1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lalaani ukandamizaji nchini Syria

4 Agosti 2011

Baada ya siku kadhaa za kushindwa kufikia uamuzi hatimaye baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limetoa tamko la kulaani hatua ambazo serikali ya Syria inachukua kukabiliana na waandamanaji wanaoipinga serikali hiyo.

https://p.dw.com/p/12BE4
Rais wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Hardeep Singh PuriPicha: picture alliance/dpa

Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito kwa wale wote wanaohusika na vitendo hivyo wawajibike. Wanachama 14 wa baraza hilo waliunga mkono taarifa hiyo ambayo inasema kuwa serikali ya Syria imetumia nguvu dhidi ya raia. Urusi ambayo imekuwa na shaka na hatua ya baraza hilo, nayo pia imeunga mkono taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imetolewa huku mamia ya vifaru na wanajeshi wa Syria wakiendelea kubakia katikati ya mji wa Hama na mji wa Deir Ezzor. Inakadiriwa kuwa kiasi ya watu 141 wameuawa tokea mwishoni mwa wiki.

Akisoma taarifa rasmi balozi wa India katika umoja wa Mataifa ambaye ndiye rais wa baraza hilo kwa sasa, Hardeep Singh Puri, amesema Umoja wa Mataifa unalaani vifo vya raia na kutaka wale wote wanaouhusika na ghasia hizo kuwajibika.

"Baraza la usalama linaelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali nchini Syria na linasikitishwa sana na vifo vya mamia ya watu. Baraza la usalama linaalani kuendelea kwa ukiukaji wa haki za binadamu na matumizi ya nguvu dhidi ya raia yanayofanywa na serikali ya Syria."

Mara baada ya taarifa hiyo Lebanon ilisema haiungi mkono taarifa hiyo na kwamba inasimama bega kwa bega na serikali ya Syria. Balozi wake kwenye umoja wa mataifa alinukuliwa akisema hakupiga kura.

Hakuna makubaliano ya azimio

Hata hivyo baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilishindwa kukubaliana juu ya azimio. Mataifa ya magharibi yalikuwa na matumaini ya kupitishwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa kuhusiana na hali inayoendelea huko Syria, lakini yamepingwa na China na Urusi ambazo zina kura ya turufu.

Witali Tschurkin
Vitaly Churkin, balozi wa Urusi katika Umoja wa MataifaPicha: AP

Nchi hizo mbili zina hofu kuwa kupitishwa kwa azimio dhidi ya Syria kunaweza kufungua njia ya kuingilia kijeshi mzozo. Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, amesema, "Tunasikitishwa na vurugu pamoja na kuendelea kwa mzozo huu na tunadhani kwamba katika mazingira haya, baraza la usalama linaweza na ni lazima litoe ishara endelevu ambayo ni kutumia siasa kuumaliza mzozo huo. Tumeshirika kikamilifu na tuna nia nzuri katika majadiliano kwenye baraza la usalama."

Kwa upande wake naibu balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa, Miguel Berger, amesema taarifa hiyo ni ishara tosha kuwa wanachama wanaguswa na kile kinachoendelea Syria.

"Nadhani ni wazi hii ni hatua moja mbele ya kwamba wanachama wote wa baraza hili wameshiriki katika majadiliano makali. Hilo pekee linatoa ishara kuwa kuna wasiwasi mkubwa katika baraza la usalama kuhusiana na kudorora kwa hali nchini Syria."

Mwandishi: Aboubakar Liongo/AFP/REUTERS/ZPR

Mhariri: Josephat Charo