1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Magharibi hatarini kuwa kitovu cha uhalifu na ugaidi.

14 Januari 2008

Kukamatwa nchini Guinea Bissau kwa wahutumiwa wa Al Qaeda waliowauwa watalii wanne wa Kifaransa nchini Mauritania kunaonyesha jinsi Afrika Magharibi ilivyokuja kuwa shimo la maficho ya wahalifu na magaidi.

https://p.dw.com/p/CpC3
Jengo la bunge Guinea Bissau mojawapo ya nchi ambapo mizizi ya uhalifu na pengine hata ugaidi imeanza kujikita.Picha: AP

Antonio Mazziteli wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Madawa ya Kulevya na Uhalifu ameyahimiza mashirika ya usalama duniani kuweka nadhari zaidi kwa eneo hilo la Afrika Magharibi ambalo amesema linageuka kuwa mahala palipokithiri maovu ya uhalifu na uwezekano wa kuwa maskani ya ugaidi.

Polisi nchini Guinea Bissau hivi karibuni imewakamata raia wawili wa Mauritania wanaotuhuimiwa kwa mauaji ya watalii wanne wa Kifaransa waliopigwa risasi kwenye mkesha wa X’masi wakati wakiwa kwenye mandari pembezoni mwa barabara kusini mashariki mwa Mauritania.

Wamauritania hao wawili ambao polisi ya Bissau imesema wamekiri kwamba wamo kwenye kundi la Al Qaeda wamerudishwa Mauritania pamoja na watu wengine watatu wanaotuhumiwa kushirikiana nao ambao pia ni Wamauritania.Polisi wamesema wametishia mashambulizi zaidi dhidi ya mataifa ya magharibi.

Mauaji hayo ya Mauritania yaliosababisha kufutwa kwa mashindano ya mbio za magari ya mwaka 2008 ya Lisbon hadi Dakar yalizusha tahadhari katika Nyanja za usalama na kuzusha uwezekano wa kuwepo matawi ya magaidi wa Kiislamu yanayoendesha harakati zake kusini zaidi kuliko ilivyokuwa kabla huko kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.

Mazziteli ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba mambo hayo yamethibitisha kile walichokuwa wakikihofia sana kwamba uhalifu wa aina yoyote ile unaweza kujitokeza katika nchi kama vile Guinea Bissau au mahala kwengine Afrika Magharibi.

Polisi ya Bissau ambayo tayari imekuwa ikipambana na uvamizi wa makundi ya biashara ya madawa ya kulevya ya Amerika ya Kusini ambayo yanaitumia nchi hiyo ndogo ya Afrika Magharibi kusafirisha madawa hayo hadi barani Ulaya imeshtuka kujuwa kwamba mmojawapo wa Mmauaritania waliyemkamata aliwahi kuishi Guinea Bissau kwa miaka miwili na alikuwa anaweza kuzungumza lugha ya wenyeji ya creole.

Mazziteli ambaye anaongoza ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu kwa Afrika ya Magharibi na Afrika ya Kati anasema Afrika Magharibi imekuwa shimo la maficho ambapo mtu yoyote yule anaesakwa anaweza kwenda na kuendesha harakati zake au kujificha wawe ni magaidi au wahalifu wa aina nyengine.

Ameongeza kusema hiyo ni pepo ya wahalifu na kutaja ishara za mapambano ya kutumia silaha ambapo uasi wa wapiganaji wa jangwani wa kabila la Tuareg kaskazini mwa Niger na Mali ambayo yalianzishwa kwa misingi ya kisiasa kwa kweli ni eneo la mapambano kwa ajili ya usafirishaji wa madawa ya kulevya na silaha.

Hofu ya mashambulizi zaidi dhidi ya wageni katika jangwa la Sahara na Sahel imeongezeka baada ya Wataliana watatu kuporwa na watu wenye silaha mapema mwezi wa Januari karibu na Timbuktu mji wa biashara wa hekaya katika Sahara ambacho ni kituo mashuhuri kwa watalii nchini Mali.

Yakiwa na wasi wasi juu ya tishio la ugaidi na usafirishaji wa madawa ya kulevya na wahamiaji kwa njia ya magendo mashirika ya ulinzi na usalama ya Ulaya na Marekani yamekuwa yakizidi kuelekeza nadhari yao katika eneo hilo la Afrika lenye idadi kubwa ya Waislamu.

Makachero kutoka nchi za Ulaya hivi sasa wanaziangalia kwa makini bandari za Afrika Magharibi kama vile Dakar,Conakry, Bissau na Nouadhibou kukamata mizigo inayoweza kuwa ya madawa ya kulevya au wahamiaji wasio halali ambao wanaweza kudukizwa baharini na manowari za Ulaya.

Kutokana na eneo hilo kubwa kubwa mno na kutokuwepo kwa ulinzi kwenye sehemu kubwa ya fukwe zake,jangwa na vichaka linaendelea kubakia kuwa mahala muafaka kwa maficho ya magaidi na wahalifu.

Hali hiyo inaashiria kwamba kunahitajika kuchukuliwa kwa hatua zaidi kuimarisha na kuboresha ushirikiano wa usalama na ulinzi Afrika Magharibi.