1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yaitaka Tanzania ifanye uchunguzi madai ya mauaji

20 Novemba 2020

Shirika la kimataifa la Amnesty International limesema serikali ya Tanzania inapaswa kufanya uchunguzi wa haraka, wa kina na ulio huru kuhusu madai ya mauaji dhidi ya wanasiasa wa upinzani na wafuasi.

https://p.dw.com/p/3lcqv
Tansania Sansibar | Wahlen | Bevölkerung geht Wählen
Picha: AFP/Getty Images

Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International tawi la Mashariki na Kusini mwa Afrika, Deprose Muchena, amesema kumekuwa na ongezeko la ukiukaji wa haki za binaadamu baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwezi uliopita. Kwa mujibu wa mawakili wanaovitetea vyama vya upinzani, karibu viongozi 77 wa upinzani na wafuasi wao walikamatwa bila kufikishwa mahakamani tangu siku ya uchaguzi.

Amnesty International imesema kuukosoa uchaguzi ulivyofanyika sio uhalifu na kwa hivyo wote waliokamatwa bila kufunguliwa mashitaka wanapaswa kuachiwa huru mara moja na bila masharti yoyote. Muchena amesema viongozi wa Tanzania wanapaswa kuzilinda haki za Watanzania za uhuru wa kijielezea, kujumuika na kukusanyika kwa amani, kuliko kuzikiuka.

ACT- Wazalendo: Seif Sharif amekamatwa

Oktoba 31, kamishna wa polisi wa Zanzibar, Mohamed Haji Hassan, alithibitisha kwamba polisi inawashikilia watu 33, akiwemo naibu katibu mkuu wa chama cha upinzani ACT-Wazalendo, Nassor Mazrui. Mawakili wanaowawakilisha watuhumiwa wameripoti kuwa wengi wa watu waliokamatwa hawajafunguliwa rasmi mashtaka au hakuna ushahidi uliowasilishwa kuhusu madai ya ugaidi dhidi yao ambayo yanaonekana kuwa ya uwongo.

Bildkombo Tansania Wahlen | Präsident John Magufuli und Tundu Lissu
Rais Magufuli na mpinzani wake wa karibu Tundu Lissu

Aidha, huko huko visiwani Zanzibar, watu wengine 18 waliachiwa kutoka katika vizuizi na kutupwa kwenye maeneo mbalimbali majira ya asubuhi siku ya Novemba 13. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya waliokuwa wanashikiliwa na kuthibitishwa na mawakili wao.

Mawakili wa vyama vya upinzani wameliambia shirika hilo kwamba takriban watu 22 wameuawa na vikosi vya usalama kati ya tarehe ya uchaguzi na Novemba 11. Wanasiasa wa upinzani na mashirika ya kiraia wamevishutumu vikosi vya serikali kwa kutumia nguvu kupita kiasi, ikiwemo risasi za moto, kwa lengo la kuwatawanya waandamanaji. Viongozi lazima waanzishe uchunguzi kuhusu mwenendo wa vikosi vya usalama.

Hatimaye Lissu aondoka Tanzania

Katika matukio mawili, Amnesty International iliwahoji ndugu za watu waliouawa, ambapo walikiri kwamba waathirika walikuwa na majeraha ya risasi. Aidha, wamesema ndugu zao waliouawa, hawakuwa wafuasi wa chama chochote kile cha kisiasa. Katika matukio mengine manne, shirika hilo limethibitisha kupitia mahojiano na watu walioshuhudia kwamba vikosi vya serikali vilihusika na mauaji. Kuna uwezekano kwamba idadi ya visa ikawa kubwa zaidi.

Kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binaadamu na mawakili wanaoviwakilisha vyama vya siasa, tangu kipindi cha uchaguzi zaidi ya watu 300 wamekamatwa nchini Tanzania, wengi wao wakiwa wameachiwa kwa dhamana na wengine bila kufunguliwa mashtaka. Miongoni mwa waliokamatwa na kuachiwa huru ni aliyekuwa mgombea wa urais wa chama cha upinzani Chadema, Tundu Lissu, mgombea urais wa ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar, Seif Sharif Hamad na viongozi wengine wa upinzani,  Zitto Kabwe, Freeman Mbowe, Godbless Lema, Lazaro Nyalandu, Isaya Mwita, Boniface Jacob, Nassor Mazrui na Ayoub Bakari.