1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Baghdadi ajitokeza baada ya miaka mitano

Amina Mjahid Mhariri: Daniel Gakuba
30 Aprili 2019

Kiongozi wa juu wa kundi la Dola la Kiislamu, Abu Bakr al-Baghdadi amejitokeza katika vidio ya propaganda akikiri kushindwa kwa kundi hilo nchini Syria, lakini akitishia mashambulizi zaidi ya kulipiza kisasi.

https://p.dw.com/p/3HhJA
Irak Abu Bakr al-Baghdadi
Picha: picture-alliance/AP Photo/Al-Furqan

Abu Bakr al-Baghdadi; mtu anayetafutwa duniani kwa udi na uvumba, alionekana mara ya mwisho mjini Mosul mwaka 2014, akitangaza kuanzishwa kwa kundi aliloliita Dola la Kiislamu  - kundi linaloogopewa na lillilokuwa limeyakamata maeneo makubwa ya Iraq na Syria.

Katika mkanda huo wa vidio uliotolewa na chombo cha habari cha IS, Al Furqan, mtu huyo aliyetajwa kuwa Al-Baghdadi alizungumzia mapigano yaliyodumu miezi kadhaa mjini Baghouz, Syria,na kumalizika mwezi Machi. 

Al-Baghdadi alionekana katika vidio hiyo akizungumza na wanaume watatu ambao nyuso zao zilikuwa zimefunikwa, akisema "mapigano mjini Baghouz yamemalizika," huku akiangazia maeneo mengi ambayo kundi lake lilishindwa katika mapigano mjini Mosul, Iraq, na Sirte, Libya.

Kiongozi huyo wa juu wa kundi hilo la kigaidi aliongeza kuwa bado kundi hilo,halijayaachia maneo hayo kabisa kabisa na kutishia kufanya mashambulizi zaidi ya kulipiza kisasi.

Utata kuhusu al-Baghdadi

Irak Abu Bakr al-Baghdadi
Abubakar al-Baghdadi kwenye vidio ya mwaka 2014 akitangaza kuanzishwa kwa Dola la Kiislamu, IS.Picha: imago/United Archives International

Haijawa wazi ni lini au wapi vidio hiyo ya dakika 14 ilipochukuliwa, lakini al-Baghdadialiyeonekana akiwa na ndevu nyekundu na kijivu, akiwa ameketi chini huku kukiwa na bunduki pembeni mwake, aliyataja na kuyasifia mashambulizi ya hivi karibuni, kwa mfano yale ya Sri Lanka yaliyosababisha vifo vya  watu 253 huku zaidi ya 500 wakijeruhiwa.

Kiongozi huyo wa kundi la kigaidi alisema hayo yalikuwa "mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa ndugu zao wanaouwawa mjini Baghouz" na kushindwa kuudhibiti mji huo ambao ni ngome yao muhimu na ya mwisho nchini Syria. 

Alisema mashambulizi yao dhidi mataifa ya Magharibi ni sehemu ya mapigano yao ya muda mrefu na kwamba IS ingeliendelea kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa wanachama wake wanaouawawa.

Hata hivyo Marekani iliyotoa kitita cha dola milioni 25 kwa yeyote atakayetoa taarifa za aliko al-Baghdadi, ilisema inaendelea kuchunguza ukweli wa vidio hiyo, huku ikiapa kuendelea na vita vya kuliangamiza kundi zima la IS.

Vyanzo: AFP, Reuters