1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii

Josephat Nyiro Charo5 Februari 2010

Kesi ya rais Bashir kuchunguzwa upya huku kundi la al Qaeda likijiimarisha Afrika

https://p.dw.com/p/LtSU

Gazeti la gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung ambalo liliripoti juu ya uamuzi wa kitengo cha rufaa cha mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC mjini The Hague kuwataka majaji wa mahakama hiyo wachunguze upya uamuzi wa kumuondolea mashtaka ya mauji ya halaiki rais wa Sudan Omar Hassan al Bashir. Muongoza mashtaka mkuu wa mahakama hiyo Luis Moreno Ocampo alitaka rais wa Sudan ashtakiwe kwa mauaji katika jimbo la Darfur, lakini mpango wake haukufaulu.

Gazeti la Frankfurter Allgemine Zeitung limeripoti kuwa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch limeupongeza uamuzi mpya wa kitengo cha rufaa cha mahakama ya ICC. Nalo gazeti la Tageszeitung kuhusu uamuzi huo limesema umezusha mjadala katika ngazi ya kimataifa kwa nini kesi ya Bashir imechipuka tena wakati huu uchaguzi ukikaribia kufanyika mwezi Aprili nchini Sudan. Rais Bashir atagombea na kushinda na hivyo kuhakikisha kumalizika kwa muda wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kushika doria katika jimbo la Darfur na Sudan Kusini.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung pia limeripoti kuhusu kundi la al Shaabab kuapa kuendeleza vita vya jihad katika eneo la pembe ya Afrika na Afrika Mashariki. Gazeti hilo limesema kiongozi wa kundi hilo, Sheikh Dahir Arweys, ambaye ni miongoni mwa watu wanaosakwa sana ulimwenguni, alifanya mkutano na waandishi wa habari Jumanne iliyopita katika kitongoji cha Bar Ubah kinachopakana na soko kubwa la Bakara ambalo ni uwanja wa vita mjini Mogadishu, Somalia. Kiongozi mwingine wa kundi la al Shabaab aliyehudhuria mkutano huo amenukuliwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung akisema wanataka kuendeleza vita vyao vya jihad pamoja na vita vya kimataifa vya mtandao wa al Qaeda na kiongozi wao Osama bin Laden.

"Kundi la al Qaeda lapata wafuasi barani Afrika," limeandika gazeti la Financial Times Deutschland. Kwa mara ya kwanza wanamgambo wa kiislamu nchini Somalia wametangaza kufanya kazi pamoja na mtandao wa kimataifa wa al Qaeda chini ya uongozi wa Osama bin Laden na kuanzisha taifa la kiislamu katika eneo la pembe ya Afrika. Gazeti limeripoti kuwa wanamgambo wa al Qaeda wanawazuilia mateka sita wa rehani raia wa Ulaya kaskazini magharibi mwa Afrika na wametishia kuwaua. Kundi hilo limewataka waislamu wa kaskazini mwa Nigeria wapigane vita vitakatifu dhidi ya wakristo wa eneo hilo. Mhariri anasema kundi la al Qaeda linazidi kuimarika barani Afrika.

Umoja wa Ulaya unaendeleza juhudi zake kupambana na uharamia katika pwani ya Somalia. Hayo yameripotiwa na gazeti la Neue Zürcher Zeitung. Mhariri amesema kwa mujibu wa kamanda mkuu wa operesheni ya umoja huo katika pwani hiyo, juhudi zaidi za kulinda usalama zinahitajika. Gazeti limemnukulu kamanda wa Uingereza, Hudson, akisema kazi kubwa ya operesheni hiyo iliyopewa jina la Atalanta, inayolenga kulinda usafirishaji wa vyakula vya shirika la chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, na mahitaji ya wanajeshi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika walioko nchini Somalia, AMISOM, imetekelezwa vyema.

Kamanda Hudson amesema haitoshi kukabiliana na maharamia wa kisomali upande wa baharini tu, bali kunahitajika suluhisho la kisiasa litakalowezesha kufanya harakati katika nchi kavu ndani ya Somalia. Kwa mantiki hiyo, Umoja wa Ulaya utafadhili mafunzo kwa vikosi maalum vya Wasomali huko nchini Uganda mwezi Mei mwaka huu yatakayofanywa na jeshi la Uganda, ambalo tayari lina wanajeshi wake nchini Somalia. Wapiganaji 2,000 watapewa mafunzo katika makundi mawili kwa lengo la kuiimarisha serikali ya mpito ya Somalia inayokabiliwa na shinikizo kutoka kwa wanamgambo wa kiislamu na wababe wengine wa kivita.

Gazeti la Tageszeitung lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema, "Afrika inatakiwa kuwachukua walionusurika katika tetemeko la ardhi nchini Haiti." Kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika uliomalizika Jumanne iliyopita mjini Addis Ababa, Ethiopia, rais wa Senegal, Abdoulaye Wade, alipendekeza nchi za Afrika ziwachukue raia wa Haiti walioponea chupuchupu tetemeko la ardhi la Januari 12 mwaka huu. Ametaka kuanzishwe mipango ya kuwachukua watoto mayatima na nchi za Afrika ziwape haki ya uraia Wahaiti watakaorejea.

Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping, raia wa Gabon, amenukuliwa na gazeti la Tageszeitung akisema pendekezo la rais Wade litajadiliwa na viongozi wa umoja huo ili Wahaiti wanaotaka kurejea Afrika waruhusiwe kufanya hivyo.

"Hotuba iliyobadilisha kila kitu", ndivyo lilivyoandika gazeti la Der Spiegel kuhusu hotuba ya aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, Frederick Willem de Klerk, miaka 20 iliyopita. Katika hotuba yake aliyoitoa mnamo Februari 2 mwaka 1990 alifuta marufuku dhidi ya vyama vya upinzani, kuamuru kuachiwa huru bila masharti yoyote wafunga wote wa kisiasa, akiwemo Nelson Mandela, na kukomesha ubaguzi wa rangi nchini humo uliodumua kwa takriban miaka 50. Gazeti linasema de Klerk hajajuta kutoa hotuba hiyo ambayo ilikuwa kama mlipuko wa bomu katika nchi za kigeni.

"Mtoto wa siri wa rais Jacob Zuma," ndivyo lilivyoandika gazeti la Tageszeitung. Gazeti limesema kuna mzozo unatokota kati ya michezo na siasa kwani rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma inasemekana amezaa mtoto wake wa 20 na msichana wa rafiki yake Irvin Khoza ambaye ni mwenyekiti wa kamati inayoandaa michuano ya kandanda kuwania kombe la dunia itakayofanyika nchini humo mwezi Juni mwaka huu. Mtoto huyo amekuwa mada inayozungumziwa kila siku Afrika Kusini na watu wengi wanajiuliza rais Zuma ana watoto wangapi.

Chama tawala ANC kimesema hilo ni swala la kibinafsi la rais Zuma na kwamba hajavunja sheria yoyote. Kimesema uhusino wake na Sonono Khoza si wakuabisha kwani wote ni watu wazima. Vijana wa ANC wamesema ripoti zinazotolewa na vyombo vya habari zinamvunjia heshima rais Zuma, lakini wanasiasa wengi ndani ya chama hicho wanamuona rais akitoa mfano mbaya kwa vijana wa Afrika Kusini.

Mwandishi: Charo, Josephat/ Pressedatenbank

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed