, amejiuzulu wadhifa wake leo hii (Jumanne, 01.03.2011).

Gazeti maarufu la Bild limesema kwamba tayari zu Guttenberg, ambaye mwishoni mwa mwezi uliopita alivuliwa jina la udaktari na Chuo Kikuu cha Bayreuth cha Ujerumani, ameshawasilisha uamuzi wake huo kwa Rais Christian Wullf na Kansela Angela Merkel.

Zu Guttenberg mwenye miaka 39, ambaye vyombo vya habari vimempachika majina ya "Baron Cut-And-Paste" na "Zu Googleberg", ni miongoni mwa mawaziri wenye umashuhuri mkubwa kwenye serikali ya Merkel na kujiuzulu kwake kutakuwa na mshtuko mkubwa kwa Kansela Merkel.