1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua ya wazi ya CPJ kwa rais wa Tanzania Magufuli

Sekione Kitojo
13 Agosti 2019

Kamati ya kimataifa ya kulinda waandishi habari CPJ imeandika barua ya wazi kwa rais wa Tanzania John Magufuli kutaka serikali kufuta mashitaka dhidi ya mwandishi habari Erick Kabendera na maelezo kuhusu Azory Gwanda.

https://p.dw.com/p/3Nouk
Tansania Daressalam Präsident John Magufuli
Picha: DW/E. Boniphace

Barua hiyo ya  wazi kwa  rais  wa Tanzania  John Pombe  Magufuli imeeleza  kwamba  ni mwezi  uliopita  tu  wakati  wa mkutano wa kutetea uhuru wa  vyombo vya  habari mjini  London, waziri  wa mambo  ya  kigeni  wa  Tanzania  Palamagamba  Kabudi amethibitisha  kwamba  serikali  yake  inataka "kuwezesha  uandishi habari  wa  kiuchunguzi"  na "kuhakikisha  kwamba  waandishi  habari wanalindwa  dhidi  ya  hatua  zozote, kushitakiwa  ama  kukamatwa." Kumruhusu  Kabendera  kurejea  katika  kazi  yake, na  kulichukulia kwa  dhati  suala  la kupotea  kwa  Gwanda, litakuwa  hatua  muhimu kuelekea  kutimiza  ahadi  hizi.

Tansania Daressalam Präsident John Magufuli
Rais wa Tanzania John Joseph Pombe MagufuliPicha: DW/E. Boniphace

Kabendera  alichukuliwa  kwa  nguvu  kutoka  nyumbani  kwake  Julai 29, 2019, na  kunyimwa uwezekano  wa  kuwakilishwa  na  wakili kwa  zaidi ya kipindi cha masaa 24. Polisi  awali  walidai  kwamba wanachunguza  uraia  wa  Kabendera. Hata  hivyo, siku chache baadaye  baada  ya  kukamatwa  kwake waendesha  mashitaka walibadilisha  njia  na  kumshitaki kwa  uhalifu  wa  kiuchumi, mashitaka  ambayo  hawezi  kupata  dhamana.

Kuhojiwa Kabendera

Alihamishwa  katika  vituo  mbali  mbali  vya polisi katika  wakati  wa kuhojiwa. Utaratibu  wa  kukamatwa  kwake  na  kushikiliwa kunaonesha kulipizwa  kisasi  ambako  kunaelekea  kutaka kunyamazisha  hatua  yake ya uandishi wa kukosoa, ikiwa ni pamoja na migawanyiko ndani ya chama tawala.

Gwanda  pia alifanya kazi  kama  mwandishi  wa  kujitegemea, katika eneo  la  mkoa  wa  pwani. Alipotea  Novemba  21, 2017, akiwa pamoja  na  watu  ambao hawajajulikana wanaoaminika  kuwa watu wa  usalama wa  taifa, barua  hiyo  ya  CPJ imeandika.

LOGO CPJ
Nembo ya shirika la CPJ linalotetea waandishi habari

Katika  mahojiano  mwezi  Julai  mwaka  huu, waziri wa  mambo  ya kigeni  wa  Tanzania  Kabudi alidai kuwa  Gewanda  alikuwa  mmoja wa  watu  wengi ambao, kwa  maelezo  yake "walipotea  na  kufariki" katika  wilaya  ya  Rufiji, licha  ya  kuwa  Kabudi  baadaye  alisema matamshi  yake yalichukuliwa  vibaya, na  hafahamu  hatima  ya Gwanda. Matamshi  yake shirika  la  CPJ linasema  yanaleta ukakasi na  kuonesha  umuhimu wa  haja  ya  uchunguzi  w kile  kilichomkuta mwandishi  huyo.

Shirika  la  CPJ pia  limesema  linakaribisha  fursa ya kukutana  na wawakilishi  wa  serikali  kujadili wasi  wasi  huu. DW imejaribu kuwatafuta wasemaji wa serikali kuzungumzia barua hii  lakini hatukufanikiwa.