1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad atembelea Ghouta Mashariki

Sudi Mnette
19 Machi 2018

Bomu lililoripuka katika jengo moja la ghorofa nne katika mji wa Afrin kaskazini mashariki mwa Syria limesababisha vifo vya watu 11 wakiwemo raia saba na wapiganaji wanne.

https://p.dw.com/p/2uZVY
Syrien Assad besucht Truppen in Ost-Ghuta
Rais Bashar al Assad alipotembelea eneo tete la Ghouta Mashariki nchini SyriaPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/Syrian Presidency

Ikiwa ni kipindi kifupi tu baada ya rais wa taifa hilo kutembelea eneo lililozingirwa la Ghouta Mashariki kuwapongeza wanajeshi kwa kukidhibiti kiunga hicho.

Bomu hilo ambalo linaelezwa kutegwa na magaidi, liliripuka wakati wapiganaji wa kundi lijiitalo Jeshi Huru la Syria, FSA, wakifanya msako mkali baada ya kufanikiwa kuwaondoa wanamgambo wa Kikurdi wa kundi la YPG na kutangaza udhibiti kamili, kufuatia mapambano makali ya takribani wiki nane yakisaidiwa na jeshi la Uturuki.

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Uturuki, Anadolu, limesema bomu hilo lilisababisha shimo la kina cha mita nne kwenda chini na pia kuyavunja vibaya majengo mengine na magari yalikuwa karibu na eneo hilo. Msemaji wa wapiganaji wa Kituruki wenye kuungwa mkono na waasi wa Syria wa kundi la FSA alisema walifanikiwa kuingia Afrin jioni ya Jumapili pasipo upinzani wowote.

Wapiganaji wagoma kuondoka 

Lakini Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria lilisema baadhi ya wapiganaji wa YPG walikataa kuondoka katika mji huo, ingawa jeshi la Uturuki lilikuwa katika udhibiti. Uturuki inasema wapiganaji wa YPG ni mwendelezo wa kundi la wanamgambo la PKK ambalo linafanya mashambulizi ndani ya Uturuki, na taifa hilo limeapa kuliangamiza kwa kile wanachokiita wapo katika uwanda wa kigaidi, kwa yale maeneo yanayodhibitiwa na YPG, eneo la mpakani mwa Uturuki na Syria.

Watu 6,000 waondoka Ghouta Mashariki

Syrien Ost Ghouta Evakuierung Verwundete
Baadhi ya wakazi majeruhi wa Gohuta MasharikiPicha: Reuters/Sana

Katika hatua nyingine Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kuwa zaidi ya watu 6,000 wameondoka mashariki mwa mji uliozingirwa wa Ghouta, ulio karibu na mji mkuu, Damascus. Hilo linakoea baada ya Rais Bashir al Assad kufanya ziara katika eneo hilo linalopiganiwa, kuwapongeza wanajeshi kwa kufanikisha hatua ya kuwaonda waasi kwenye ngome yao hiyo ya mwisho karibu na makao makuu ya nchi.

Televisheni ya serikali ya Syria imeonesha picha ya Rais Assad akiwa amezungukwa na wanajeshi akiwa amevalia suti katika eneo ambalo, hata hivyo, halikuweza kutambulishwa. Waasi nchini Syria wamekuwa wakikidhibiti kiunga cha Ghouta Mashariki tangu 2012, lakini mashambulizi ya jeshi la serikali katika kipindi cha mwezi uliopita yamefanikiwa kulirejesha eneo hilo kwa takribani asilimia 80.

Katika vidio ambayo imetolewa na ofisi yake, Assad amesikika akisema "Wakazi wa Damascus wanawashukuru na labda watavieleza vizazi vyao kwa namna gani walivyoweza kuunusuru mju wao mkuu."

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria lenye makao yake makuu mjini London, Uingereza, limesema operesheni ya vita vya angani na ile ya ardhini katika eneo la Ghouta Mashariki imesababisha vifo vya raia zaidi ya 1,400 tangu kuanzishwa kwake Februari 18. Jumuiya ya kimataifa imekasirishwa sana na jinsi operesheni hiyo ilivyofanyika. Katika kipindi hicho pia, kiasi cha raia 50, wakiwemo watoto 10 wameuwawa mjini Damascus kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na waasi.

Mwandishi: Sudi Mnette AFP/RTR
Mhariri: Mohammed Khelef