1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asasi za kiraia Tanzania zataka katiba mpya

Hawa Bihoga27 Septemba 2017

Zaidi ya asasi 10 za kiraia nchini Tanzania zimetangaza kuwa hazitaacha mchakato wa kudai katiba mpya, licha ya rais wa John Magufuli kutangaza wazi kuwa suala la katiba mpya sio kipaumbele katika serikali yake.

https://p.dw.com/p/2kndC
Severine Niwemugizi Bischof Dar es Salaam
Picha: DW/W.Boniphace

Asasi za kiraia nchini Tanzania zimetangaza hadharani kuwa hazitaacha mchakato wa upatikanaji wa kudai katiba mpya, licha ya rais wa nchi hiyo john Magufuli kutangaza wazi kuwa kuwa suala la katiba mpya sio kipaumbele katika serikali yake. Hayo yamewekwa wazi katika mkutano wao wa pamoja uliolenga kuendeleza vuguvugu la kudai katiba mpya na kuongeza kuwa huu ni wakati sahihi kwani mchakato huo uliligharimu taifa rasilimali watu, muda pamoja na fedha.

Mjadala huo ulihusisha zaidi ya asasi kumi za kiraia kutoka Tanzania bara na Zanzibar pamoja na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali.

Asasi hizo zimetoka na kauli moja kuwa, wakati huu ni sahihi kudai katiba mpya kutokana na kwamba hakuna mihemko ya kisiasa ambayo itawafanya Watanzania kupeleka mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya kwa kuangalia viongozi wao wa kisiasa wapo katika mrengo gani.

Wameongeza, hawawezi kuchoka kuihamasisha serikali kuendeleza mchakato wa kupata katiba mpya licha ya kuwa ni haki ya kimsingi ya raia, lakini mchakato huo uliligharimu taifa rasilimali fedha, muda pamoja na watu.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli
Rais wa Tanzania John Pombe MagufuliPicha: DW/E. Boniface

Onesmo ngurumo ambaye ni mwanasheria pamoja na wakili Anna Henga kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wamesema kuwa kwa umoja wa asasi hizo, kwa pamoja watatumia njia ya mijadala ya amani katika kupata katiba mpya.

Shinikizo la kutaka katiba laongezeka

Matamko mbalimbali yanayotolewa na asasi za kiraia yakidai katiba mpya yameshuhudiwa katika kipindi cha awamu hii ya tano ya uongozi, kadhalika asasi hizo zimeweza kukutana moja kwa moja na wabunge wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ili kuhakikisha swala hilo linazungumzwa bungeni kwa lengo la kuwakumbusha viongozi kuhusiana na muendelezo wa kupata katiba mpya.

Haya yote yalimfanya rais John Magufuli kuweka wazi kuwa, suala la katiba mpya sio kipaumbele cha serikali ya awamu ya tano. Kwa hili askofu Severine Niwemugizi kutoka Ngara anasema kuwa, dira ya nchi ikiwa imara ni rahisi kupata maendeleo thabiti yanayotoka kwa wananchi wenyewe.

Hata hivyo wawakilishi kutoka wizara ya katiba na sheria walioiwakilisha serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania katika mjadala huo wa wazi wa kudai katiba mpya, wameahidi kuchukua yale yote ambayo asasi za kiraia wameyafikia na kuyafikisha katika serikali kuu na huko maamuzi zaidi yatafikiwa.

Hatua tano za kisheria katika kupata katiba mpya zilifanikiwa bila kizuizi, ikiwemo, kuundwa kwa tume ya kuandaa katiba iliyoongozwa na jaji Warioba, na baadaye, tume kukusanya maoni ya wananchi, kisha rasimu ya kwanza iliyopelekwa katika baraza ambapo rasimu ya pili ya katiba ilifanikiwa na ilipelekwa katika bunge la katiba na hatimaye katiba inayopendekezwa lakini mchakato umekwamia hapo. Endapo rais ataliweka katika kipaumbele chake hatua itakayofuata ni katiba inayopendekezwa kupigiwa kura na wananchi.

Mwandishi: Hawa Bihoga

Mhariri: Josephat Charo