1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Aung San Suu Kyi afunguliwa mashtaka baada ya mapinduzi

Saumu Mwasimba
3 Februari 2021

Polisi nchini Myanmar imemfungulia mashitaka kiongozi wa kiraia Aung San Suu Kyi aliyepinduliwa mwanzoni mwa wiki hii kwa kumkuta na simu chungu nzima za upepo nyumbani kwake.

https://p.dw.com/p/3opfH
Myanmar Aung San Suu kyi
Picha: Thet Aung/AFP/Getty Images

Kwanza kinachoelezwa ni kwamba Suu Kyi alikamatwa Jumatatu pamoja na wanasiasa wengine waandamizi baada ya jeshi kuchukua madaraka kwa nguvu siku hiyo hiyo ambayo bunge jipya lililochaguliwa lilitarajiwa kufunguliwa rasmi.

Maafisa wa chama chake cha NLD wanasema mwanasiasa huyo hajaondolewa nyumbani kwake ambako amewekwa kifungoni.

Polisi imemfungulia Suu Kyi mashtaka ya kumiliki simu chungu nzima za upepo, ambazo kawaida hutumiwa na jeshi la polisi.

Simu hizo zilikutwa nyumbani kwake bila ya kusajiliwa. Na mashtaka hayo yanaonesha adhabu yake ni kifungo cha hadi miaka miwili jela.

Nyaraka za mashtaka zinaonesha simu hizo za upepo hazikusajiliwa na zilikuwa ni kwa ajili ya kutumiwa na walinzi wa Suu Kyi. Sakata hili linaipa polisi uhalali wa kisheria kumshikilia hadi Februari 15.

Chama cha Suu Kyi chathibitisha mashtaka dhidi yake 

Chama cha NLD kimethibitisha juu ya mashtaka hayo kupitia msemaji wake, Kyi Toe, aliyetowa ufafanuzi kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Weltspiegel 02.02.2021 | Myanmar Putsch | Militär
Picha: AFP/Getty Images

Rais aliyepinduliwa na jeshi, Win Myint, naye ameshtakiwa kwa ukiukaji wa sheria ya kusimamia majanga, ameeleza wakili wa chama hicho.

Polisi na maafisa wa mahakama katika mji mkuu Naypitaw hawakupatikana kutoa tamko.

Taarifa iliyotolewa leo kwa niaba ya watendaji wakuu wa chama cha Suu Kyi imesema maafisa wa jeshi walianza kuvamia ofisi mbali mbali za chama chao katika jimbo la Mandalay na majimbo mengine na mikoa na kuchukua nyaraka pamoja na kompyuta za mkononi.

Msemaji wa chama cha NLD, Aung Kyi Nyunt, ameeleza kwamba makabati yalivunjwa katika ofisi zao chungu nzima, uvamizi alioutaja kuwa sawa na mapinduzi yenyewe ya kijeshi, ni kitendo kisichokuwa na uhalali na kutaka kikomeshwa.

''Kitendo cha jeshi kuchukua madaraka ya nchi sio kizuri baada ya nchi kuendeshwa chini ya mfumo wa demokrasia, kuwa na amani, mazingira bora ikiwa ni pamoja na kuwa na makubaliano ya kitaifa ya kuacha vita. Nchi pia ina taratibu nzuri za kuzia maambukizo ya Covid-19. Haya mapinduzi sio kitu kizuri kabisa kwa wananchi wote.'' amesema Nyunt.

NLD yaitisha maandamano kulaani mapinduzi 

Myanmar Militärputsch | Militär in Yangon
Picha: AFP/Getty Images

Chama cha NLD cha Suu Kyi kimeitisha maandamano ya kupinga mapinduzi yaliyofanywa na jeshi na jana usiku shangwe zilisikika baada ya umati kujitokeza katika mji wa Yangon ambao ni mji mkubwa kabisa wa Myanmar kujiunga na maandamano yaliyoitishwa na wanaharakati.

Lakini hiyo hiyo jana wafuasi wasiopungua elfu tatu walijitokeza kuliunga mkono jeshi.

Mapinduzi yaliyofanyika yanaonekana kama mtihani kwa jumuiya ya kimataifa. Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 7 tajiri kiviwanda duniani, G7, wametowa taarifa ya pamoja leo wakitaka Suu Kyi na wenzake waachiwe huru na amri ya hali ya dharura iondolewe sambamba na kurudishwa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.