1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aahidi chanjo milioni 100 za COVID-19

Lilian Mtono
9 Desemba 2020

Rais mteule wa Marekani Joe Biden ameuainisha mpango wake wa kupambana na janga la virusi vya corona katika siku zake 100 za mwanzo za urais huku akiahidi kwamba serikali yake itatoa chanjo milioni 100 kote nchini humo.

https://p.dw.com/p/3mSIS
USA Wilmington, Delaware | Joe Biden, Vorstellung Team | Joe Biden
Picha: Mark Makela/Getty Images

Kwenye kikao kilichofanyika Wilmington, Delaware, Biden amesema ataliomba bunge kuruhusu ufadhili kamili wa mchakato wa kusambaza chanjo kote nchini humo na kuongeza kuwa katika siku zake 100 za mwanzo za urais wake, kwa pamoja wataweza kubadilisha mkondo wa ugonjwa huo nchini humo, lakini pia hali ya Waamerika.

Biden ambaye pia aliitambulisha timu yake ya afya ya umma, amesema kuwarejesha watoto shuleni, ni suala ambalo serikali yake italipatia kipaumbele.

"Jambo la tatu ambalo nitaomba katika siku 100, litakuwa ni kipaumbele cha kitaifa cha kuwarudisha watoto wetu shuleni. Na ikiwa bunge litatoa ufadhili tunahitaji kuwalinda wanafunzi, waalimu na wafanyakazi... ikiwa majimbo na miji pia itaweka hatua madhubuti za afya ya umma na sisi sote tukazifuata, basi timu yangu itahakikisha kuona kwamba shule zetu nyingi zinaweza kuwa zimefunguliwa hadi mwishoni mwa siku zangu 100 za kwanza." alisema Biden.

Takriban watu 283,000 wamekufa nchini humo kutokana na corona na mamilioni wakipoteza ajira. Mamlaka ya dawa na chakula ya Marekani ilichapisha waraka jana ambao haukuwa na lolote jipya kuhusiana na usalama na uthabiti wa chanjo ya Pfizer Inc's ambayo huenda ikapata idhini ya dharura mwezi huu kutumika Marekani.

Washington | Nancy Pelosi & Chuck Schumer PK
Spika wa bunge Nancy Pelosi amesema majadiliano ya vyama viwili ndio pekee yataleta suluhu.Picha: Michael Brochstein/Zuma/picture alliance

Katika hatua nyingine, ikulu ya White House imezindua pendekezo la mpango wa kuchochea uchumi wa dola bilioni 916, katika jaribio la mwisho la kuvuka kihunzi cha miezi kadhaa juu ya mpango mpya wa kunusuru uchumi wa taifa hilo ulioathiriwa na janga hilo la corona kabla rais Donald Trump hajaondoka madarakani Januari mwakani.

Waziri wa fedha Steven Mnuchin ametangaza mpango huo ambao amesema unahusisha fedha za serikali kuu na za mitaa lakini pia ulinzi wa biashara, shule na vyuo vikuu. Masuala hayo ndio yalikuwa makuu kwenye majadiliano kati ya wabunge wa Democratic na Republican.

Mnuchin amewasilisha mapendekezo hayo kwa spika wa bunge Nancy Pelosi.

Ujerumani, hali bado ni tete.

Nchini Ujerumani, majimbo mawili ya Saxony na Bavaria hapo jana yalikaribia kuanzisha vizuizi vikali zaidi, wakati maafisa wakionya kwamba kuendelea kuongezeka kwa maambukizi kunaweza kusababisha hospitali kuelemewa.

Waziri mkuu wa jimbo la Saxony Michael alitangaza kuzifunga shule kuanzia Jumatatu ijayo hadi January 10, wakati hali ikizidi kuwa mbaya kwenye jimbo hilo, huku mwenzake wa Bavaria Markus Soeder akiwaomba wabunge kuunga mkono uamuzi wa serikali kutangaza hali ya dharura na kuanzisha vizuizi vikali zaidi.

Soma Zaidi: Ujerumani: Chanjo ya COVID-19 kuanza Januari

Taasisi ya kudhibiti magonjwa ya Robert Koch imeripoti visa vipya 14,054 vya corona katika kipindi cha msaa 24 yaliyopita na kufanya jumla ya maambukizi kufikia takriban milioni 1.2.

Wakati jana Uingereza ikianza kutoa chanjo, wataalamu wa magonjwa ya virusi wanakiri kuwa ni mwanzo mzuri wa kukabiliana na janga hilo, ingawa bado kuna mengi yanayohitaji majibu.

Mashirika: DW/APE/AFPE