1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aunga mkono mazungumzo kati ya Maduro na upinzani

9 Juni 2022

Rais wa Marekani amezungumza kwa njia ya simu na kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan Guaido na kueleza uungaji mkono wa Marekani wa kuanzishwa upya mazungumzo kati ya serikali ya Rais Nicolas Maduro na upinzani.

https://p.dw.com/p/4CRPS
USA US-Präsident Joe Biden
Picha: Michael Reynolds/MediaPunch/IMAGO

Hayo yanatokea wakati mkutano wa viongozi wa mabara ya Amerika unaofanyika mjini Los Angeles ukigubikwa na utata baada ya Rais wa Mexico Andres Manuel Lopez na viongozi wengine wa nchi za Amerika ya kati na kusini kuusia mkutano huo.

Akizungumza kutoka ndege aina ya Air Force One akiwa njiani kuelekea mkutano wa kilele wa viongozi wa mabara ya Amerika unaofanyika mjini Los Angeles Marekani, Rais Joe Biden amesisitiza kuwa Washington iko tayari "kulegeza vikwazo" dhidi ya Venezuela kwa kutegemea matokeo ya mazungumzo kati ya serikali na upinzani.

Soma pia: Maduro asema Venezuela haitasalimu kutokana na vitisho

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ambaye hakualikwa kwenye mkutano huo wa viongozi wa mabara ya Amerika, hata hivyo bado hajaweka tarehe maalum ya kuanza tena kwa mazungumzo hayo. Marekani inamtambua Guaido kama rais wa mpito baada ya kukataa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2018 yaliyomrudisha tena Maduro mamlakani ikidai uchaguzi huo ulikumbwa na dosari nyingi.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa kisoshalisti bado amesalia madarakani katika nchi hiyo mwanachama wa jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani Opec, licha ya vikwazo vikali vya Marekani.

Washauri wakuu wa rais wasema mkutano huo haujapoteza hadhi licha ya kususiwa

Mexikos Präsident Lopez Obrador will nicht am Amerika-Gipfel teilnehmen
Rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador Picha: Luis Barron/Eyepix Group/NurPhoto/picture alliance

Utawala wa Biden umekataa kuialika serikali ya Maduro, serikali ya kikomunisti ya Cuba na serikali ya mrengo wa kushoto ya Nicaragua kwenye mkutano huo wa viongozi wa mabara ya Amerika kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni rekodi zao mbaya juu ya haki za binadamu na kubinya demokrasia.

Kutengwa kwa nchi hizo kulimshurutisha Rais wa Mexico Andres Manuel Lopez pamoja na viongozi wengine wa nchi za Amerika ya kati na kusini kuususia mkutano huo wa mjini Los Angeles, na hivyo basi kudhoofisha ajenda ya Biden.

Biden azuru Uingereza

Washauri wakuu wa Rais Biden hata hivyo wamesema licha ya mkutano huo kususiwa na viongozi kutoka Mexico, Bolivia, Grenada na Hondura, bado haujapoteza hadhi au mwelekeo wake.

Soma pia:Biden aomboleza mauaji ya kutumia bunduki huko Texas

Vyanzo vya upinzani vimesema Biden na Guaido walizungumza kwa takriban dakika 15. Katika taarifa, Ikulu ya White House imesema Biden alionyesha kuunga mkono mazungumzo kama njia bora kuelekea kurudi kwa amani, uchaguzi huru na wa haki nchini Venezuela.

Marekani imesema pia iko tayari kulegeza vikwazo dhidi ya Venezuela iwapo tu kutakuwepo na maendeleo ya maana katika mazungumzo kati ya serikali ya Rais Nicolas Maduro na upinzani, na katika wiki za hivi karibuni Washington imeonekana kulainisha sera zake kuelekea Venezuela katika hatua za makusudi za kuwezesha mazungumzo mapya.

Maduro alijiondoa kwenye meza ya mazungumzo na upinzani, katika mazungumzo yaliyofanyika katika mji mkuu wa Mexico City mnamo mwezi Oktoba. Hata hivyo, alibadili msimamo wake kufuatia ziara ya ujumbe wa ngazi ya juu wa Marekani mjini Caracas na baadaye kuashiria utayari wake kurudi tena katika meza ya mazungumzo.