1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma ajiuzulu

Lilian Mtono
15 Februari 2018

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameamua kujiuzulu mara moja kufuatia kuongezeka kwa shinikizo kutoka kwa chama chake, kinachotawala nchini humo cha African National Congress, ANC.

https://p.dw.com/p/2sia4
Südafrika | Präsident Zuma tritt zurück
Picha: Reuters/S. Sibeko

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma hatimaye ameamua kujiuzulu jana Jumatano, baada ya kushinikizwa na chama chake, kinachotawala nchini humo cha African National Congress, ANC, kufuatia miaka 9 ya kukabiliwa na kashfa za rushwa, kuporomoka kwa uchumi na kushuka kwa umaarufu.

Zuma alikilalamikia chama cha ANC kwa kumtaka aondoke madarakani, ikiwa ni pamoja na kumtishia kumuondoa kupitia kura ya bunge ya kutokuwa na imani naye, iliyopangwa kupigwa hii leo, Alhamisi.

Rais Zuma amesema ataheshimu maagizo ya chama chake cha ANC kwa kujiuzulu wadhifa wake, baada ya wiki kadhaa za uvumi kuhusu mustakabali wake. Alinukuliwa akisema “nimeamua kujiuzulu kutokana na kura ya kutokuwa na Imani iliyokuwa imepangwa kupigwa siku ya Alhamisi".

Katika hotuba ya kitaifa aliyoitoa kwa dakika 30 kupitia tekevisheni, Zuma alisema, hatua hiyo inaanza kutekelezwa mara moja. 

Zuma amekuwa katika mvutano wa kimadaraka na mfanyabiashara bilionea wa zamani na makamu wa rais, Cyril Ramaphosa ambaye sasa anakuwa rais wa mpito. Ramaphosa aliyeshinda nafasi ya kukiongoza chama cha ANC, baada ya kuchaguliwa mwezi Disemba, atapigiwa kura na wabunge nchini humo kuwa rais mpya ama leo au kesho Ijumaa. 

Mwandishi: Lilian Mtono/afpe/dw
Mhariri: